Huku mizozo ya ardhi ikiendelea kutafutiwa suluhu kwa udi na uvumba, hasa eneo zima la Pwani kwa ujumla, swala hilo limechukua mkondo mpya baada ya familia moja kutoka Utange kaunti ya Mombasa kulalamikia mawakili wao kunyakua ardhi ambayo walikuwa wanawawakilishia kesi yao ya shamba la ekari kumi katika kijiji cha Maweni sehemu ya Shanzu eneo bunge la Kisauni.
Walalamishi Mzungu Chengo na Thoya Chengo mwenye umri wa karibu miaka 58 na Bahati Thoya Kamandi, wanadai ndio wamiliki halisi wa kipande hicho cha ardhi ambacho waliachiwa na Mhindi zaidi ya miaka 22 Sasa.
Walalamishi hao wanasema wamekuwa wakiishi katika shamba hilo kama wafanyikazi wa Mhindi huyo miaka hiyo yote wakiwa waangalizi wa shamba hilo na walikuwa wameaminiwa na jamaa huyo wa Kihindi Baada ya Mhindi huyo kuwaamini wangwana hawa wawili na kuwa hali yake ya afya ilizorota, ikambidi kuwaita mabwana hawa wawili kuwakabidhi karatasi ambayo aliwaandikia kuwakabidhi wazee hao usimamizi wa shamba hilo hadi pale atakaporudi.
“Na kwa kuwa alikuwa mgonjwa wa ini akawa ni mtu wa kuenda kwa matibabu India na kutuacha sisi kuendeleza kazi za shamba,” akasema Mzungu.
Mhindi huyo yadaiwa alikuwa na mtoto mmoja wa kike naye pia alikuwa anaishi Marekani na hakuwahi hata siku moja kuja hapa nchini kufuatilia mali ya babaake ambaye yaaminika kwa sasa huenda ikawa aliaga dunia.
“Mimi na mjombaangu tuliitwa na mhindi akatuandikia karatasi akatukabidhi hili shamba, lakini kwa sababu ni kitambo sasa ile karatasi ya kuonyesha tulikabidhiwa hili shamba ikapotea, ikabidi tuende kwa chifu atuandike barua upya ya kuonyesha sisi ndio watu halisi ambao tuliachiwa hili shamba”.
Hata hivyo kulingana na barua ambayo PAMBAZUKO iliipata inaonyesha kuwa naibu chifu wa Shanzu Athman Fondo aliandika barua hiyo na kuiweka sahihi mnamo Agosti 8 mwaka wa 2014, huku baadhi ya maelezo ya barua hiyo yakisema; “This is to certify and confirm that Mzungu Chengo and Bahati Thoya are the onwers of a shamba /land (in surveyed) within the area of Utange-Maweni Village of Bamburi Location. They have been residing and cultivating there shamba with three families for more than 22 years.” mwisho wa nukuu.
Barua hiyo iliandikwa kwa nia ya kuanzisha na kufuata Sheria kama inavyohitajika kwa sababu shamba hilo tayari lilikuwa limeanza kunyakuliwa bila wao kujua ni nini kilichokuwa kikiendelea wakati huo.
Walipoona hali imebadilika na shamba hilo likaanza kupimwa vipande na kugawanywa bila fahamu zao, ikawabidi kukimbilia mahakama na barua hiyo kutoka kwa naibu chifu ili mahakama itoe agizo la kusitisha kugawanya kwa shamba hilo.
Mahakama inayohusika na ardhi kweli ikatoa agizo hilo la kusitisha kugawanywa kwa shamba hilo pamoja na kusimamisha shughuli zozote katika shamba hilo mwaka wa 2016 hadi pale kesi itakaposikilizwa na kuamuliwa.
Baada ya hayo yote kufanyika wazee hao waliendewa kinyume na mmoja wa karibu wa familia yao Goerge Kitsao Chengo ambaye kwa njia isiyojulikana aliandika hati kiapo kudai kuwa yeye ndiye mmiliki halisi wa shamba hilo kupitia kwa wakili ambaye yadaiwa alimfunza jinsi ya kuandika hati kiapo hiyo “laghai.”
