Serikali, mashirika ya Umoja wa Mataifa UN na yale ya kutetea haki za kibinadamu yametakiwa kuchukua hatua madhubuti kuendeleza na kuwekeza katika usaidizi wa kisaikolojia kwa watu walioathiriwa na mizozo ya kivita.
Shirika la Human Rights Watch linasema idadi kubwa ya watu walioathirika kiakili mwaka huu inatokana na mizozo ya kijamii na vita pamoja na hali ngumu ya kimaisha kufuatia ukame na baa la njaa.
Kaulimbiu ya maadhimisho ya tarehe 10 Oktoba, Siku ya Kimataifa ya Afya ya Akili mwaka 2022, ni "Kuboresha afya ya akili na kuifanya kipaumbele kwa ustawi wa kimataifa. "
Katika maadhimisho hayo, serikali zimeshauriwa kushirikiana na washikadau mbalimbali kuwekeza katika kuboresha huduma za afya ya akili.
Kwa mujibu wa Shirika la Human Rights Watch, vurugu inayohusiana na migogoro inaweza kusababisha mfadhaiko wa kisaikolojia, hofu, wasiwasi, na mfadhaiko wa baada ya kiwewe.
Utafiti katika nchi za Afghanistan, Cameroon, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Ethiopia, Gaza, Iraq, Sudan Kusini, na Syria umeonesha kwamba watu, hasa wanawake na watu wenye ulemavu, mara nyingi hutatizika kupata huduma za afya ya akili.
Asilimia 22 ya watu wanaoishi katika maeneo yaliyoathiriwa na mapigano wana matatizo ya afya ya akili, kulinganisha na asilimia 13 katika idadi ya watu duniani.
Utafiti wa WHO unaonesha kwamba matatizo ya afya ya akili huchangia hadi asilimia 11 ya sababu za hatari zinazohusiana na visa vya watu kujiua.
- Call for understanding: What it's like to live with epilepsy
- Clinical officers: What government must do for us to return to work
- Private doctors to join strike in 7 days as church, Raila speak out
- Pharmacists want chemists selling prescription drugs to minors punished
Keep Reading
Nchini Kenya, hali ngumu ya maisha, ukame na athari za janga la COVID-19 ni mambo ambayo yametajwa kuchangia ongezeko la watu wanaoathirika kiakili.
Barani Afrika, takriban watu 11 kwa kila 100, 000 kwa mwaka, hufariki dunia kwa kujiua katika Ukanda wa Afrika, juu ya wastani wa kimataifa wa tisa kwa kila watu 100,000.
Hali hii inatokana kwa kiasi fulani na hatua zisizotosheleza za kushughulikia na kuzuia mambo hatarishi, kama vile hali ya afya ya akili ambayo kwa sasa inaathiri watu milioni 116, kutoka milioni 53 mwaka 1990.
Kutokana na uwekezaji mdogo katika huduma za afya ya akili, Afrika ina daktari mmoja wa magonjwa ya akili kwa kila wakazi 500,000, ambayo ni mara 100 chini ya mapendekezo ya Shirika la Afya Duniani WHO.
Zaidi ya hayo, wahudumu wa afya ya akili wako wengi katika maeneo ya mijini, kuliko vituo vya afya katika maeneo ya mashinani ambavyo vina wagonjwa wengi na madaktari wachache.
Kulingana na takwimu, mtu mmoja kati ya kila watu wanne wanaotembelea vituo vya afya wana matatizo ya afya ya akili nchini Kenya.
Inaamaanisha kwamba Wakenya milioni 11. 5 wanaugua magonjwa ya akili ambapo wanaume ndio wanaoathirika zaidi.
Kulingana na utafiti, wanaume huathirika zaidi na matatizo ya afya ya akili kwa sababu ni vigumu kwao kuzungumza ama kutafuta usaidizi kwa watu wengine kuhusu mambo yanayowasumbua.
Kwa wanawake, hali ni tofauti kwa sababu wao ni wepesi wa kuzungumza na kutafuta suluhu kuhusu changamoto zinazowakumba.
Wajibu wa binafsi wa kujilinda ndio lengo kuu la vita dhidi ya matatizo ya afya ya akili, mfadhaiko na kuzuia kujiua.
Kwa kuongea na kutafuta ushauri kuhusu changamoto za kimaisha, kunaweza kusaidiwa pakubwa kuepusha athari za matatizo ya kiakili.
Dalili zinazoashiria magonjwa ya akili ni nyingi, japo zimegawanywa Kisayansi katika makundi matatu ambayo ni: Kihisia, kimwili na kiakili.
Ushauri wa wataalamu wa afya ya akili ni kwamba watu wanapaswa kujenga desturi ya kupima hali zao za afya ya akili.