Sokwe aliyetumia dawa za kupanga uzazi sasa azaa

Loading Article...

For the best experience, please enable JavaScript in your browser settings.

Kisa cha hivi majuzi kimewafanya wanasayansi kujikuna vichwa huku wakijiuliza vipi sokwe jike lilokuwa kwenye mpango wa dawa za kudhibiti uzazi alipata mimba na kujifungua mtoto.

Haya yametokea katika hifadhi moja ya sokwe huko Uganda katika kisiwa cha Ngamba eneo la ziwa Victoria.

Kinacho waumiza watafiti vichwa ni kwamba kwenye hifadhi hiyo, watoto wanne pekee wa sokwe ndo wamewahi kuzaliwa kwa kipindi cha miaka 20 iliopita.

Kwa mujibu wa wasimamizi wa kisiwa cha Ngamba, hali hiyo wamekuwa wakiiona kama kithibitisho kwamba mpango huo wa dawa za uzazi kwa masokwe umekuwa ukifanya kazi. Sasa swali limezuka, je, iweje sokwe huyu anayefahamika kama Natasha kashika mimba na kuzaa? Kulingana na msimamizi wa hifadhi hiyo, ni sera ya mahala hapo pa hifadhi ya kuwasaidia sokwe majike wasizae ili kudhibiti idadi ya wanyama wao kwa sababu hawana uwezo wa kulea idadi kubwa kwenye hifadhi hiyo.

‘’Sawa na binadamu, sokwe wa kike wanatumia dawa za kupanga uzazi ili kujilinda na mimba zisizotarajiwa. Mbinu hii hutumiwa kudhibiti idadi ya sokwe katika hifadhi hiyo iliyotengwa kuwatunza wanyama mayatima,’’ Titus Mukungu, ambaye pia ni daktari wa wanyama, aliiambia BBC.

Kufuatia kuzaliwa kwa mwana sokwe huyo wa mama Natasha mnamo mapema Septemba, sasa idadi ya sokwe katika hifadhi hiyo imefikia 50.

Kisa hicho kinachoonekana kutatiza uthabiti wa kisayansi unao aminiwa kwa matumizi ya dawa za kupanga uzazi, sasa kimewasukuma wahifadhi hata kufanya uchunguzi wa vinasaba, almaarufu DNA, ili kubaini uhalali wa mimba ya Natasha na pia kwa nini alibeba mimba.

Akifafanua zaidi kuhusu sera ya hifadhi hiyo ya upangaji uzazi kwa masokwe, msemaji wa hifadhi Dorothy Masemera alieleza kwamba kisiwa cha Ngamba ni kidogo na ndio maana idadi yao inadhibitiwa.

“Pia tuko na mpango wa kuwarudisha msituni baada ya miaka michache ijayo,” alisema Masemera.

Ripoti hiyo ilizua mchanganyiko wa mishangao, kejeli na misuto hasa mitandaoni ambapo watu wa tabaka mbalimbali walimimina hisia zao kwa kisa hicho.

Wengi waliudhiwa na fikira kwamba iweje binadamu amejitundika kazi ya kuamua kwa niaba ya wanyama, huku wakiona maamuzi hayo kama ukanyagaji wa haki za wanyama.

“Alicho kipanga Mungu binadamu hawezi kukipangua. Huyo sokwe ana haki ya kuzaa, wanao mkataza kuzaa mbona wao wana familia zao,” alikashifu Baraka Faustin.

Kitura Pastory naye alitaka mhudumu wa sokwe huyo kuchunguzwa. “Anaye mhudumia kutumia dawa za uzazi ndiye baba ya hiko kitoto,” alisema.