For the best experience, please enable JavaScript in your browser settings.
Wengi wenu mkisikia neno uswahilini unajawa na mawazo kwamba, haya ni maeneo ya watu wa hali duni, sehemu zile zinazoitwa Majengo au mitaa ya mabanda. Ni lazima kutakuwa na maisha ya kihuni huni au ukora tena kuna udaku usabasi na uongo. Baadhi huchukua uswahilini ni kwa watu wavivu wanaopenda starehe, watu wakujipenda wataaradhi na kadhalika. Lakini kwa maana kubwa zaidi ya hiyo, uswahilini ni uafrikani, yaani kule wanakoishi waafrika tena wa hali ya kadiri au kwa lugha nzuri watu wenye kipato cha kati wastaarabu na wenye maadili, na miendo yao ya kimaisha. Licha ya hayo, maeneo mengi ya aina hiyo huwa yana msongamano wa watu.
Kwa sababu maisha katika maeneo hayo huwa nafuu kiasi. Kutokana na hali hiyo, wenye pesa wakakuita uswahilini, maana mchanganyiko huo wa makabila tofauti tofauti, dini na desturi unalazimisha wakazi hao kuzungumza kiswahili ndio lugha kuu ya mawasiliano yao, kikifatiwa kidogo na kingereza, kisha makabila yao pale wanapo kuwa wamekutana watu wa kabila moja na wapo mahala fulani pamoja, wanajikuta wanazungumza lugha yao.
Lakini hawawezi kuendelea kuzungumza lugha yao kama ataingia hata mtu mmoja asiye wa kabila lao. Hao sasa ndio waswahili wanaoishi kiswahili japo siyo waswahili halisi ni waswahili lugha. Nataka kuweka wazi kabisa, juu ya waswahili hawa na waswahili wenyewe wenye lugha ya kiswahili. Makundi haya mawili yanatofauti kubwa mno nazo ni hizi: 1. Mswahili asili ni yule aliezaliwa babaka na mamake ni waswahili, kwa maana ni wa kabila la waswahili ambalo kiasili walikitwa wangovi ( wangozi) ambao sasa kama wapo basi ni wachache sana, ila waliopo sasa ni wamiji kenda ambao ndicho kizazi cha mgovi alie pewa jina la mswahili toka kwa muarabu, kwakua alikutwa Mgovi huyo, akiishi kwenye ufukwe wa rasi ya bahari Hindi, ukanda wa pwani ya Kenya.
Kuanzia ya mji wa Mambrui hadi Kilifi, makao makuu yao yakiwa Gede. Ambako hivi sasa kuna kazi ya kuufukua mji huo wa asilia ambao sasa ni magofu ya Gede. Kazi hiyo yafanywa ili kuutafuta ukweli wa Mswahili na kupata tariikh ya Mgovi ambaye kwa jina jingine mswahili. 2. Waswahili wa aina ya pili ni waswahili wa kuzungumza lugha ya kiswahili tu kwa kujifunza shuleni na kwa waswahili. Waswahili hawa ni wa makabila mengi waliojumuika pamoja katika miji
kwa ajili yakuja kutafuta kazi au biashara, wakajikuta wanatafuta lugha ya kuelewana ndipo wanapojifunza Kiswahili ili waweze kuelewana na kuishi pamoja kwa amani. 3. Waswahili wa mapokeo, waliokirithi kiswahili, japo wao si waswahili na sio waliosomea kiswahili na kupata shahada au stashada, uzamili na uzamivu, lakini waliwasikia wazazi wao wakikizungumza kwa fasaha uliokubalika bila ya kukosoana au kurekibishana. Waswahili hawa nao wakapokea na kuendeleza kama walivyo pokea toka kwa wazazi wao, Haya ndio makundi matatu yanayo hadhi lugha ya Kiswahili na kila kundi linajaribu kukikuza kiswahili.
Tatizo linalo jitokeza ni kwamba, kuna kundi la pili la wasomi waliosomea kiswahili wazamifu katika lugha hii, ndio wanaozua mengi yasiyo ya kiswahili kutaka yawe ya Kiswahili kupitia fikra zao na waonavyo wao ni sahihi. Sasa mswahili akubali akatae lazima lipachikwe likubalike na liwe ndilo. Wao kwa imani yao wanaamini kwamba kiswahili ni lugha ya kuungaunga kutokana na lugha za kibantu ndipo kikazuka kiswahili, kwahiyo basi hakina mwenyewe. Na kisicho na mwenyewe huchezewa kikafanywa vyovyote hakina mtetezi. Mswahili mimi nasema paruwanja kuwa, Kiswahili wenyewe bado wapo, wawe wamapokezi au wajadi wa asili au wamiji kenda (Wangozi).
Hawako tayari kukaa kimya wakiangalia mnavyo kichokora, kukitia madoadoa, kukifanya duni na hakijiwezi. Kiswahili kinajiweza kipo kamili, na kinauwezo wa kutumika shuleni (Sio Mashuleni) kufundishia kuanzia chekechea hadi chuo kikuu. Kwanini hakiwezi , kwa sababu tunakidharau, imani ya mtu mweusi ni kwamba bila kujua kingereza huwezi kupata maendeleo. Nawauliza ni nchi gani ilipata maendeleo kwa kutumia lugha ya taifa jingine? Mswahili ana kijiba.
Ni muhimu tuache kubishana kulaumiana na kuonyeshana ujuzi, ubora na ubunifu wa maneno mapya wakati yazamani hatujayajaliza ,tuwe wamoja tukubaliane kwamba waswahili wapo na tuwasake kwa kina watusaidie katika istilahi, msamiati, matamshi, usuli na asili ya maneno ambayo hayatumiki ambayo yapo na yamebuniwa mengine badala ya yale yalo kuwepo. Tukiwa na umoja huo, kiswahili kitaongoza afrika. Mswahili anakijiba cha moyo, Asema Usiku ni wa mchawi mwizi na askari, Sasa Kiswahili kisiwe huko.