Huku athari za sera tata ya serikali kuu kulazimisha usafirishaji mizigo inayowasili bandari ya Mombasa kupakiwa hadi Nairobi kwa njia ya reli ya SGR ikizidi kubainika, mjadala kuhusu hilo unazidi kupamba moto kila uchao. Pigo la uamuzi huo haswa kwa uchumi wa mji wa Mombasa, pamoja na miji mengine kwa jumla inayotegemea mtiririko wa biashara kutokana na usafirishaji makontena kwa njia ya barabara, umekuwa mfano wa zimwi litakalodhuru sehemu hizo kwa muda mrefu siku za usoni. Huku mjadala huo ukiwavuta wadau wa nyanja mbalimbali husika, baadhi yao sasa wanaonekana kutilia shaka hususan uaminifu wa wajumbe wa kisiasa kuambatana na misimamo yao katika suala hili.
Ripoti iliyotolewa majuzi na Chuo Kikuu cha Nairobi ikiangazia athari na mustakabali wa kiuchumi na kijamii kutokana na mfumo huo tata, imebainisha wazi Mombasa inapoteza mng’aro wake kama kitovu cha biashara na ajira. Kwa mfano ripoti hiyo inatabiri kwamba zaidi ya watu 8000 Mombasa wanaotegemea mkate wao wa kila siku kutokana na biashara za bandari ndogo, shughuli za mawakala na usafirishaji wa barabarani huenda wakapoteza kazi zao.
Vile vile uchunguzi huo unaashiria kwamba kaunti ya Mombasa imepoteza hadi shilingi bilioni 17 tangu amri hiyo ya SGR ilipoanza kutekelezwa. Ni hali halisi namna hii ambayo imepelekea kuzuka kwa ngurumo za malalamishi aidha kutoka kwa wafanyi biashara, mashirika ya kijamii ama viongozi wa kisiasa wote wakionekana kukubaliana kwamba hatua hiyo imezorotesha siha ya kiuchumi na kijamii Mombasa na pwani pia. Hata hivyo wengine wanahisi kwamba hususan viongozi wapwani wa kisiasa wamekuwa kama ndumakuwili katika msukumo huu wakiwa guu moja ndani guu jengine nje.
Akiongea hivi majuzi wakati wa maandamano ya kupinga uamuzi huo wa serikali kuu, Mkurugenzi Mkuu wa shirika la utetezi wa haki za kibinadamu Hussein Khalid alieleza kufa kwake moyo na uongozi wa kisiasa wa jimbo la pwani ambao umeshindwa kutetea vilivyo masilahi ya wakazi.
“Kutoka waleo tunatangaza kwamba Mombasa haina viongozi walio chaguliwa na wananchi ambao wanaweza kutetea watu wao,” alisema mkuu huyo wa Haki Africa. Hakuwachia hapo tu, kwani pia alifananisha uchangamfu wa wajumbe wa kisiasa wa pwani katika jambo hili na ule wa viongozi wa jimbo la Bonde la Ufa kwenye mzozo wa uvamizi wa msitu wa Mau. Alisema kwamba viongozi wa Bonde la Ufa wamesimama kidete kuwatetea watu wao japokuwa wanadaiwa kuuvamia msitu huo kinyume cha sheria, akimaanisha kwamba kwa kufanya hivyo angalau viongozi wale wanatetea masilahi ya wananchi wao. Kwa kifupi, Hussein Khalid anaonekana kuwakashifu wanasiasa wa Mombasa na pwani aidha kwa usaliti ama uzembe.
Mchanganuzi wa siasa, mwanaharakati na mtangazaji Stambuli Abdillahi Nassir pia ni mmoja wa wakereketwa wanaotilia shaka misimamo ya baadhi ya wanasiasa wa pwani katika harakati zinazo ambatana na suala la SGR. Stambuli ametia doa mienendo ya wajumbe wapwani ikizingatiwa kwamba wao ndio walifaa kuwajibika mapema katika kuwaelimisha na kuwatayarisha watu wao kwa muda mrefu tangu SGR ilipoanza kupangwa na tangu ilipoanza kujengwa.
Lakini badala yake, anasema wanasiasa wamejitokeza sasa kuenua sauti zao wakati ambapo mambo yameshaharibika. “Wanasiasa mara nyengine malengo yao sio mazuri, na bila ya umma kutafakari na kuchunguza hili suala vizuri ni rahisi watu kutumika vibaya na wanasiasa,” alihoji Stambuli Abdillahi Nassir katika kipindi cha uchambuzi kwenye stesheni moja ya redio. “Yakulaumiwa sio serikali, hichi kitu ni baina ya wajumbe kulemaa kimawazo kwenye kuwaelimisha raia katika miaka 11 iliyopita (tangu 2008 mradi wa SGR ulipo pendekezwa) ingawa wao wamo kwenye kamati husika (za bungeni) pamoja na wabunge wenzao ambao hawamo kwenye kamati lakini wamo ndani ya bunge,” alieleza. Hoja yake kuu ni mipango ya serikali haianzishwi tu ghafla. Anasema kwamba kanuni ya kiserikali huhitaji miswada ya miradi kujadiliwa na kupitishwa bungeni kwanza kabla ya kuidhinishwa rasmi.
“Ili kuelewa suala la SGR vizuri ni muhimu mtu aone ripoti mbili za kamati za bunge ambapo baadhi ya hawa wabunge wanaoongea (hivi sasa) walikuwemo kwenye kamati hizo,” anasema, akimaanisha ripoti za Kamati ya Uwekezaji (PIC) zilizoangazia mradi wa SGR 2014 na ambamo wabunge wawili wa pwani walikuwemo kwenye vikao hivyo.
Japo wabunge pia wanalalamika kwamba maamuzi ya serikali kuambatana na mfumo huo wa kibiashara kulazimisha utumiaji wa SGR kwa usafirishaji makasha ulifanywa bila ya wao kuhusishwa. “Hakukuwa na uhusishaji. Sisi tunawakilisha wananchi na ingekuwa serikali imetuongelesha na tungeweza kuwashauri njia gani nzuri ya kufuata,” alisema mbunge wa Lunga Lunga Khatib Mwashetani wiki iliyopita.