Vita baridi dhidi ya miraa na muguka vyazuka

Loading Article...

For the best experience, please enable JavaScript in your browser settings.

Mchuuzi akishika kifungo cha miraa katika soko. Kuna uhasama kati ya wafanyibiashara wa miraa na wale wa Muguka kutoka Embu na Meru.

Ni asubuhi na mapema na wazee wawili wanawasili katika soko la Kiamuringa katika sehemu ya Mbeere ya kusini kaunti ya Embu wakibebamagunia mawili yaliojaa huku shamra shamra za ununuzi wa miraa aina ya Muguka ukiendelea.

Bw Njuki ambaye ni mnunuzi wa jumla wa Muguka anafungua gunia moja na kuanza kukagua miraa huku mazungumzo yakipamba moto kati yake na wazee hawa.

Anaingiza mkono katika mojawapo ya magunia mara kadhaa huku akitoa mabunda ya bidhaa hii na kuitizana kwa  makini. Anafanya hivyo hivyo kwa gunia la pili na baada ya kuungiza mkono katika kina cha gunia kutoa bunda kubwa bila kusita anasema, “aaahhh kwani ni majani haya ama ni Muguka gani mumeleta sokoni leo jamani mbona mliachiliwa miraa iharibike?” anauliza Bw. Njuki.

Baada ya dakika kadhaa za kukagua bidhaa hiyo katika magunia yote mawili, mnunuzi huyu anatoa bunda kwa gunia na kulitupa barabarani kwa hasira huku akitangaza kuwa hatolipa hata peni moja ama hata kuichukuwa miraa hiyo.

Huku wazee husika wakimtazama kwa huzuni, punde si punde mfanyabiashara mwingine anaaza kukagua miraa maguniani na bila kusita kuwaeleza wazee husika wamwage bidhaa ili kuhifadha magunia matupu kubebea miraa siku zijazo.

Kwa hasira, mzee James Njeru ambaye in mmoja wa walioleta miraa hiyo sokoni anachukuwa magunia hayo moja baada ya lingine na kumwaga miraa yote katika shimo la takataka.

“Jana tu hawa wafanyi biashara wa jumla walikuwa wakinunua miraa kwa Sh100 kwa kilo, vipi leo, mbona madharau,” anauliza Bw. Njeru.

“Wewe huoni mvua imezidi, kila shamba la miraa sasa linanawiri na lazima uvune miraa yako wakati unaofaa usiachilie iwe mirefu,” mfanyi biashara mwingine wa jumla wa Miraa Peter Ndengu anamwekeza.

Mvua kubwa ilionyesha katika kaunti ya Embu imesababisha kuongezeka kwa miraa na kusababisha bei kuteremka kwa kiasi cha kutisha.

Kuongezeka kwa utafunaji wa Muguka katika kaunti nyingi nchini na mataifa jirani kama vile Somali kumechangia kuongezeka kwa kilimo na biashara ya mumea huu ambao unashindana kiasi cha haja na miraa ya kaunti ya Meru.

Hivi majuzi kulitokea fujo kati ya wafanya biashara wa Embu na Meru kutokana na mashindano ya biashara kati ya Miraa na Muguka katika soko la Kamuketha mjini Embu.

Wafanya biashara wa miraa wa kutoka Meru wamekuwa wakilaumiwa na wale wa Embu kwa kununua Muguka na kuchanganya na majani kutoka katika miraa ya Meru na hivyo basi kawaharibia wafanya biashara wa Muguka kazi zao.

Watumizi wa miraa ya Meru kwa kawaida hutafuna ngozi ya mumea huo, huku wanaotumia muguka wakitafuna majani kama yale ya majani chai.

Kinachowavutia zaidi wakazi wa Embu na Kirinyaga kujitosa katika kilimo cha Muguka ni biashara yake kwani isipokuwa wakati wa mvua ambapo mavuno uongezeka na kuwalazimu wakulima wachache kutupa mavuno yao kwa kawaida Muguka unauzwa kwa haraka punde tu unapofikishwa sokoni. Wakulima wanakili kuwa hata kama mashindano ya wanunuzi wa jumla kunachangia kuweko kwa bei tofauti kwa kila kilo ya Muguka kila mkulima anayefika sokoni hurejea nyumbani na tabasamu usoni mbali na kuwa na pesa mfukoni.

“Sipendi kuwasikia wakulima wa Muguka wakilalamikia bei mbaya za Muguka kwani mbali na bidhaa nyingi za kilimo wanazojihusisha nazo hakuna bidhaa yoyote inayofikishwa sokoni na kuuzwa kijumla baada ya dakika chache tu tena kwa bei za kufurahisha,” anasema mkulima Bw Kigondu Ndavano.

