JSC yamhoji Profesa, Dkt Moni Wekesa

Na Caren Omae,

NAIROBI, KENYA, Profesa, Dkt Moni Wekesa amefika mbele ya Tume ya Huduma za Mahakama, JSC kuhojiwa katika harakati za kumsaka Jaji Mkuu mpya. 

Moni ambaye kwa sasa ni Mkuu katika Chuo Kikuu cha Daystar kitengo cha Uanasheria, ana Shahada ya Elimu kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi vilevile Diploma ya utabibu katika michezo kutoka Chuo Kikuu cha Cologne nchini Ujerumani.

Aidha, ana shahada ya pili katika sheria kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi aliyoipata mwaka 2002 na stashahada ya uwanasheria kutoka Kenya School of Law ambayo pia aliipata mwaka 2002.

Wekesa atakuwa mwaniaji wa tisa kuhojiwa kwa wadhifa wa Jaji Mkuu huku Alice Yano akikamilisha mahojiano hayo Ijumaa.

Hata hivyo, kizungumkuti sasa kina zingira shughuli nzima ya kumteua Jaji Mkuu baada ya Mahakama Kuu kuiagiza Tume ya JSC, kutomteua mwaniaji anayepaswa kupendekezwa kwa Rais Uhuru Kenyatta kwa ajili ya kuidhinishwa.

Licha ya mahakama kuruhusu kukamilishwa kwa mahojiano ya kumsaka Jaji Mkuu, imeagiza kuahirishwa kwa shughuli ya kupendekeza anayefaa kwa wadhifa huo hadi pale kesi zilisowasilishwa kupinga mchakato huo zitakaposikilizwa na kuamuliwa.

Uamuzi huo umetolewa na jopo la Majaji watatu, Anthony Mrima, Reuben Nyakundi na Wilfrida Okwany. Majaji hao aidha wameagiza kusitishwa kwa shughuli ya kuwahoji wawaniaji wa wadhifa wa Jaji wa Mahakama ya Juu, ambayo ilipaswa kuanza Jumatatu wiki ijayo.

Majaji wanasema kuwa rufaa zilizowasilishwa mbele yao na Tolphin Nafula, Philip Muchiri na Memba Ocharo zina hoja nzito ambazo haziwezi kupuuzwa. Miongoni mwa maswala yaliyoibuliwa katika kesi hizo hatua ya vikao vya mchujo kuendeshwa na Naibu Mwenyekiti wa JSC, Profesa Olive aMugenda badala ya Kaimu Jaji Mkuu, Philomena Mwilu.

Mugenda na JSC wametakiwa kuwasilisha utetezi wao. Aidha, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Paul Kihara ameorodheshwa kuwa miongoni mwa watakaowasilisha utetezi. 

Related Topics