Please enable JavaScript to read this content.
Miaka nenda miaka rudi, kivuko cha Likoni Ferry kimekuwa kikifanyiziwa tambiko maalum na Wazee wa Kidigo ambao wamekuwa na jadi zao za kimila kwamba pepo wa bahari lazima kufanyiwa karamu yao kwa kuchinjwa ng’ombe mwakani na kutupwa ndani ya bahari hindi.
Kulingana na wazee hawa, tambiko la kumwaga damu baharini hususani katika kivuko cha Likoni ni kuepuka majanga ya maafa ama ajali za kufa maji ambazo wahenga huamini kuwa endapo matambiko ya aina hiyo hazitekelezwi kwa wakati ufaao, pepo hao wa baharini huja kama nuksi kusababisha ajali ya aidha gari kuzama na watu baharini au mtu kujirusha majini bila simule.
Itakumbukwa kwamba mnamo mwaka 1986, kabla ya janga la ajali ya feri ya Mtongwe ya mwaka wa 1994 ambapo tuliwapoteza watu zaidi ya 270, kulikuwa na vituko katika kivuko cha Likoni.
Kumbukumbu hiyo ya mwaka 1986 inaeleza kuwa siku hiyo feri ilikwama katikati ya bahari baada ya kizuka aina ya mtu kuchomoza mbele ya feri na kusababisha ikwame kwa masaa 12.
Walioshuhudia kisa hiki wanashangaa mpaka leo kwamba kizuka huyo alichomoza mbele ya feri huku hajulikani amesimama vipi ndani ya maji ama amemea vipi mpaka kusimama kidete huku akiwa amevalia fulani aina ya vesti.
Tambiko Jitihada za idara husika za halmashauri ya bandari na jeshi la maji wakati huo, hazikufua dafu kwani mtu yule kizuka hakuwa anaongea wala kupepesuka macho.
Ndani ya feri, halaiki ya watu waliokuwa wamejawa na wasi wasi mkubwa waliomba mung una kujiona ni kana kwamba wamo ndotoni. Iliwabidi wahusika kuwasiliana na Wazee wa Kidigo ambao walifanya kikao cha dharura na kutoa uamuzi kwamba kweli, kulikuwa na haja ya kufanya tambiko ambazo awali walikuwa wamezipuuza.
Na kweli maisha ya watu waliokuwa ndani pamoja na feri yenyewe, waliona afueni punde baada ya wazee hao kutimiza masharti ambayo wanaamini kwamba “Bahari inao wenyewe” wanaodai mara kwa mara.
Kulingana na mzee mashuhuri wa Likoni ambaye hakutaka jina lake litajwe, anasema kwamba kutoka wakati huo, wamekuwa wakitimiza tambiko hizi lakini kadiri muda unavyodizi kuyoyoma na rika la wazee halisi kuaga, sasa kuna hatari kwamba visa vya aina hii katika kivuko cha Likoni lazima vizushe wasi wasi.
“Siku hizi hakuna wazee wa kutosha kujadili suala hili na hali ya uchumi pia umewalemea wengi hakuna mtu wakati huu anaweza kujitolea kutoa ng’ombe ama kuon goza mchango wake kwa sababu ya tambiko kama zama zetu,” azungumza Mzee mwenye hisani.
Anaendelea kusema kwamba anasikia kuwa mara kwa mara usimamizi wa feri hujaribu kutolea karamu pepo hawa wa baharini kwa kuchinja vibuzi alfajiri na kisiri lakini kulingana na utaratibu wa wazee wa mila za Kidigo, huwa kunazo kanuni na masharti ya kufuatwa kikamilifu.
Kufuatia kisa cha mapema wiki hii cha mama na mwanawe kuzama na gari lake baharini, kumezua tena suala nyeti hili na wengi kujiuliza iwapo hivi ni visa vya kawaida ama ni mvuto wa kafara kutoka kwa pepo wa baharini, wengine wakawaita majini.
Kabla ya mama na mtoto kuingia baharini baada ya gari lao kurudi kinyumenyume, hali kadhalika kumekuwa na visa vinginevyo vya aina hiyo hapo mbeleni.
Afisa mmoja wa halmashauri ya bandari (KPA) hali kadhalika aliingia baharini mfano huo huo na gari lake pasipo kuchunguzwa chanzo halisi cha ajali hizi.
Dereva Kombo
Stay informed. Subscribe to our newsletter
Mnamo miaka ya sitini, basi zima la waimbaji wa kwaya kama alivyoimba marehemu Fundi Konde kwamba likiendeshwa na Dereva Kombo, liliangamia baharini baada ya kushindwa kupiga breki ufuoni likivuka.
Kutoka wakati huo, visa vimekuwa vingi na badala ya kuelekezana vidole vya lawama kwa wasimamizi wa shirika la huduma za feri (KFS), Jeshi la Majini (Kenya Navy), KPA na Coast Guard, pia kuwepo na kikao cha dharura na wazee waliobaki wa Kidigo kuulizana ushairi hata uwezekano wa kuzienzi tambiko ambazo zimekuwepo miaka yote.
Mvuto wa pepo
Siku moja, yapata miaka minne hivi iliyopita, nilikuwa ndani ya feri yapata mwendo wa saa mbili unusu usiku. Haya ni masaa ambayo ukiwa unatokea bara ya Likoni kuelekea kisiwani Mombasa, huwa hamna abiria wengi kama ilivyo kutoka upande wa kisiwani.
Ndani ya feri, niliongozwa na mpanga magari ferini kuegesha upande wa kushoto ukitoka upande wa Likoni unaoangaliana uso kwa uso na bandari kuu ya Kilindini. Mbele yangu kwenye kisugu cha kukazia kamba (pondo) ya feri inapoegeshwa, kulikuwa na mwanamke wa makamu ameketi, aliyevalia rinda jekundu na mfuko wake wa nguo kando ya miguu yake.
Vazi lake lilinijia kwa haraka mno kuwa ulikuwa ni wakati wa wapendanao kwa jamii ya Wakristu maarufu kwa machekibobu wengi (vijana) kama “Valentine Day”.
Kwenye upande alioketi dada yule, kulikuwepo pia na abiria wengine sawia na mimi lakini sote tulipigwa na bumbuazi kuhstukia chubwi! Kwenye maji.
Tuliokuwa karibu sote tulishikwa na bumbuazi kwani feri ilikuwa imefi ka katikati ya bahari na mwanamke yule amejitosa baharini mfuko wake ukiwa pale pale ulipokuwa.
Mara wahudumu wa shirika la feri wakaleta mashua ya kumsaka mwanadada yule pasipo mafanikio hivyo mfuko wake ukakabidhiwa maafi sa wa usalama wa feri.
Kufuatilia kisa hiki siku ya pili yake, niliarifi wa kuwa mwili wa mwanamke huyo aliyejitosa baharini usiku nikishuhudia kwa macho yangu mawili pamoja na abiria wengine, ulipatikana umesombwa na maji masaa 24 baadaye.
Visa vya Feri
Kwa wale wanaovuka kila siku katika kivuko cha Likoni, visa vya aina hii kwao ni jambo la kawaida. Wale ambao wameokolewa wakijirusha baharini, huonekana kujawa na bumbuazi na kutoa sababu fi nyu za kujitaka kujitoa roho wenyewe.
Kunao ambao wameokolewa na kushtakiwa mashtaka ya kutaka kujitoa uhai. Wengine husingizia wamechoshwa na maisha, baadhi yao hawajui wafanyalo lakini ni kwa sababu gani kuwepo na hofu ya aina hii?