Seneta Cleophas Malala kupewa ulinzi zaidi kufuatia madai ya maisha yake kuwa hatarini

Inspekta Mkuu wa Polisi, Hillary Mutyambai ameagizwa kumpa ulinzi Seneta wa Kakamega, Cleophas Malala kufuatia madai kwamba maisha yake yamo hatarini.

Mwenyekiti wa Kamati ya Pamoja ya Sheria na Usalama katika Seneti, Yusuf Haji amesema madai yaliyoibuliwa na Malala yana uzito hivyo basi anapaswa kupewa ulinzi haraka iwezekanavyo.

Aidha, wanachama wa kamati hiyo wamesikitishwa na jinsi polisi walimtia mbaroni Malala wenzake Christopher Lang'at wa Bomet na Steve Lelegwe wa Samburu. Hata hivyo, Mutyambai amesema polisi hawakutumia nguvu kupita kiasi kuwanasa maseneta hao.

Haya yanajiri huku Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi, DCI George  Kinoti akisema yuko tayari kuwasilisha vitambulisho vyote vya maafisa wa polisi ili kufanyiwa ukaguzi kubaini waliotishia kumuua Malala.

Akizungumza mbele ya kamati hiyo, Kinoti amesema tayari ofisi yake imepokea picha iliyotumwa na Malala kuonesha maafisa wa polisi anaodai wanapanga kumwangamiza. Hata hivyo, Kinoti amesema uchunguzi wake wa awali umebaini kwamba madai ya Malala ni ya uongo.

Mpema leo, Malala ambaye alizungumza huku akilengwalengwa na machozi amesema maisha yake yangali hatarini akijua kuna polisi watano wanaolenga kumwangamiza.

Wakati uo huo, Seneta Lang'at ambaye pia alikamatwa kwa madai ya kuwachochea wakazi wa Marioshoni Kaunti ya Nakuru, ameelezea jinsi polisi walivyomhangaisha.

Masaibu maseneta hao yalianza baada ya kukamatwa mwezi uliopita kwa kile kilichofasiriwa kuwa kushinikizwa kubadili msimamo wao kuhusu ugavi wa fedha za kaunti.

Ikumbukwe maseneta hao wanapinga mfumo uliopendekezwa na Tume ya Ugavi wa Mapato, CRA kwamba fedha zigawanywe kulingana na idadi ya watu katika kaunti.

Related Topics