“Ingawa wakati wa mvua wakulima hawatumii maji na madawa ya wadudu kama wakati wa kiangazi hata hivyo kunawili kwa mumea huu kumesababisha kuvurika kwa Muguka katika masoko ya Embu, Mbeere na Kirinyaga,” anasema Bw Lenny Njiru.

Changamoto kuu Jambo lingine ambalo linawatatiza wakulima ni malipo kwa wanaovuna miraa.

Kwani ni lazima walipwe hata kama bei ziko  chini kiasi cha kutoweza hata kulipia nauli kufikisha bidhaa hiyo sokoni.

Hali hii inatatiza sana wakulima kwani asilimia kubwa ya Muguka huvunwa nyakati za usiku katika mazingara ya baridi na mvua.

Hata hivyo wakulima wanasema kuwa Muguka ni lazima uvunwe kwa haraka kila baada ya wiki moja la sivyo majani yanarefuka na kuegeuka rangi kuwa kijani kibichi na ilhali ikiwa michanga huwa na rangi kati ya dhahabu na nyekundu Wanaofanya kazi za kuvuna Muguka mara nyingi huongeza bei za kila kilo ya Muguka wanayovuna kwa kutilia maanani bei za mauzo.

Wakati wa msimu wa kiangazi bei za Muguka huwa nzuri hata kwa wakulima lakini wafanyi biashara wa jumla yaelekea huwania asilimia kubwa za  faida kiasi kwamba wakati kilo ya Muguka inapofikisha Sh1200 mashambani huko Nairobi hufikisha hadi Sh 3,000.

Wakati wa kiangazi wakulima hulazimika kutumia kiasi kikubwa cha fedha kunyunyizia Muguka maji na madawa ya kukabiliana na wadudu na baridi ingawa pia faida huwa za kufurahisha.

Kwa kuwaida ni wakulima walio na maji ya visima ama walioko karibu na mito ambao hunufaika zaidi kutokana na biashara za Muguka.

Haya ni kwa sababu  wengi hutumia maji ya mfereji na yenye kuuzwa kwa bei za juu kutoka kwa kampuni ya uenezaji maji wa Embu yaa Ewasco.

Utumizi wa maji ya Ewasco kunyunyizia Miraa maji ni hatia na wanaopatikana hupigwa faini ama kukatiwa maji. Kwa kawaida kumwagia miraa kiasi cha mimea 800 maji mara moja kwa wiki hugharimu mkulima takribani Sh2000 huku mauzo ya mavuno baada ya wiki yakiwafaidi kwa zaidi ya Sh8,000.

Imarisha biashara Ukulima wa Muguka siku za hivi karibuni umechangia kuongezeka kwa kiasi  kikubwa cha biashara ya usafirishaji wa maji ya kilimo kwa magari.

Katika sehemu ya Kusini mwa Mbeere wakati wa msimu wa kiangazi wa hivi majuzi wakazi waliwekeza katika magari zaidi ya 50 aina ya kanta yaliowekwa matangi ya plastiki ya maji mawili yenye lita 3000 kila moja. Kila lita 3000 zilikuwa zikiuziwa wakulima kwa Sh. 2500 huku kila gari likiwa na wafanyakazi wawili wa kumwaga maji hayo moja kwa moja katika mashamba ya Muguka kwa kutumia mashine.

Utafiti uliofanywa na Pambazuka unaonyesha ya kwamba kuna magari fulani yaliokuwa yakisaidia wekezaji kujipa hadi Sh50,000 kila siku kuuza maji. Faida za uuzaji wa maji pamoja na uajiri uliokuwa unatolewa na biashara hiyo ulichangia vyema uchumi wa sehemu za kusini mwa Mbeere mbali na faida za moja kwa moja kwa wakulima wa Muguka waliojivunia faida kocho kocho.
Miaka iliopita mumea wa Muguka ulikuzwa kwa kiasi cha chini sana katika sehemu za Mbeere Kusini na kutumika kwa kiasi chini mno nje ya kaunti ya Embu.

Lakini hivi leo utumiaji wa Muguka umezidi na kuenea katika kaunti zote nchini Kenya na hali hii inaendelea kuchangia kupanuka kwa kilimo na biashara hii.

Kumekuwa na wengi wanaopinga kilimo na utumizi wa Muguka huku wakiutaja kama dawa ya kulevya na kulaumu watumiaji kama wapenda starehe zinazochangia kupoteza kwa wakati.

Lawama zimekuwepo pia huenda aina fulani ya Muguka hutatiza nguvu za kiume lakini usiku na mchana ukulima, uuzaji na utumiaji wa Muguka unapanuka na kuendelea kuchangia  udhabiti wa uchumi wa wakazi wa Embu na kwingineko.