Please enable JavaScript to read this content.
Gavana wa Kajiado Dkt David Nkedianye amemsuta mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria na kumtaja kama asiye na maadili yanawafaa viongozi wenye nembo ya ‘mheshimiwa’.
Akizungumza kwenye mahojiano Jumatano asubuhi katika Radio Maisha, Nkedianye amesema kwa wakati mmoja mbunge huyo alitusi viongozi katika eneo la Isinya na kumtaka akome tabia hiyo.
“Yeye ni mheshimiwa lakini nataka akome tabia ya kutusi watu. Ikiwa huna kura mahali kama kiongozi, haimaanishi uanze kutusi watu,” alisema Nkedianye.
Bw Kuria ni miongoni mwa viongozi wa chama cha Jubilee ambao wamekuwa mstari wa mbele kumpigia debe Bw Joseph Olelenku ambaye anawania kiti cha ugavana Kajiado dhidi ya Bw Nkedianye.
Mapema katika mahojiano hayo, Gavana Nkedianye aliishtumu kamati iliyotwikwa jukumu la kuandaa hafla ya maziko ya aliyekua waziri wa usalama wa ndani Joseph Nkaissery.
Nkedianye amesema viongozi waliochaguliwa katika kauti ya Kajiado walikosa kupewa muda wa kuhutubu na kutoa pole kwa familia ya mwendazake jambo ambalo halikuwafurahisha wakazi wa eneo hilo.
Baadhi ya viongozi katika muungano wa NASA walinyimwa ruhusa ya kuingia katika boma la Nkaissery siku chache baada ya kifo chake.