Na, Beatrice Maganga
Mgomo wa madaktari unaendelea kwa siku ya 76 sasa huku wakisisitiza kwamba ni lazima matakwa yao yatimizwe. Wengi wamekuwa wakijua kwamba wanachotaka madaktari ni nyongeza ya mishahara ya asilimia 300. Lakini je, mkataba wa malipo uliotiwa saini mwaka 2013 unahusu nini hasa?
Katika nakala ya kurasa ishirini na saba iliyotiwa saini na aliyekuwa Katibu wa KMPDU, Sultani Matendechero, aliyekuwa Mwenyekiti, Victor Ng’ani na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Mark Bor na kutiwa muhuri na Tume ya Kuratibu Mishahara ya Wafanyakazi wa Umma, SRC, masuala kadhaa yaliafikiwa katika mkataba huo.
Kipengele cha tano cha mkataba huo kilihusu kuboreshwa kwa mazingira ya kufanyia kazi ambapo kila daktari alistahili kufanya kazi saa arubaini kila wiki na iwapo atazidisha, basi anastahili kulipwa marupurupu. Kila ofisi ya daktari ilistahili kuwa na tarakilishi, huduma za mtandao na televisheni.
Kila hospitali ambayo daktari angehitajika kuhudumu ilistahili kuwa na vifaa vyote vya matibabu ambavyo dakrari angehitajika ili kufanikisha utendakazi wake. Katika mkataba huo, iliafikiwa kwamba iwapo mahitahi hayo yasingetimizwa basi daktari alikuwa na haki ya kulalama.
Vilevile iliafikiwa kwamba serikali ihakikishe madaktari walioajiriwa katika hospitali za umma wanaendelea kuhudumu huku madaktari wapya 1, 200 wakiajiriwa kila mwaka kuanzia mwaka 2013 ambapo mkataba huo ulitiwa saini ili kuongeza idadi ya madaktari nchini.
Katika suala nyeti la mishahara lililonakiliwa katika kipengele cha nne cha mkataba huo ni kwamba kila daktari alistahili kulipwa kwa kuzingatia viwango vilivyowekwa katika kila gredi kuanzia gredi ya L ambayo ni ya kiwango cha chini kinachowajumuisha wanafunzi wanaohudumu katika hospitali mbalimbali za umma hadi gredi ya T ambayo ni ya juu zaidi.
Hata hivyo yalikuwapo masharti kwamba mabadiliko yoyote yaliyokuwa yakipendekezwa kuhusu viwango vya mishahara na kubadilishwa kwa gredi za kazi yangetekelezwa baada ya Tume ya Kuratibu Mishahara, SRC kutathmini viwango vya mishahara vinavyostahili kulipwa kila mfanyakazi kwa kuzingatia kazi anayofanya.
Tathmini hiyo ingefanyika kwa kipindi cha miaka miwili kumaanisha kwamba SRC ingebainisha viwango hivyo kufikia mwaka 2016. Hata hivyo SRC ilipotangaza kukamilisha tathmini hiyo, madaktari wakiongozwa na Katibu wao wa sasa, Ouma Olunga na Mwenyekiti, Samuel Oroko wakalalamika pakubwa kwamba SRC haikubainisha viwango wanavyostahili kulipwa. Kutokana na hilo, wakasisitiza kwamba ni lazima mapendekezo ya viwango wanavyotaka yatimizwe.
Kulingana na mapendekezo yao, daktari wa kiwango cha L anastahili kulipwa mshahara wa shilingi laki moja, elfu ishirini na nne mia saba sabini kutoka shilingi elfu arubaini na tano, mia nane na themanini. Wa kiwango cha juu zaidi anastahili kulipwa mshahara wa shilingi takriban laki tano kutoka laki tatu mbali na marupurupu.
Ikumbukwe serikali iliahidi kuwapa nyongeza ya asilimia 40 kiwango ambacho madaktari wanasema ni cha chini muno. Serikali inasema hitaji la kuwapa nyongeza ya asilimia 300 haliwezi kuafikiwa sasa kutokana na matatizo ya kifedha. Mvurutano huu utadumu hadi lini? Hapa Radio Maisha tutaendelea kuangazia.