Kauli ya Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Nchini KNUT Wilson Sossion kwamba wanafunzi wa shule za Sekondari nchini wanafaa kuruhusiwa kumiliki simu za rununu na kuwa nazo wakiwa shuleni, bila shaka itaibua hisia kali miongoni wa washikadau katika sekta ya elimu.
Kwa maneno yake mwenyewe, Sossion amesema ni sharti Waziri wa Elimu Fred Matiang'i atoe amri ya kuwaruhusu wanafunzi kumiliki simu hizo. Kulingana naye hatua hiyo itawasaidia wanafunzi katika kijiendeleza kimasomo, kukiwamo kufanya utafiti. Lakini swali langu ni je, umiliki wa simu za rununu miongoni mwa wanafunzi wa shule za sekondari nchini hautaathiri masomo yao? Kumbuka, humu nchini wanafunzi wa sekondari ni wa kati ya umri wa miaka 14 hadi 18 ikizidi mkubwa zaidi atakuwa wa umri wa miaka 20.
Hawa ni vijana wanaobalehe. Katika umri huu zaidi ya asilimia 85 huyaelewa mambo kwa njia tofauti, wapo wanaoamini wanajua kila kitu ulimwengu huu, wasiotaka kuambiwa wala kusikiliza. Je, ukiwapa chombo kama hiki, una hakika kwamba watakitumia kwa manufaa yao ya kimasomo? Upo ushawishi katika mitandao ya kijamii, watatazama wanamitindo, waigizaji na kutaka kuishi kama wao bila kufahamu kwamba maisha ya wanaowatamani labda ni ya uigizaji tu. Mwanafunzi ataketi darasani badala ya kufanya utafiti kuhusu Historia au somo lolote inavyostahiki atasalia kutazama vipinbi kama vile''Keeping up with the Kardashians, Rich Kids of Bervaly hills'' au masuala ambayo sio ya manufaa hata kidogo. Ukweli ni kwamba ni asilimia ndogo sana itakayotenga muda labda kuvitazama vipindi vya manufaa au vituo kama KTN News, CNN na BBC.
Mwanafunzi wa kidato cha kwanza mwenye umri ya miaka 14 akivitazama vipindi kama vile vya familia ya Kardashian ni rahisi kuwa na tamaa ya kuishi maisha kama yale na huenda akashawishika kutafuta njia za kumwezesha kuishi vile.
Sisemi wanafunzi kumiliki simu za rununu ni kosa. Lakini kwangu mimi wanafunzi hawafai kamwe kuruhusiwa kwenda na simu za rununu shuleni na kuingia nazo darasani. Sababu yangu ni hii; utamthibiti vipi yule mwanafunzi anapokuwa darasani badala ya kumsikiliza mwalimu, au kusoma, yuko kwenye Twitter, WhatsApp, Instagram au Facebook?
Kwa sasa sidhani kwamba Kenya imefika katika kile kiwango cha kuwaruhusu wanafunzi hasa katika shule za umma kufanya utafiti wao kwenye simu za rununu. Iwapo ni lazima basi ni jukumu la serikali kuyajenga maabara na kuzinunulia kila shule kompyuta ambapo wanafunzi wanaweza kufanyia utafiti wao kwa mwongozo wa walimu.
Ni dhahiri kwamba shule ni sehemu ambapo usawa wa wanafunzi hutiliwa mkazo. Ndiyo maana kuna mavazi sare, mitindo sawa ya nywele na hata vitafunywa wanavyoruhusiwa wanafunzi kuwa navyo mabwenini. Nijuavyo kwa sasa hakuana viwango vilivyowekwa vya aina za rununu wanazoweza kuwa nazo wanafunzi. Je, itakuwaje ikiwa baadhi ya wanafunzi wataweza kununua simu mahiri ilhali wenzao, wazazi wenyewe hawawezi hata kumudi rununu za kawaida almaarufu mulika mwizi? Ule usawa hautakuwepo na visa vya kuoneana kinyongo na hata wizi vitashuhudiwa.
Ikumbukwe serikali ya Jubilee tayari imeanza ule mpango wake wa ahadi kwamba kila mwanafunzi anayejiunga na darasa la kwanza atapata kipakatalishi na iwapo utatimia itakuwa njia mwafaka kuwaruhusu wanafunzi kuanza kutumia teknolojia katika masomo yao wakiwa wachanga. Lakini kwa sasa simu za rununu, la hasha. Carren Omae, Ripota Radio Maisha
[email protected] [email protected]
Twitter: @CallenOmae