Mwanadamu ameumbwa na kuwekwa katika mazingira ambayo inamlazimu kuugua au kuwa mgonjwa kutokana na sababu mbali mbali. Hata hivyo imebainika wazi kwamba wanawake huathirika zaidi na baadhi ya magonjwa kuliko wanaume. Mwanamke ana magonjwa maalum yanayomsibu kuliko mwanaume. Zaidi ya hayo magonjwa ya wanawake hayafanyiwi upekuzi wa mapema kulingana na wataalamu, na majaribio mengi ya madawa hayashirikishi masuala ya wanawake.
Kuna magonjwa kadha ambayo hayo yanawasibu mno wanawake yakiwa ni pamoja na saratani ya matiti, saratani ya mfuko wa uzazi, kufikia kukoma kwa siku zao za hedhi, na mimba. Wanawake hupata magonjwa ya mshtuko wa moyo na kuwasababishia vifo kuliko wanaume. Kupata dhiki za moyo na wasiwasi ni magonjwa ambayo humkumba zaidi mwanamke anapougua. Mbali na hayo mwanamke hukabiliwa zaidi na matatizo ya njia ya haja ndogo yaani mkojo, kuliko wanaume, na magonjwa ya zinaa pia huleta madhara makubwa kwa wanawake. Miongoni mwa magonjwa ambayo humsibu mwanamke zaidi magonjwa manane yanayofuata ndiyo yanayomvamia mara kwa mara zaidi na kutishia hali yake ya afya.
Ugonjwa wa moyo
Ingawa inachukuliwa kwamba ugonjwa wa moyo ni swala kuu la kiafya kwa wanaume, ugonjwa huu huwasibu wanaume na wanawake kwa kiwango sawa, huku asilimia 54 ya wanawake hasa nchini Marekani wakidhani kwamba ugonjwa wa moyo ndio unaoongoza katika magonjwa yanayosibu wanawake zaidi nchini humo. Katika nchi hiyo taarifa zinaeleza kwamba asilimia 49 wanaugua magonjwa ya buhari kuu, yaani (high blood pressure) chembe chembe za kemikali zinazojulikana kama cholesterol ambaazo hupatikana ndani ya damu, na zinapokuwa nyingi husababisha magonjwa ya moyo.
Saratani ya matiti
Saratani ya matiti ambayo huanzia kwenye kibomba cha kupitishia maziwa ya mama, ina uwezo wa kusambaa hadi kwenye viungo vingine, na ndio ugonjwa hatari zaidi unaowaathiri wanawake kote ulimwenguni. Ugonjwa huu unapatikana zaidi miongoni mwa wanawake wa nchi zilizostawi kwa sababu ya ongezeko la vipindi vya muda wa maisha. Mnamo mwanzo wa ugonjwa huu, mwanamke mwenye ugonjwa wa saratani ya matiti hupata kivimbe kikubwa zaidi ya chunusi. Nyingi ya chunusi hizo huonekana kutokuwa tishio, lakini ni muhimu kwa wanawake kwenda kufanyiwa uchunguzi na wahudumu wa afya.
Saratani ya mfuko wa uzazi
Watu wengi hawafahamu tofauti kati ya saratani ya ngai za mayai na saratani ya mfuko wa uzazi. Saratani ya ngai ya mfuko wa uzazi huanzia
katika mfuko wa uzazi, nayo saratani ya ngai za mayai huanzia kwenye vifereji au vijibomba vinavyopitisha mayai ya uzazi. Huku aina hizo mbili za saratani zikiwa na maumivu sawa, saratani ya mfuko wa uzazi husababisha mwanamke kutokwa na utomvu katika sehemu zake za siri, na kusikia maumivu makali wakati wa kitendo cha kujamiiana na mwanamume. Huku saratani ya ngai za mayai ikijitokeza na dalili zisizoeleweka,
ugonjwa huu kadhalika ni vigumu kueleweka. Uchunguzi wa ugonjwa wa saratani wa kutumia taaluma inayojulikana kama “pap smear” ambapo chembe chembe za sehemu ya tupu ya mwanamke katika eneo ambalo mtoto hukua, huchukuliwa na kufanyiwa uchunguzi, hugundua saratani ya mfuko wa uzazi, lakini haiwezi kugundua saratani ya ngai za mayai.
Malezi ya afya ya mwanamke
Kutokwa na damu na kutokwa na utomvu ni hali ya kawaida ya mwanamke ambaye yuko katika hedhi. Hata hivyo kunapotokea dalili nyingine zaidi ya hizo wakati wa hedhi, na dalili zisizo za kawaida kama kutokwa na damu katikati ya majira tofauti ya hedhi, na kwenda haja ndogo mara kwa mara kwaweza kuiga aina nyingine ya dalili za magonjwa. Matatizo mengine ambayo yanaweza kuchipuka katika sehemu za siri za mwanamke yanaweza kuashiria matatizo mabaya kama vile magonjwa ya zinaa, ama saratani ya vibomba vya uzazi. Huku wahudumu wa afya wakiwa na uwezo wa kutibu dalili hizo kwa urahisi kama hazijakuwa sugu, kama hazitibiwi mapema zinaweza kuleta madhara kama vile kukosa rutuba ya uzazi na magonjwa ya figo kutofanya kazi.