×
The Standard Group Plc is a multi-media organization with investments in media platforms spanning newspaper print operations, television, radio broadcasting, digital and online services. The Standard Group is recognized as a leading multi-media house in Kenya with a key influence in matters of national and international interest.
  • Standard Group Plc HQ Office,
  • The Standard Group Center,Mombasa Road.
  • P.O Box 30080-00100,Nairobi, Kenya.
  • Telephone number: 0203222111, 0719012111
  • Email: [email protected]

Moha Jicho Pevu: Je, Wakenya tutameza mate hadi lini?

News
 Leo nasema kuleni, kesho mtatapika! Picha: Hisani

Nilipozungumzia uongozi wa kijiji katika mojawapo ya makala yangu, yamkini watu wengi hawakunielewa.

Uongozi wa kijiji ni uongozi wa kiburi, ukabila na chuki dhidi ya wanaoulizia nafasi yao uongozini.

Mwalimu Julius Nyerere alisema na nikinukuu, “Mnaingia karne ya 21 mmepanda basi la ukabila, mnaona sifa kuulizana makabila. Mnataka kutambika?” Hii ndio hali halisia ya Kenya. Taifa la viongozi kufoka hadharani na kuwataka wakenya kujua wazi kwamba watazidi kumeza mate wao wakila nyama.

Jambo la kusikitisha zaidi ni kwamba serikali iliyo mamlakani iko tayari kupambana na wananchi wake wanaodai haki na uhuru wa kusikilizwa zaidi, kuchagua viongozi wawatakao na kuamua kuhusu mustakabali wa nchi yao.

Katika mazishi ya William ole Ntimama, kiongozi mmoja wa dini alisimama tisti na kumtaka Uhuru Kenyatta afahamu ima wazi kuwa mambo hayakwendi sambamba. Mchungaji huyu alinikumbusha wachungaji wengine maarufu kama vile Father Kaisser na Bishop Muge, wachungaji waliokufa wakipigania ukweli kama inavyopendekeza dini zote.

Nafurahi kuanza kuona viongozi wa dini wakisimama na kupinga dhulma, tofauti na wale tulionao ambao uongozi wao wa dini hauna tofauti na chama kipya cha siasa.

Uhuru Kenyatta katika mazishi hayo alifoka sana na kupoteza dira ya uongozi kiasi cha kuwaambia wakenya wazidi kumeza mate minofu ni yao. Uongozi hauhitaji hasira dhidi ya waliokuchagua wala kujipiga kifua na utawala wa ki-imla. Uongozi ni kuwa na hekima na busara.

Sasa bwana Uhuru Kenyatta wakenya walalahoi, wengi ambao wamezidi kumeza mate kwa kipindi cha miaka mitano wameungana kupigania huo mnofu. Kila mmoja wao sasa barazani anazungumzia machungu ya kumeza mate hata bila ya maji kwa kipindi cha miaka mitano. Kenya nzima inaimba wimbo wa kutaka kula nyama. Hili ni wimbi la wawindaji wanaowawinda viongozi wawili tu, Uhuru Kenyatta na William Ruto.

Viongozi waliokataa kugawa nyama kwa taifa na badala yake kuwaambia wakenya wazidi kumeza mate. Kutia donda msumari wa moto kwenye kidonda picha ya kiongozi wa taifa akila nyama mitaani iliendelea kuwachoma wengi na hata kuwafanya sasa waamini zaidi kuwa hili swala la nyama lilikuwa jambo la kweli.

Bwana Uhuru Kenyatta kuna msemo unaosema kuwa hata uwe na gari la kifahari, chooni ni lazima utashuka kujisaidia. Dira ya uongozi huonekana kutoka kwa matamshi na vitendo ya viongozi waliotwikwa majukumu na wananchi wa taifa lao. Kunapotokea dalili ya kiongozi kutapatapa na kuanza kububujikwa na maneno basi uongozi huo unakaribia ukingoni kwani nguvu za wengi hushinda nguvu za wachache.

Haiba iliyojengwa na wapigania uhuru wa Kenya imepotea. Imepotea kwa sababu Kenya sasa inapata viongozi wenye uroho wa madaraka. Kenya limekuwa taifa la visa na mikasa. Inasikitisha sana. Kenya imesimama, Kenya imezama. Kenya halitembei kiuchumi, kidemokrasia, kiteknolojia. Taifa hili linaelekea kupotea katika uso wa dunia. Mkoloni hajaondoka Kenya! Bado yupo. Iliondoka tu ngozi nyeupe, lakini ukoloni ulibaki. Ipo ngozi nyeusi inaendeleza ukoloni uliokuwa umeasisiwa na ngozi nyeupe.

Namalizia kwa kusema kuwa ipo siku Kenya litakuwa taifa lakujihami. Watawala wa taifa hili watambue kwamba Wakenya hawakuutafuta uhuru kwa ajili ya kuwanyenyekea wao, bali waliutafuta uhuru ili waondokane na kongwa la ukoloni lililokuwa limewafunga.

Tatizo la Kenya sio jinsi ya kubinafsisha uchumi na kuchochea uchu wa kupata, bali ni jinsi ya kupiga vita jeuri ya ufahari, majivuno na majigambo ya kiuzawa katika kutawala uchumi.Viongozi hapa nchini wanatumia sana mdomo, tumbo, macho, pua, ulimi na sehemu zingine za mwili ili kuweza kutatua matatizo yao. Leo nasema kuleni, kesho mtatapika!

Mohammed Ali ni Mhariri Mkuu wa Kitengo cha Upekuzi KTN.

Kuwasiliana naye: [email protected], FB: Official Jicho Pevu with Mohammed Ali, Instagram: @mohajichopevu, Twitter: @mohajichopevu

Related Topics


.

Popular this week

.

Latest Articles