Mpeperusha bendera wa Muungano wa Azimio Raila Odinga sasa anadai kuwa hatashiriki katika mjadala wa Kitaifa wa wawaniaji wa urais na mshindani wake, William Ruto wa UDA.
Msemaji wa kamati ya Kampeni ya Raila Profesa Makau Mutua anadai kuwa mfumo wa mjadala wa marais nchini ambapo washindani wa karibu wanawekwa pamoja kuulizwa maswali si mzuri.
Katika taarifa kwa vyombo vya Habari profes Mutua amedai kuwa mjadala huo wa wagombea wa urais pia haulengi kujadili masuala ya uongozi, ufisadi na maadili ambayo ndiyo yanawahusu moja kwa moja Wakenya.
Badala yake Azimio sasa imesema itashiriki mjadala wa moja kwa moja wa wananchi utakaoandaliwa katika ukumbi wa Jericho hapa jijini Niarobi.
Ikumbukwe, juma lililopita kuliandaliwa mjadala wa wagombea wenza ambao Martha Karua wa Azimio na Rigathi Gachagua wa UDA walikabiliana wakati wa awamu ya pili baada ya Ruth Mutua wa Agano na Justina Wamae wa Roots.
Awali ilidhaniwa kwamba UDA ndiyo ingesusia mjadala huo kwa kuwa mara si moja ilikuwa imevishtumu vyombo vya habari katika kuwabagua hasa katika kuangazia taarifa zao. Alhamisi iliyopita upande wa Kenya Kwanza ulithibitisha kuwa Ruto atahudhuria mjadala wenyewe na kusisitiza usawa.
Mjadala wa Urais umepangiwa Jumanne ijayo, ambapo awamu ya kwanza imetengewa Profes George Wajackoya wa Roots na David Mwaure wa Chama cha Agano. Huku Rila na Ruto wakipangiwa awamu ya pili.