Siku moja nilikuwa nikititazama mchezo wa Bao la Kiswahili, katika mtaa mmoja wa kiswani wa Mwembe Tanganyika mjini Mombasa. Ni zamani sana, ni mwishoni mwa miaka ya 1960. Maskani hiyo ilikuwa ikihudhuriwa na watu wa makabila yote pasipo kubaguana. Palikuwa hapazungumzwi lugha nyingine zaidi ya Kiswahili. Kati ya waliokuja kucheza bao maskani hiyo, walikuwa wamepiga vita vikuu vya pili vya Dunia vilivyokuwepo kati ya 1939 hadi 1945. Kwa tajriba hiyo tu utaona kuwa maskani hiyo wengi walikuwa watu wazima. Mimi kwa wakati huo nilikuwa kijana wa miaka 24 hivi, nikimfuata babu yangu Mzee Msabila ambaye alikuwa manju katika ufundi wa kulicheza bao hilo. Wenyewe wasema mcheza bao anayeweza kupiga duru saba na kuendelea, huyo ni fundi. Licha ya kuwa na miaka hiyo niliootaja, katika maskani hiyo nilionekana mtoto.
Nilikuwa nikitumwa tumwa, hata kupeleka mahitaji muhimu ya nyumbani kwenye nyumba za wazee hao. Naweza kutumwa nipeleke pesa , kitoweo au mbogamboga, samaki, ama nikanunua sigara, tumbaku aina ya ogoro au niende Mwembe Tayari soko la papa kununua papa na kadhalika. Tena sio kama utapewa asante au pole la, Wazee hao waliamini kwamba unatekeleza wajibu wako. Maskani ya watu wazima na wazee panakuwa na wanautani wao wa asili kati ya kabila Fulani na kabila Fulani. Mfano nilijulia hapo kwamba Mnyamwezi kutoka Tanzania ni mtani wa Mkamba kutoka Kenya. Mjaluo na Muhaya ni watani wa jadi Mdigo na Mnyamwezi, Wanyasa walitaniana na Wazaramo na kadhalika. Kulikuwa na matusi yazungumzwa lakini huwezi kujua kama wazungumza matusi kama huji kufumbua. Maana wali? cha sana sisi vijana tusigundue. Hata wakiwa wanamsema mwenzao ili waje kumkanya, basi watatumia ku? cha tusijue.
Mimi nilijifunza mengi sana kukaa na wazee hao, nilisikia hadithi za vita vya Burma, nikajua mkusanyiko wa waafrika wengi huko Burma, ndiko kuliko zua vuguvugu la kuanzishwa kwa harakati za kudai uhuru kutoka kwa wakoloni ilijifunza maadili, maisha ya ndoa heshima utu na adabu. Mzee Msabilia asili yake Tanganyika lakini kaloweya Mombasa Kenya, kaoa na ana watoto wengi tu, ndugu yake Msabilia ndie alie wazaa baba zetu kina Khamsini, nao wakatu zaa sisi. Babu huyo alinambia, tumegawanywa bila ya sisi kutaka. Tukawekewa mipaka kama ng’ombe zizini. Sababu kubwa ni kutufanya tusielewane ili waweze kututawala. Haiyumkini tuwe na wadigo Kenya wadigo Tanzania, Wamasai Kenya, wamasai Tanzania, wajaluo Uganda wajaluo Kenya, wajaluo Tanzania.
Tumelazimishiwa mipaka ya lazima kwa matashi yao, bila kuwauliza wafalme au viongozi wa makabila hayo. Maneno hayo nilitafakari sana nikajiuliza , lakini sikupata jibu zaidi ya kumwambia , lakini tunaelewana. Mzee Msabilia akanicheka sana akanambia mjinga mpumbavu, kwa sasa tutaelewana sana hata hatutoona hilo kosa. Taabu inakuja mjukuu wangu, pale ngozii hii ( akiishika ngozi yake nyeusi) itakapo kuwa huru ijiongoze yenyewe. Mdigo wa Tanga na wa Mombasa kutembeleana itakuwa taabu shida na mashaka. Nikamuuliza kwa nini wakati wao wote ni Wadigo?
Akanijibu, ngozi yetu nyeusi na nyoyo pia nyeusi, tutautafuta na kijitwika ubwana, tuwe mabwana kuliko walio tutawala. Tutabaguana kwa makabila yetu badala ya kuuangana tuwe pamoja. Kila mtawala atapendelea wakwao kwanza ndipo wengine wafuate. Kutakuwa na mashakili kuliko hivi sasa, Mimi kwa wakati huo, nilimuona kama mpinzani wa ukombozi wa bara la Afrika, nikamuona si mmoja wa waswahili wanao taka kuwa huru, nikampuuza. Lakini yale alioyasema Mzee huyo, yameshatokea na mengine bado yanatokea katika nchi mbalimbali za Afrika. Kusema kweli mfano mdogo ulitukuta sisi majirani wawili mpaka kukafungwa mipaka vikawa vitisho karibu tuvaane, Ila Mungu akaliepusha.
Kukosekana umoja
Jumuia ikavunjika tukawa kila nchi na lake. Chanzo ni kile alicho sema Mzee Msabilia cha kujivika ubwana kujali ukwenu na kudharau wengine. Huo ndio uswahili uliozaliwa baada ya kujikomboa. Tumshukuru Mungu leo hii mambo yanaanza kubadilika na watu wameanza kujitambua kwa Ukenya wao na si kwa makabila yao. Umoja wetu huo umeanza kuleta chachu za maendeleo na kuwasogeza karibu majirani zetu ambao walikua baridi nasi, Tumesikia na kuona nia ya kuifanya Jumuia mpya ya Afrika Mashariki ilo? kia miaka ishirini kuwa chombo cha kuondoa yale mawi yote yalio tukingama siku za nyuma, yakatugawanya.
Wamenuia kuwa na umoja thabiti utakao panua soko la bithaa zetu ndani na nje ya jumuia. Wahenga walisema soko la kwanza ni wingi wa watu mlio nao. Unapata soko la uhakika kwa bidhaa mnazo zitengeza ndani ya nchi zetu . Dhamira ya kurahisisha uvukaji mipakani iwe kwa vitambulisho tu. Kuwepo kwa uhuru wa mwanajumuia kufanya kazi katika nchi yoyote kati ya nchi za jumuia.
Na ikiwezekana tuwe na sarafu moja. Utajiri uliopo ndani ya nchi sita zinazo unda jumuia hii ya AFRIKA Mashariki, ni mkubwa mno, kama utatumika vizuri, utakuwa ni ukombozi wa wananchi waliomo ndani ya jumuia hiyo. Hebu tujitahidi kuondoa ukabila ufe kabisa, tuilinde amani tuongeze juhudi nguvu na maarifa, tuwe na utangamano. Tunako kwenda lazima tuta? ka. Hata Mbuyu ulianza kama mchicha. Mswahili bwana!