Kulingana na Bahati kupitia wakili wake Ratemo, ambaye alikuwa akitumia ofi si ya wakili Andrew Mandi, aliandika hati kiapo ya kubatilisha hati kiapo ya George Kitsao Chengo ambaye anadai yeye hajawai kukanyaga na kuishi katika shamba hilo .
Na wakati wa kuandikwa kwa hati kiapo hiyo, yeye alikuwa bado mwanafunzi wa shule ya msingi mwaka wa 1980. Inadaiwa George alipewa vipesa na wakili wake ambaye yaaminika pakubwa alitumia hati kiapo hiyo “laghai” na kuanza kujinufaisha na aridhi hiyo hata licha ya mahakama kusitisha ugawaji na shamba hilo.
Vile vile baada ya wazee hao wawili kuanza kesi wakili wao aliwashauri kuuza kipande cha ardh, ili wapate pesa za kusukumia kesi yao na baada ya kuuza, sehemu ndogo ya shamba hilo na kumpa wakili shilingi elfu mia moja na themanini mambo yakazidi kuharibika.
Wakili wao anadaiwa kufanya mambo bila kuwahusisha tena na wale hawakuitwa na wakili huyo kuhudhuria hata kikao kimoja cha kesi yao.
Stay informed. Subscribe to our newsletter
“Baada ya kulipa kiwango hicho cha pesa wakili wetu hatukumuona tena, hajawahi hata siku moja kutuambia tarehe ya kesi imefi ka, na hata kwa sasa hatujui kesi inaendelea namna gani. Kile tunachoona ni shamba letu kuuziwa mabwenyenye bila fahamu na hii nyumba tulimokuwa tukiisha pia tumefurushwa,” akasema Bahati.
Wanahofu kuwa mawakili wao kwa sasa, ambao ni zaidi ya watatu, waliwaendea kinyume na wao kuhusika pakubwa katika kuvamia shamba lao.
“Tukiwafuata mawakili wetu Ratemo, Mogaka Omwenga hatuwaelewi wamekuwa wakituzungusha huku na kule bila ya sisi kufahamu nia yao. Kwa hivyo sisi tunataka haki itendeke na ile kesi ya mwaka 2016 tunataka ianze upya kwa sababu imetuweka gizani, tunamuomba waziri wa ardhi aingilie swala hilo,” akasema Bahati.
Waziri wa ardhi Waziri wa ardhi Farida Karonery hata hiyo alihusika pakubwa katika kufuatilia shamba hilo ili kutatua mzozo ulioko kwa sasa.
Kulingana na mtetezi wa maswala ya ardhi eneo hilo Eliud Otieno, Waziri Karonery aliwashauri kufuatilia shamba hilo katika afi si za ardhi eneo la Pwani. Ilibidi afuatilie, baada ya kugizwa na waziri huyo. Ilimlazimu Otieno kufuatilia swala la aridhi hiyo katika afisi za Mombasa akaelewa shamba hilo lilikuwa katika umiliki wa mhindi huyo kwa jina la Poutry Farm Care baada ya kubadilishwa hadi kwa Goerge Kitsao Chengo ambaye yaaminika alitumiwa na mawakili kuandika hati kiapo “laghai”.
Otieno anadai kuwa ametafutwa na mawakili hao ili walemaze juhudi zake kwa kuwa ameonekana kuwa msitari wa mbele kutetea ardhi hiyo.
“Kesi ya hii shambani ni tata sana, hawa mawakili wamekuwa wakitumia mabwenyenye na kuwauzia shamba hili, wameniita katika hoteli moja tukazungumze lakini mimi nimekataa. Nataka tukutane mahakamani na hii kesi izungumziwe huko, sio kwenye mahoteli,” akasema Otieno.
Kwa upande wake wakili Ratemo anasema kesi hiyo iko mahakamani ingali bado inaendelea na akawataka wateja wake kuwa wavumilivu.
“Kesi iko mahakamani na katika shamba hilo kwa sasa hakuna kitu chochote kinachoendelea, tunaifuatilia na wateja wangu wamekuwa wakihudhuria vikao mahakamani, lakini mahakama zilikuwa hazikai kusilikikiza kesi hiyo,” akasema Ratemo.