Hongera na pongezi kwa Team Kenya

Na, Hassan Ali

Sasa ni wazi kuwa jamvi la mashindano ya olimpiki huko Rio Brazil limekwisha kukunjwa rasmi. Ni hongera na pongezi kwa Team Kenya walioshinda na walioshindwa mradi walishiriki na kujituma kulitangaza jina la Kenya na kuipeperusha bendera ya Kenya. Kenya imemaliza ikiwa bingwa wa bara hili. Huu sio muujiza. Sasa hivi ni nderemo na vicheko vya mursik kwa washindi wa dhahabu David Rudisha mita 800, Vivian Churuiyot mita 5000, Eliud Kipchoge marathon, Faith Chepngetich mita 1500, Conseslus Kipruto mita 3000 kuruka maji na viunzi na kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hii medali wanawake marathon Jemima Sumgong. Walioshinda fedha na shaba twasema ahsanteni. Cha kuzungumziwa maana wahakiki wa michezo nchini hasa riadha, wanasubiri kutoka kwa serikali kupitia wizara ya michezo chama cha riadha nchini na kamati ya taifa ya olimpiki kujua ripoti ya tathamini ya mashindano ya mwaka huu inasemaje. Redio maisha kitengo cha michezo kinajiunga na Wakenya kujua kiini cha meneja Rotich na kocha Anzra kurejeshwa nchini kilikuwa kipi? Je, hali ilikuwaje kambini kabla ya Team Kenya kuondoka nchini na pia hali na mazingira yalivyokuwa huko Rio Brazil.
Je, kilitokea nini kuihusu tiketi ya mshindi wa fedha huko Rio mrusha mkuki Julius Yego na kocha wake? Labda kama angekuwa timamu kiakili na kisaikolojia hapa Kenya ingemega dhahabu? Vipi kuhusu uteuzi wa wanariadha hasa kutokana na aibu tuliopata mbio za mita 5000 wanaume? Kwa nini wanariadha Wakenya wanatorokea mataifa mengine kila kukicha? Kwa nini bonasi za washindi wa dhahabu na fedha huchelewa kutoka hadi kufikia kiwango cha fukuza fukuza?
Hivi, twauliza kujua gharama ya ujumbe uliosafiri Rio Brazil, kila mjumbe alikwenda kufanya nini? Kitengo cha michezo redio maisha kinaomba tu Wakenya kuwajibika au siyo? Maswali haya tutayauliza hadi lini. Rais Uhuru Kenyatta ni wewe ndiye uliyewapokeza bendera ya taifa timu hii ya Kenya kwenda Rio Brazili. Je, hapo ulipo una raha kutokana na hali ilivyokuwa kabla, wakati na baada ya mashindano haya? Naibu rais William Ruto mwenyewe ulikuwa Rio na kushuhudia kwa jicho lako. Je una raha hapo ulipo? Kazi kwako sasa Dr. Hassan Wario? Maswali japo kiduchu ndio hayo ndugu Kipchoge Keino na mwenzio Stephen arap Soi.