Mwili wa aliyekuwa Afisa Mkuu wa Tume ya Uchaguzi IEBC wa eneo Bunge la Gichugu aliyefariki dunia utafanyiwa upasuaji leo hii kubainisha kiini cha kifo chake.

Maafisa wa Idara ya Upelelezi DCI wanaoendesha uchunguzi kwa sasa wamefutilia mbali madai kwamba huenda afisa huyo, Geoffrey Gitobu aliuliwa.

Mkuu wa DCI katika eneo la Nanyuki Onesmus Toiwet amesema kwa sasa wanachunguza kisa cha kifo cha ghafla akisema uchunguzi wa leo ndio utakaoweka bayana, kilichosababisha kifo cha Gitobu.

Inaarifiwa Marehemu Gitobu alikuwa ameenda kuitembela familia yake baada ya kukamilisha shughuli ya usimamizi wa uchaguzi katika Eneo Bunge la Gichugu.

Inaarifiwa alianza kuugua alipokuwa na nduguye mjini Nanyiki na alithibitishwa kufariki dunia alipofikishwa hospitalini kwa matibabu.

Kisa hiki kinajiri wakati ambapo IEBC imeelezea wasiwasi kuhusu usalama wa maafisa wake kufuartia matukio mbalimbali kipindi hiki cha uchaguzi.

Jumatatu wiki hii tume hiyo ilitao taraifa kuelezea kutibuliwa kwa jaribio la kuwashambulia maafisa wake waliokuwa wakiandaa stakabadhi za kesi za kupinga matokeo zilizowasilishwa mahakamani.

Aidha Aliyekuwa Afisa Msimamizi wa Uchaguzi katika eneo la Embakasi Mashariki alipatikana akiwa amefariki dunia siku chache baada ya kutoweka. Afisa mwingine katika eneo la Eldas Kaunti ya Wajir anauguza majeraha baada ya kushambuliwa katika kituo cha kupiga kura.


Embakasi IEBC ELDAS