Please enable JavaScript to read this content.
Hi leo nawaza, nawazua maswala tata
Huzuni menijaza, mauaji ovyo yalowapata
Wakaazi kuwaliza, vilio na huzuni yakata
Serikali yafanyani? Wakenya waangamia
Makala ya jicho pevu, yanayofanya kwa makini
Zaonyesha ulegevu, kwa usalama nchini
Serikali ni nyamavu, wakenya wamo taabani
Serikali yafanyani? Wakenya waangamia
Wana-adamu na hawa, wamegeuka hayawani
Ule upendo na usawa, umegeuka chuki yakini
Ile Amani ya kawa, mepotea tumo vitani
Serikali yafanyani? Wakenya waangamia
Stay informed. Subscribe to our newsletter
Mauaji kule Lamu, sisahau na Mpeketoni
Yalomwagika yote damu,sababu siasa na dini
Manduguna binamu, waangamia hamna Amani
Serikali yafanyani? Wakenya waangamia
Arobaini na saba wote, wanafunzi wa Garissa
Hadi leo twalia sote, utulivu mioyoni kukosa
Za kijasusi habari zote, mlipuuza kwa nini hasa
Serikali yafanyani? Wakenya waangamia
Baada ya upekuzi, upelelezi wa kina
Mwafanya ipi kazi, ama kazi kuhongana
Ya jicho pevu upekuzi,nauliza una maana?
Serikali yafanyani? Wakenya waangamia
Tambueni tumechoka, kwa habari za tanzia
Kila tunapoamka, ajali uhalifu yaua twalia
Zote twaweza epuka, iwapo mtabadili tabia
Serikali yafanyani? Wakenya waangamia
Tamati meshafika, ila kuandika sitachoka
Iwapo tungewajibika, kila mtu bila kuchoka
Tungeweza kuepuka, vifo na kilio liyotughubika
Serikali yafanyani? Wakenya waangamia
https://yegonemmanuel8.wordpress.com