Mahakama ya Juu imeorodhesha masuala makuu 9 ambayo itayachunguza na kutafuta majibu yake katika kesi inayopinga matokeo ya uchaguzi wa urais.

Akizungumza wakati wa kikao cha utangulizi wa kesi hiyo, Jaji Mkuu Martha Koome amesema masuala hayo lazima yajibiwe wakati wa kutoa uamuzi.

Masuala hayo ni kama vile kubainisha iwapo mfumo uliotumiwa kuchapisha matokeo ulikuwa wa kuaminika, unaoweza kuthibitishwa na kutegemewa, iwapo kuahirisha uchaguzi katika maeneo manane kuliathiri kujitokeza kwa wapiga-kura katika maeneo hayo, iwapo IEBC iliendesha shughuli ya kuhesabu kura inavyohitajika kisheria, na iwapo Rais Mteule, William Ruto alipata asilimia 50 na kura moja zilizopigwa.

Suala jingine ni iwapo kulikuwa na tofauti zozote katika matokeo ya fomu 34A yaliyochapishwa katika wavuti wa IEBC na yaliyowasilishwa moja kwa moja katika ukumbi wa Bomas.

Aidha, mahakama hiyo imeagiza kufunguliwa kwa masanduku ya kupigia kura katika vituo kumi na vitano ili kufanyiwa ukaguzi na kura kuhesabiwa upya kufikia siku ya Alhamisi wiki hii.

Vituo hivyo ni kama vile Nandi Hills, Shule ya Msingi ya Sinendeti iliyoko kwenye Kaunti ya Nandi, vituo vya Belgut, Kapsuser, Chepkutum kwenye Kaunti ya Kericho, Jomvu, Majengo, Mvita, na Mikindani kwenye Kaunti ya Mombasa. Vingine ni Jarok, Gathanji na Kiheo kwenye Kaunti ya Nyandarua. Fomu 34A na 34C zilizotumiwa kunakili matokeo ya vituo hivyo pia zitawasilishwa.

Mahakama pia imeagiza kuwasilishwa kwa fomu zilizoandikwa na Mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati kunakili dosari mbalimbali zilizogunduliwa wakati wa kuthibitisha matokeo katika Ukumbi wa Bomas kati ya Agosti 10 na Agosti 15. Nyingine ni nakala ya maneno ya siri yaani password na wamiliki wake vilevile wenye ruhusa ya kuitumia mifumo ya IEBC.