Raila Odinga kutoa tangazo kuu Jumatatu
Na Beatrice Maganga
Kabla ya tangazo la Mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati kwamba uchaguzi umeahirishwa kwenye kaunti za Siaya, Homabay, Migori na Kisumu, suitafahamu ilikuwa imetanda hasa kufuatia kauli za viongozi wa NASA za kuwashauri wakazi kususia shughuli hiyo. Wakazi nao waliapa kusambaratisha marudio hayo huku Kinara wao, Raila Odinga akiahidi kutoa mwelekeo zaidi kwa wafuasi wake siku ya Jumatatu wiki ijayo.
Kufuatia tangazo la Tume ya Uchaguzi, IEBC jana kwamba itarejelea uchaguzi kwenye maeneo mengine, Kinara wa National Resistance Movement, NRM Raila Odinga amesema wakati wa kaunti hizo hawastahili kulazimishwa kushiriki. Raila Odinga amesema Jumatatu wiki ijayo, atatoa tangazo kuu kuhusu mwelekeo watakaouchukua baada ya uchaguzi wa jana. Akihutubia umma kwenye Eneo Bunge la Kibra, Raila aidha amesema serikali imewatumia maafisa wa polisi kuwadhulumu wakazi.
Ameongeza kuwa NASA inafanya mpango kukarabati miundo-misingi iliyoharibiwa eneo la Kibra wakati wa maandamano ya wafuasi wake. Amesema Mbunge wa eneo hilo, Ken Okoth ndiye atakayesimamia ukarabati huo, kisha yeye kuukagua baada ya kumalizika.
Mapema leo, akihojiwa na kituo kimoja cha habari leo hii, Raila ameutaja uchaguzi wa jana kuwa usiodhihirisha uamuzi wa Wakenya wote huku akiwasihi wafuasi wake kudumisha amani. Raila amesema wanajiandaa kwa uchaguzi ambao anasema unastahili kufanyika katika kipindi cha siku 90 baada ya mahitaji yao kutimizwa.  
Wakati uo huo, NRM imedai kwamba serikali inapanga kutekeleza mauaji eneo la Nyanza wakati wa kurudiwa kwa uchaguzi. Wameyapuuza madai kwamba utovu wa usalama kwenye Kaunti za  Migori, Homabay, Kisumu na Siaya ndio uliochangia kufutiliwa kwa uchaguzi huku mmoja wa vinara, Musalia Mudavadi akisema kwamba wakazi hawataki kushiriki uchaguzi na ni shari haki yao iheshuimiwe.
 
Awali, vongozi wa dini na wa kisiasa mjini Kisumu walimtaka Mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati kuagiza kuondolewa kwa vifaa vya uchaguzi kwenye maeneo hayo.
Viongozi hao wanahofia vifo zaidi iwapo shughuli hiyo itaendelea kesho, kwani mauaji yamekuwa yakishuhudiwa maeneo hayo kila mara waandamanaji wanapokabiliana na maafisa wa polisi.
Wakazi wa kaunti za Siaya na Homabay vilevile wamepinga marudio ya uchaguzi huku wale wa Kanisa la Seventh Day Adventist wakitaka ufanyike siku tofauti.
Gavana wa Kisumu, Profesa Anyang' Nyonyo amesema marudio ya uchaguzi hayakufuata utaratibu wa kisheria hivyo huwezi kuwa huru na haki. Amesema ni sharti msimamo wao wa kutotaka kushiriki shughuli hiyo uheshimiwe, huku akikashifu visa vya mauaji ya polisi maeneo hayo.
Chama cha Wanasheria nchini LSK, vilevile kimewataka maafisa wa polisi kukoma kutumia nguvu wanapowakabili waandamanaji ikizingatiwa visa vya mauaji na majeruhi vilivyoshuhudiwa maeneo ya Nyanza. Aggrey Nyamwamu ni mwanachama wa LSK kwenye Kaunti ya Kisumu.  
Wakati uo huo Raila amesema wanafanya mipango ya kukarabati miundo-misingi iliyoharibiwa eneo la Kibra wakati wa maandamano ya wafuasi wake. Amesema Mbunge wa eneo hilo, Ken Okoth ndiye atakayesimamia ukarabati huo, kisha yeye kuukagua baada ya kumalizika.