Pilipili ni matunda ya mpilipili, ni matunda ambayo sio matamu kama matunda mengine lakini ni mazuri kwa afya ya mwanadamu. Ni matunda yanayochukiwa na wengi kiasi kwamba huwezi kununua na kupelekea mtu kama zawadi, pengine akikutuma umletee. Pilipili ziko za aina nyingi na inasemekana zilitoka bara la Asia na kusambazwa hadi Marekani kabla ya kuletwa Afrika na nchi zingine ulimwenguni.
Pilipili zaweza patikana kwa rangi tofauti tofauti kama vile nyekundu, zambarau, manjano na kijani kulingana na mazingira au aina ya mmea wa pilipili. Kisayansi pilipili waeza kuziita Capsicum, kiambata ambacho hufanya pilipili kuwa na ladha kali ya uchachu na pia kuongeza ladha nzuri kwa chakula ni Capsaicin. Kuna pilipili ambazo ni kali na zingine ambazo sio kali.
Pilipili ambazo hazina ukali ni kama vile pilipili hoho. Pilipili ambazo ni kali na ambazo zaweza kukufanya ukatokwa na machozi kama mtu ambaye analia ni pilipili mbuzi na pilipili kichaa, pilipili kichaa ndio kali zaidi. Licha ya tunda hili la pilipili kutopendwa na watu wengi, ina manufaa na faida katika mwili wa mwanadamu.
Walaji wa pilipili huongeza pilipili kwa samaki au nyama ambayo imepikwa vizuri ili wafurahie mlo lakini hawafahamu umuhimu wake. Kwanza pilipili ina Vitamini A ambayo humkinga mtumiaji dhidi ya hatari ya kupata magonjwa mengi kama vile saratani za aina mbali mbali na ugonjwa wa moyo.
Madini mwilini
Pilipili pia ina Vitamini C ambayo kazi yake kubwa ni kuzuia magonjwa ya kupooza, moyo na pia magonjwa ya macho. Pilipili tena iko na Vitamini K ndani yake ambayo husaidia ukuaji wa mifupa, pia pilipili ni muhimu katika kufanikisha mzunguko wa damu mwilini.
Pilipili husaidia kuondoa kichefuchefu, kikohozi, homa na ugonjwa wa magoti,Pilipili pia husaidia kupunguza uzito wa mwili, kuzuia vidonda vya tumbo, kuondoa maumivu makali mwilini na kuzima kuvimba kwa tezi mwilini. Wataalamu wanasema kuwa pilipili pia ni muhimu zaidi katika kuimarisha nguvu za kiume kwasababu hufanya mzunguko wa damu kuwa mzuri mwilini.
Pilipili inasemekana kuwa na uwezo mkubwa sana wa kupunguza kasi ya uzee, hivyo basi, kama hautaki kuzeeka haraka basi hakikisha unaongeza pilipili kidogo kwa chakula chako kila siku. Kama wewe sio mlaji wa pilipili na unataka kuanza kula, usitumie pilipili nyingi kwa chakula, usiongeze pilipili nyingi kwa chakula hata kikakushinda kula.
Chukua pilipili kidogo na uongeze kwa chakula, fanya hivyo kila siku hadi wakati utazoea. Wengine huongeza pilipili nyingi kwa chakula hadi wakati wanakula chakula machozi yanadondoka kana kwamba wamepigwa na kulazimishwa chakula kwa nguvu. Hata kama wewe pia ni mlaji sugu wa pilipili, usitumie pilipili nyingi japokuwa ina manufaa mwilini, kumbuka, kitu hata kiwe cha manufaa, ukitumia kwa wingi kinaleta madhara.