Goldalyn aelezea ndoto zake

Na, Rosa Agutu
Goldalyn aelezea ndoto zake
Mtahiniwa aliyeibuka wa kwanza kote nchini katika Mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Nane, KCPE, Goldalyn Kakuya aliandaliwa hafla ya kusherehekea matokeo yake na Shirika la Watu Wenye Ulemavu wa Ngozi katika Shirika la Kitaifa la Vipofu lililoko eneo la Lang'ata jijini Nairobi.
Akizungumza katika sherehe hiyo, Goldalyn amesema ulemavu hauwezi kuzuia mafanikio katika maisha na watu wenye maumbile sawa na yake wanafaa kuwezeshwa kuafikia ndoto zao maishani. Aidha, amesisitiza kuwa sherehe ya matokeo hayo mama si yake pekee bali jamii nzima ya wanaokabiliwa na matatizo ya ngozi, akiongeza kuwa hahisi kuwapo tofauti baina yake na watu wengine. Vilevile Goldalyn ameahidi kuendelea kuelimisha jamii kuhusu ulemavu wa ngozi.
Mamaye Goldalyn, Matilda Cherono Tanga ameeleza kufurahishwa na matokeo ya mwanawe na kusema hatua hiyo imewapa motisha wenzake. Amewashauri wananchi kuwachukulia watoto kama Goldalyn kuwa sawa na watu wengine na kutowatenga. Kwa mujibu wa Matilda, bintiye alipitia changamoto tele za unyanyapaa.
Babaye Harrison Webo Tanga amewapongeza wote waliofanikisha ndoto ya mwanawe, hasa kumsaidia kukabili changamoto zinazomkumba.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mkurugenzi wa Baraza la Kitaifa la Watu Wenye Ulemavu, NCPWD, Isaac Mwaura amesema watu wanaokabiliwa na matatizo ya ngozi kama Goldalyn wanaweza kuwa watu wa kutegemewa katika jamii. Goldalyn aidha amekabidhiwa hundi, vilevile kupewa nafasi ya kujiunga katika Shule ya Kibinafsi ya Mpesa.
Goldalyn aliyeongoza kwa alama 455 juu ya 500, alizoa alama 99 katika Masomo ya Kingereza na Kiswahili, 85 Hisabati, 88 Sayansi na 84 Somo la Kijamii na Dini, na kusema alitarajia kufanya vyema lakini si kiwango cha kuwa wakwanza katika taifa.

Related Topics