Barua kwa rais Uhuru kenyatta

Mkenya Mzalendo

Kijana Mpwnda Amani

Tarehe: Kenya Hii Leo

 

Kwa

Rais

Jamhuri ya Kenya

Uhuru Muigai Kenyatta

S.L.P Ikulu ya Nairobi

 

Mtukufu Rais

 

MINT: TAIFA LA WAYAWAYA

Ninasikitika sana! Matatizo chungu nzima nchini! Rais, hapana sababu ya kutabasamu wakati wagonjwa wanakosa kuhudumiwa mahospitalini. Wengi tayari wamepoteza maisha kutokana na mgomo huu wa matabibu.

Hivi majuzi sakata ya bilioni 5.3 za fedha za wizara iyo hiyo ya afya imetokea. Rais, huku ni kuwaibia wagonjwa! Ndicho hasa chanzo cha vifo ambavyo vimeshuhudiwa . Kuhusu swala lote la ufisadi, Rais una nguvu na uwezo wa kuchukua hatua dhidi ya wote wanaofuja fedha za umma. Tangaza msimamo wakenya wakuelewe vema. Rais, samahani ila, ni aibu sana kusema kwamba umeshindwa na la kufanya! Wananchi walikupa jukumu la kulinda mali na fedha za umma. Tumia muda mchache uliosalia kusafisha nyumba yako.

Rais, jinamizi hili la ufisadi ambalo ni ndugu wa karibu na ukabila, limalize kabisa hapa Kenya. Hata kama kwa mara moja, nakusihi Rais, iga mifano ya Rais Magufuli wa Tanzania na Kagame wa Rwanda. Uwe kielelezo kwa wananchi wa Kenya kwa kuchukua hatua madhubuti dhidi ya wote wanaohusika, hata akiwa naibu wako. Ukionyesha dalili za huruma na mapendeleo ama kutojali, vita hivi hatutavishinda karne hii.

Rais, uongozi wa nchi kwa jumla unahitaji badiliko. Uwazi unafaa kuzingatiwa kote kote. Viongozi wote wanapaswa kuwa waadilifu. Ewe, rais, waonyeshe njia, ongoza kwa mfano.

Hali ya maisha yaendelea kuwa ngumu kila kukicha! Uchumi waendelea kuzorota. Vijana hawana ajira! Mliahidi kutengeza nafasi za ajira ila, vijana wengi hawana ajira hii leo. Umasikini umekita mizizi nchini! Wakulima hawapati soko kwa mazao yao kwa sababu ya bidhaa kutoka nje ambazo zinauzwa kwa bei ya chini katika masoko ya humu nchini.

Kabla ya kulalama kuhusu vijana wanaojiunga na makundi ya kigaidi, Rais, zingatia yafuatayo: boresha viwanda vya humu nchini, komesha ununuzi wa bidhaa muhimu kutoka nchi zingine na kisha boresha shirika la vijana NYS ili kuhusisha ajira baada ya mafunzo.

Suala la mazingira! Rais, hapana hatari kubwa zaidi kuliko hili! Msilifanyie mzaha swala la mabwawa ya maji. Msije mkageuza taifa kuwa jangwa huku mkiwafaidi wachache kwa miradi ya maji. Msitu wa Mau kwa mfano, ndio msingi wa mito mingi inayowasaidia wakulima wengi na pia mbuga ya Mara. Miradi hiyo ya Itare, pamoja na ya Murang’a, kwa heshima ya marehemu Wangari Maathai na wakenya wote watakaoathirika, naomba uzisitishe.

Rais, siasa za wala nyama na wale watazamao sio nzuri kwa amani ya taifa. Wakati huu tunapokaribia uchaguzi mkuu zingatia sana kuwaunganisha wakenya. Hatutaki machafuko kama tuliyoyashuhudia baada ya uchaguzi wa 2007.

Mwisho kabisa, ni muhimu kusisitiza kuwa tunataka amani nchini. Lirejeshe taifa katika ile hali iliyokuwa wakati wa hayati babako Mzee Jomo Kenyatta! Hatutaki matata Kenya!

Zingatia shughuli zitakazowaunganisha wakenya wote; anzisha miradi ya maendeleo kote nchini, tengeza nafasi za ajira kwa vijana na muhimu zaidi, angamiza ufisadi nchini. Ndilo jukumu lako hasa.

Uwe kielelezo kwa viongozi , wananchi tufanye sehemu yetu.

Kama vijana, tunafanya sehemu yetu; hatutaki ukabila wala uongozi mbaya.

Safisha jumba lako kwa muda uliosalia. Badiliko laja.

 

Wako Mwaminifu

Kijana Mpenda Amani

Mzalendo Daima

Yegon Emmanuel