IEBC yatangaza Disemba 8 kuwa ya kufanyika kwa uchaguzi mdogo wa Useneta katika Kaunti ya Bungoma

Tume ya Uchaguzi, IEBC imetangaza Disemba 8 kuwa ya kufanyika kwa uchaguzi mdogo wa Useneta katika Kaunti ya Bungoma.

Ikumbukwe kiti cha useneta kilisalia wazi kufuatia kuteuliwa kwa Moses Wetangula kuwa Spika wa Bunge la Kitaifa.

Chebukati amevitaka vyama vya kisiasa kuwasilisha majina ya wanaopendekezwa kumrithi Wetangula kufikia Oktoba 19.

Aidha maafisa wa umma wanaolenga wadhifa huo wanahitajika kujiuzulu nyadhifa zao siku saba baada ya Spika wa Seneti kutangaza wadhifa huo kuwa wazi.

Wanaolenga kuwania wakiwa wagombea huru hawastahili kuwa wanachama wa chama chochote cha kisiasa miezi mitatu kabla ya tarehe ua uchaguzi huo kutangazwa.

Mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati ametangaza wadhifa huo kuwa wazi pamoja na za wadi tano ambazo ni Ololmasani, Kyome/Thaana, Utawala, Mumias Kaskaizini, Gem Kusini katika Kaunti ya Narok, Kitui, Nairobi City, Kakamega na Siaya.

Chaguzi katika wadi hizo ziliahirishwa baada ya wawaniaji wengine kufariki dunia kabla ya uchaguzi kufanyika.

Ikumbukwe uchaguzi mdogo wa Useneta utatarajiwa katika Kaunti ya Elgeyo Marakwet iwapo Seneta wa kaunti hiyo, Kipchumba Murkomen ataidhinishwa kuwa Waziri wa Barabara na Uchukuzi, Garisa mjini Iwapo mbunge wa eneo hilo Adan Duale ataidhinishwa kuwa Waziri wa Ulinzi na Eneo Bunge la Kandara iwapo Alice Wahome ataidhinishwa kuwa Waziri wa Maji na Unyinyiziaji Mashamba.