×
The Standard Group Plc is a multi-media organization with investments in media platforms spanning newspaper print operations, television, radio broadcasting, digital and online services. The Standard Group is recognized as a leading multi-media house in Kenya with a key influence in matters of national and international interest.
  • Standard Group Plc HQ Office,
  • The Standard Group Center,Mombasa Road.
  • P.O Box 30080-00100,Nairobi, Kenya.
  • Telephone number: 0203222111, 0719012111
  • Email: [email protected]

Moha Jicho Pevu: Wanahabari Kenya ni makatuni

News
 Taarifa zimekuwa maonyesho ya paja na ukubwa wa makalio

Huu ni wito kwa wanatasnia ya habari nchini.

Leo mwenzenu nalia kuona taaluma bora zaidi ikisambaratishwa na wahalifu wachache ndani ya uanahabari. Wahalifu wanaojiita wanahabari wa kizazi kipya. Leo taaluma hii imebakwa na watu wasiojua lolote kuhusu uanahabari.

Kenya ya sasa ukitaka kuwa mwanahabari kama wewe ni mwanadada, basi valia nguo itakayobana makalio yako, onyesha kifua chako kuwavutia watazamaji, fanya uhusiano wa kimapenzi na wahariri au lala kitanda kimoja na wakuu serikalini. Ukifanya hivyo basi nyota yako itang’aa kwa haraka upesi.

Kwanza, Mkuu wa kitengo au Mhariri ataanza kukupa safari za humu nchini na za kimataifa, atahakikisha kuwa wewe utakuwa ukisoma taarifa zote za habari, kila unapopendekeza jambo hata kama ni la kijinga, utasikizwa kwa maana ujinga wako umeteka nyara ujinga wa mhariri. Utapewa safari za mikutano ya kampuni lakini kila unapopewa safari hizo ole wako jioni kichinjio. Huu ndio umaarufu wa wanahabari wa sasa.

Leo hii katika vyombo vya habari ni nadra sana kupata sauti za wanahabari shupavu, wanahabari wanaotambulika na kuaminika na wakenya. Siku hizi sauti utakazoziskia ni sauti za kinafiki. Sauti za kuimba na serikali badala ya kuwa macho ya wakenya, sauti za dhulma badala ya kupiga vita dhulma, sauti za wezi na wafisadi wakuu wanaokula na serikali na kunyamaza wakati wakenya wanapoangamizwa na serikali ya wezi.

Kwa wanahabari wa kiume sawia na wa kike, wanunulie gari ndogo kuwapumbaza akili, watumie pesa za wizi za NYS au Eurobond na kuwanunulia nyumba, watumie shilingi elfu tatu kila ijumaa za kunywa pombe, waite katika hafla zenu za anasa na kuwasifu mbele ya wezi wenzenu ndani ya serikali.Kisha jioni kwenye habari wao ndio wanaokuwa wakwanza kuripoti sifa na uwongo za wezi wakuu serikali.

Leo kila mwanasiasa ana ripota wake, kila mwizi ana ripota wake ndani ya vyumba vya habari. Idadi ya wezi ndani ya vyumba vya habari imeongezeka kutokana na wahariri waharibifu na wabaya zaidi. Wahariri hawa hawana elimu tosha ya uanahabari. Wengine ni waoga wakubwa wasiosimama na wanahabari wadogo na wajasiri. Wahariri hawa ndio chanzo cha matatizo katika taaluma hii.

Wengi wao hupewa mamilioni ya pesa kudhulumu taarifa za wanahabari. Wao ndio hupanga ratiba ya uongo badala ya kuweka ajenda ya kulinda maslahi ya kila mkenya. Leo ukitembelea vyumba vya habari utapata watu wa sampuli tofauti wakitikwa majukumu ya wanahabari. Utapata mtu asiyejua lolote kuhusu uanahabari akipaza sauti yake katika mikutano ya wanahabari na kujifanya kujua zaidi.

Ngono na ufisadi zimetawala taaluma hii. Leo njama za kukinga serikali zinaandaliwa katika ikulu na kutumiwa wahariri hawa ambao huwalazimisha wanahabari wadogo kufuata ajenda zao. Leo taarifa zimegeuzwa na kuwa maonyesho ya paja, matiti na ukubwa wa makalio. Leo twatangaza ngono, safari za Rais, mahojiano tasa badala ya kutangaza dhulma, mauaji, wizi, ufisadi na ukiukaji wa haki za binadamu.

Kila mwanahabari ana maslahi yake. Hawajali kama wanahabari wa zamani. Leo naumwa nikiwakosa wanahabari mti wenzangu wa zamani kama vile Linus Kaikai, Farida Karoney, John Allan Namu, Njoroge Mwaura, Wazir Khamsin, Cathrene Soi, Peter Moss, Sinjiri Mukoba, Kizito Namulanda, Newton Ndebu, Ondeko Aura, John Mwendwa, Ali Mtenzi, Swaleh Mdoe, Nuhu Bakari, Katua Nzile miongoni mwa wanahabari na wahariri wengine chapa kazi. Jameni mko wapi? Taaluma hii imebakwa na watu wasiodhamini kazi hii yetu tunayoipenda.

Kwetu sisi huu ni mwito ila kwa wengine ni biashara na maslahi. Kila ninapotizama runinga nashangaa kuwakosa maripota wa kiume waliobobea katika taaluma hii. Sura ni sura za kike kuanzia jioni hadi usiku. Jameni waume wenzangu kuna nini? Sina chuki na kina dada zangu lakini kama mwanahabari aliyepitia mengi ninahofia taaluma hii inakufa kifo cha pole pole.

Naogopa wakenya wameanza kupoteza imani na sisi. Hawatuamini kama wanahabari kwani hatuna lolote la kuwaambia. Leo hii wakitaka habari wanakimbia mitandaoni kupokea taarifa za kina kutoka kwa wanablogu maarufu nchini. Hii ni dalili ya wao kupoteza imani nasi.

Naomba turudi tulikotoka. Turudi miaka ya 2007 wakati uanahabari ulikuwa uanahabari kamili. Tuondoe chuki ndani ya vyumba vya habari, tuondoe ukabila, ukiritimba, ufisadi, ngono na mapendeleo tuweze linda maslahi ya wakenya na kuwa macho yao.

Mohammed Ali ni Mhariri Mkuu wa Kitengo cha Upekuzi KTN. Kuwasiliana naye: [email protected], FB: Official Jicho Pevu with Mohammed Ali, Instagram: @mohajichopevu, Twitter: @mohajichopevu

Related Topics


.

Latest Articles

.

Recommended Articles