Barua Kwa Raila Odinga

JavaScript is disabled!

Please enable JavaScript to read this content.

MKENYA MZALENDO

KIJANA MPENDA AMANI

Kwa,

RAILA AMOLLO ODINGA

KINARA WA CORD

JAMHURI YA KENYA

 

Bwana Odinga,

MINT: UPINZANI KWENYE MIZANI

Mwaka huu ni wa uchaguzi. Kongole kwa kazi ambayo wewe, pamoja na viongozi wengine mmekua mkifanya nchini; kuikosoa serikali.

Nakubaliana nawe kwa hili: kwamba nchi hii yahitaji badiliko. Ila nina haya ya kukuelea kuhusu harakati za kuleta mabadiliko:

Kwanza kabisa, tambua kwamba wewe, pamoja na viongozi wengine wote, wa upinzani na wale walio serikalini, ni wananchi wa Kenya. Ni muhimu nyote mjue ya kwamba, kando na mamlaka mlio nayo, la kwanza na la msingi ni kwamba ninyi ni wananchi kama wakenya wengine. Hivi ni kumaanisha kwamba shida tulizonazo humu nchini zatuathiri sote sawa na hivyo hapapaswi kuwa na tofauti yoyote.

Bwana Odinga, nchi hii ilishuhudia machafuko katika uchaguzi uliopita. Mwaka huu, tunapojiandaa kwa uchaguzi mwingine, tunataka amani. Huu sio wakati wa kutofautiana na viongozi wengine! Huu sio wakati wa kuendeleza uhasama baina yenu na serikali. Kumbuka wananchi wako macho.

Iwapo kikweli unataka kukomboa taifa hili na kuhakikisha kuwa demokrasia inazingatiwa, usipande chuki mioyoni mwa wananchi. Baada ya tarehe 8 Agosti, Kenya bado itasonga mbele! Yapo maisha baada ya uchaguzi.

Utafanya vema kuelekeza nguvu zako katika kuuza sera kwa wananchi badala ya kupigana vita vya maneno na maonyesho na serikali. Tumia muda wako kuzungumza na wenye nchi. Wao ndio walio na uwezo wa kufanya mabadiliko.

Ziendeshe kampeni zenu kwa njia ya amani, epuka kuwatumia vijana kuzua ghasia.

Yeyote atakayetwaa uongozi baada ya tarehe 8 Agosti anahitaji kufanya kazi ya ziada katika kampeni zake.

Iwapo unataka kuwa tofauti, epuka rabsha; zipo njia nyingi za kupitisha ujumbe. Migomo sio njia pekee ya kusuluhisha mambo. Wengi wamepoteza maisha yao na mali yenye thamana kuharibiwa katika migomo ya hapo awali. Hebu tafakari, ni kura ngapi zimepotea, na ni ngapi zinaweza kupotea iwapo watu watapoteza maisha ovyo katika migomo ya kila mara?

Ni kweli kuwa tunahitaji badiliko, ila, wape wakenya sababu ya kukuchagua wewe kama kweli ndiwe badiliko wanalohitaji.

Zingatia amani, upendo na umoja ili taifa lisirejee katika ile hali iliyokua mwaka wa 2007/08.

Safisha jumba lako na tambua upinzani upo kwenye mizani!

 

Wako mwaminifu

Kijana Mpenda Amani

Mzalendo Daima

Yegon Emmanuel