Please enable JavaScript to read this content.
Nchi yetu ya Kenya, tukufu ya kifahari
Likombolewa kwa damu Kenya,ya mababu hodari
Lipata uhuru Kenya, ila leo mna hatari
Amkeni ndugu wakenya, tuilinde nchi yetu
Maandamano kila kukicha, machafuko kila mahali
Ya taarifa video na picha, ya vifo vilivyotukabili
Majambazi usiku kucha, waua sawa na ajali
Amkeni ndugu wakenya, tuilinde nchi yetu
Serikali mekosa mwelekeo, vile vile na upinzani
Mauaji ovyo matokeo, maandamano ovyo mijini
Vitoa machozi matoleo, hamna utulivu nchini
Amkeni ndugu wakenya, tuilinde nchi yetu
Stay informed. Subscribe to our newsletter
Wanasiasa situtapeli, kutugawanya wananchi
Mezowea kutufeli, kutulaghai wenye nchi
Kwa vitendo kutukejeli, tulopiga kura wananchi
Amkeni ndugu wakenya, tuilinde nchi yetu
Wanasheria kule bungeni, mejaza sakata tele
Kuvua nguo humo bungeni, filimbi mayowe ndio ndwele
Mesahau sharia za nchini, kuzitunga tusonge mbele
Amkeni ndugu wakenya, tuilinde nchi yetu
Wito huu ni mwamsho, sio wa vita bali Amani
Tusaidiane kufikisha mwisho, uhasama na chuki nchini
Na tufanye hamazisho, la umoja hapa nchini
Amkeni ndugu wakenya, tuilinde nchi yetu
Serikali na upinzani, zungumzeni kwa yakini
Tatueni shida kikaoni, sio kwa askari na mawe mijini
Mwapanda chuki mioyoni, mwa wafuasi wenu nchini
Amkeni ndugu wakenya, tuilinde nchi yetu
Tuungane sote pamoja, viongozi wananchi wote
Tutangamane kwa umoja, tupendane sisi sote
Tuzungumze lugha moja, ya Amani kote kote
Amkeni ndugu wakenya, tuilinde nchi yetu