Naibu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, IEBC Juliana Cherera amewasilisha majibu yake kuhusu kesi ya kupinga ushindi wa Rais Mteule, William Ruto. Cherera amedai kwamba kulikuwa na aina mbili za fomu 34A nyingine ambayo Cherera amesema haikuwa halali. Pia amedai kwamba matokeo katika maeneo mbunge 27 hayakuthibitishwa kabla ya kutangazwa. Amesema matokeo yaliyotangazwa na Mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati yalikuwa yake binafsi wala si matokeo ya tume.
Mbali na hayo amedai kwamba tangu wateuliwe katika IEBC pamoja na makamishna wengine ambao ni Justus Nyang'aya, Irene Masit na Francis Wanderi hawajakuwa wakihusishwa ifaavyo katika kufanya maamuzi mbalimbali.
Cherera amedai kwamba Chebukati amekuwa akiwahamisha maafisa wa uchaguzi bila kuwahusisha makamishna vilevile kutofanya mkutano wa kujadili namna ya kutekeleza mapendekezo ya kampuni ya KPMG iliyofanya ukaguzi wa sajili ya wapiga-kura.
Aidha amedai kwamba Chebukati amekuwa akifanya vikao na wanahabari bila kuwajulisha makamishna wengine kwanza.
Hapo jana Kamishna Nyang'aya pia aliwasilisha majibu yake kwa Mahakama ya Juu ambapo alitaja masuala kadhaa likiwamo na kutengwa na Chebukati katika kuyathibitisha matokeo ya mwishio ya kura za urais.
Katika majibu ayo hayo aidha Cherera amedai kwamba uamuzi wa kuahirisha uchaguzi katika maeneo manane nchini ulifanywa na Chebukati bila kuwahusisha makamishna wengine.
Cherera amesema walifahamu kuhusu hatua hiyo kufuatia tangazo lililofanywa na Chebukati kupitia vyombo vya habari. Ameendeela kudai kuwa Chebukati amekuwa akiendesha shughuli za tume hiyo binafsi huku akiwapuuza makamishna wnegine.
Ikumbukwe mrengo wa Azimio umekuwa ukidai kwamba IEBC iliahirisha uchaguzi hasa katika Kaunti ya Mombasa na Kakamega ili kupunguza idadi ya wapigakura ambao wangejitokeza kushiriki shughuli hiyio Agosti, 9 kwa kuwa ni ngome yao.
Kando na Mombasa na Kakamega maeneo mengine ambapo uchaguzi uliahirishwa ni maeneo bunge manne ambayo ni Kacheliba, Pokot Kusini, Rongai na Kitui Rural, Wadi ya Njenga, iliyoko Embakasi na Nyaki, kwenye Kaunti ya Meru.
Uchaguzi huo utafanyika Jumatatu ijayo.