Gari ambalo bondeka [Picha: Hisani]

Umekuwa ni wimbo. Umekuwa ni mkarara. Katika vikao kwa mikao.

Kauli ni: Uwe na sikukuu njema, usafiri salama, uwe makini barabarani, ukinywa usinywe pombe na waendesha gari, nafuu unnywe maziwa... blah blah blah nyingi tu!

Wimbo huu utaimbwa hadi lini? Kila mwaka kipindi kama hiki na msimu kama huu hekaya ni zizo hizo kwa hizo.

Vyombo vya habari kutawaliwa na habari zizo hizo. Yaani hakuna habari nyingine nzuri ila mikasa.

Inauma na kusikitisha kuwa katika hafla hizi za kujienjoy na familia, nayo magazeti, redio, runinga na mitandao ya kijamii inashamiri picha na takwimu za vifo kutokana na ajali za barabarani.

Hata wino ungali kufutika kuhusu mkasa mbaya sana wa ajali iliyojiri eneo la Karai, barabara ya Nakuru-Naivasha, kukajiri ajali nyingine huko Mazeras, kisha nyingine huko Timboroa, kisha na kisha nyingi tu.

Binadamu tumeumbiwa tamaa mbaya sana! Wamkuta dereva wa Buruburu sasa kipindi hiki cha uhaba wa magari ya uchukuzi, amechukua gari lake na kulipeleka katika barabara ya Kisumu ili kuvuna vuno la haraka.

Usisahau haijuia barabara hiyo nje ndani, lakini analipiza nauli maradufu. Anaendesha gari usiku na mchana! Hadi kusinzia usukanini!
Kwani tumekwisha kukisahau kisa cha Ntulele jamani?!

Barabara zetu zimejaa maduta ambayo utadhani ni milima ya Kilimanjaro. Maduta hayo hayana alama hata chembe. Leo hii ajali zimeongezeka katika barabara zetu hadi wananchi wenyewe ‘kujilimia’ barabara ovyo na kujiwekea hizo bumbs.

Hali ni mbaya mno katika barabara zetu hivi kwamba ilibidi rais Uhuru Kenyatta “kuzikemea’ hizo bumps kwenye maadhimisho ya sherehe za 53 za sikukuu ya Jamhuri! Je, vipi hali za barabara zenyewe? Tuachie hapo.

Wizara ya uchukuzi, ikishirikiana na Halmashauri ya Taifa ya Uchukuzi na Usalama nchini, NTSA, vimekuwa vikipiga kelele lakini wepi.

Sasa hivi chunguza magari katika barababara zetu. Idadi ni kubwa ya yale ambayo haystahili kuwa barabarani. Ubovu na ukweche wao. Moshi wenye kemikali.

Baadhi hayana bima. Mengi hayana breki. Ati kuna zana za kupima kasi barabarani. Ewe! Ni vituko kama sio kasheshe!

Na wanaoendesha kasi kupita viwango je? Na wanaopitia njia za mkato? Bodaboda je? Na madereva walevi je?

Leo hii wizara ya uchukuzi, polisi wa trafiki, NTSA vimekuwa vikombe mdomo wazi vya kupokea hongo na kufumbia jicho ajali katika barabara zetu.

Hassan mwana wa Ali ni Mhariri wa Michezo na Nahodha wa Nuruyalugha (Radio Maisha).
alikauleni@gmail.com, akaulen2@standardmedia.co.ke, FB: Ali Hassan Kauleni, Hassan mwana wa Ali,
Twitter: @alikauleni