Majuzi katika kongamano la kitaifa la mchakato wa kuunganisha nchi al maaruf BBI (Building Bridges Initiative) kule Bomas, Nairobi kulizuka mgeni wa nchi jirani aliyehutubu na kuacha maswali mengi kwa wadadisi wa kisiasa.
Bwana huyu ni Waziri wa mambo za nchi za nje wa Tanzania Profesa Palamagamba Kabudi. Sambamba na hulka na sifa za watanzania alitowa hotuba ilosheheni ukwasi wa lugha teule ya Kiswahili na mahanjam mengi ya kiabunuasi. Akibwabwaja kama cherahani ya Mjerumani mfano wa baba yao wa taifa Julius Nyerere bwana huyu mwenye macho makubwa ya kung’ara kama bundi ama paka mwanga alisema mengi ambayo ni ya kutatanisha.
Aidha aliwaomba wakenya waache ukabila na kuungana huku akidai kuwa huo ni ujumbe wa kiongozi wake John Pombe Magufuli ambaye alimtajataja zaidi ya maradufu mfano wa nukuu za kitabu kitakatifu.
‘Hebu simameni na kila mmoja ashike mkono wa mwenzake na kusema hatutaki ukabila’ aliropoka bwana huyu kama aliyepandwa na maruhani ya kikwao na kulazimu waliomo kusimama kama wanajeshi kambini wakiwemo Rais Uhuru,Ruto na Raila. Palamagamba alidai kuwa viongozi hao watatu yaani Uhuru, Ruto na Raila ndio wanaosimamia Kenya.
Je, alimaanisha kuwa bila hawa watatu hakuna nchi? Sidhani. Tukitathmini hotuba ya Palamagamba twaweza kusema kuwa imetoka kwa mtu ambaye hastahili kamwe kusema aliyoyasema. Twasema kuwa Tanzania haina sifa ya kuwapa wakenya mawaidha kuhusu utawala bora ama kuhusu athari za kikabila kwani ina changamoto hizo zinazotokota ndani kwa ndani.
Tukipima Tanzania na Kenya twaona kuwa kuna tofauti kubwa za kihistoria na hususan kmaendeleo iwe kisiasa, kijamii na kiuchumi. Ukweli usio? chika ni kuwa siasa za Kenya ni kali kushinda za Tanzania.
Hii ni kwa sababu wakenya wameelimika zaidi na hivyo kujua haki zao mapema kuliko watanzania. Watanzania wameanza kuamka majuzi kutoka katika maisha ya kale kwani hata elimu yao ni duni. Mwalimu Nyerere atalaumiwa kwa kutozingatia elimu kwa watanzania.
Mwalimu Nyerere alihimiza siasa za kichina za ujamaa na kujitegemea huku akiwadanganya watanzania wakae vijiji vya ujamaa badala ya kujikuza kimataifa. Upande wa Kenya Jomo Kenyata aliboresha elimu kwa wakenya bila hiyana , wivu, uoga ama shaka za Nyerere na wengi wakaelimika huku watanzania wakiboresha lugha ya Kiswahili, Matokeo ni kwa wakenya kuerevuka zaidi na hivyo kujua haki zao mapema kuliko watanzania waliokuwa katika maisha ya kishamba ya kilimbukeni.
Ajabu Nyerere sungura mjanja alielimika hadi chuo kikuu lakini hakutaka watanzania wasome akiho? a wangetisha uongozi na falsafa yake mbovu ya ujamaa ambayo mwisho aliikana na kukiri alifeli !. Swala la ukabila ni la kidunia.Karibu kila nchi kuna ukabila.Kenya ukabila uko lakini umedhibitiwa kwa sababu wakenya wanajali na kulinda nchi yao ingawa ukabila uko.
Kenya haijakuwa kama Rwanda ambapo karibu watu milioni moja waliangamia katika mauaji ya halaiki ya 1984. Tukumbuke Rwanda ni ndogo na ilihusisha makabila mawili tu ya Hutu na Tutsi ilihali Kenya ina makabila takriban 43. Tanzania ina makabila zaidi ya 100. Twaweza kusema changamoto za kikabila ziko kila mahali lakini huzidi katika nchi yenye makabila machache ama moja lenye nguvu na watu wengi linalotaka kutawala makabila mengine.
Idadi ya makabili
Wingi wa makabila Tanzania ambayo mengi ni madogo madogo dhaifu pia hupunguza ukabila tofauti na Kenya ambapo makabila makubwa ni machache lakini yenye nguvu kama wakikuyu na waluo. Ni kinaya kikubwa kwa Tanzania kuwapa wakenya mawaidha ya kuacha ukabila kwani wao pia wana changamoto sufufu za kisiasa ambazo hazijatatuliwa na chama cha kidikteta cha mapinduzi -CCM.
Rais Magufuli anaonekana ni kiongozi wa kiimla ambaye anawahangaisha waandishi wa habari kwani anapenda kusi? wa lakini hapendi kukosolewa. Bwana huyu mfupi wa miwani kama daktari wa kibaniani amelaumiwa na asasi za kulinda haki za binadamu za kimataifa kama AMNESTY kwa kuwatesa , kuwafurusha, kuwafunga na hata kuwaua waandishi wa habari na wakereketwa wa kisiasa.
Swala la sugu la Zanzibar pia ni kero Tanzania kwani wazanzibar wamelalama kuwa hawana haki kwa kunyanyaswa kila uchao hadi kudaI taifa lao huru. Tanzania mpaka sasa wanajikokota katika kutekeleza ama kuwa na katiba ya taifa ilivyo Kenya.Hapa Kenya imekuwa nchi ya pekeeAfrika kuwa na katiba mpya ya wananchi. Ziada ya yote viongozi kwenye utawala wakiongozwa na Rais Uhuru Kenyatta wamewashirikisha wapinzani katika mwelekeo wa taifa kwa mfano Raila Oginga.
Mbona Magufuli hataki kuwashirikisha wapinzani kina Augustine Mrema wa TLP, Freeman Mbowe wa Chadema, Sheikh Shariff Hamad wa CUF alivyofanya Uhuru kwa Raila? Majuzi vyama vya upinzani vilisusia uchaguzi ambapo chama tawala cha CCM kilishinda karibu viti vyote.Kiongozi wa Chadema Freeman Mbowe asema walisusia kwa kunyanyaswa na gandamizi za Magufuli. Kwa hivyo ni unafiki mkubwa kwa kina Palamambanga kuwapa mwaidha wakenya kuhusu uongozi bora na ukabila ikiwa nchi yake inaendeleza uovu huo.Kweli nyani haoni kundule!
Stay informed. Subscribe to our newsletter