For the best experience, please enable JavaScript in your browser settings.
Hofu imeanza kuwaingia wafuasi wa chama tawala cha serikali cha Jubilee katika kaunti ya Mombasa kufuatia ilani kutoka kwa mwenye jengo linalositiri afisi za chama tawi la kaunti kwamba nyumba inauzwa. Jengo hili ambalo limo katika maeneo ya Tudor, yakadiriwa mwenyewe anataka kuliuzwa kwa jumla ya shilingi 60 milioni.
Hii inamaanisha kwamba chama cha Jubilee katika kaunti ya Mombasa lazima kigurishwe (kuhamishwa) hadi kwa makao mengine licha ya kuwa kitaifa, kimeanza kuteteleka. Ingawa hivyo, baadhi ya wafuasi wa Jubilee wa kaunti wanachukulia hatua na msukumo wa kuuza jengo hili lenye afisi za chama kuwa njama fiche ya kisiasa kutaka kuaibisha chama hiki cha serikali. Kodi ya nyumba hii imekuwa ikilipwa na mratibu wa chama jimbo la pwani, Farid Swaleh.
Kodi yake imekuwa ni shilingi 150,000 kwa mwezi. Baada ya uchaguzi mkuu kumalizika mwaka 2017, mratibu Farid aliamua kuhifadhi jengo lenye kusitiri afisi za kaunti za chama kwa niaba ya makao makuu akiona haja kuu kwamba itakuwa ni aibu kwa chama tawala kuwa bila ya afisi mjini Mombasa.
Awali mbali na afisi hii ya maeneo ya Tudor, chama cha Jubilee pia kilikuwa na nyingine katika mtaa wa Nyali lakini yasemekana ilifungwa muda mfupi baada ya uchaguzi mkuu kutokana na matatizo ya kodi. Habari za kuuzwa kwa jengo hili zimewakuta ghafla wafuasi wa Jubilee wakiteta kwamba hizi ni njama za kutaka kusambaratisha mizizi ya Jubilee katika kaunti ya Mombasa kwa kuanza kuikata kabla ya zoezi la kura za maoni kuhusiana na marekebisho ya katiba kuwafikia.
“Hutuoni uwazi wa mwenye nyumba ambaye anataka kuuza ghafla bila kumwaarifu mratibu wetu wa chama wa jimbo ili ajiandae vyema kuhamisha afisi wakati ufaao kama tulivyokubaliana awali kwenye makubaliano ya kukodishwa kwake,” asikitika mwanachama Joseph Njoroge.