For the best experience, please enable JavaScript in your browser settings.
Mambo ya mitandaoni sote twaijua. Hususan kwamba kuna watu wakora na hata wenye nia za kishetani ambao wameifanya kazi yao kuwinda wenzao kwenye mitandao ya kijamii ili kutimiza njama zao mbalimbali.
Sasa hebu fikiri tu kidogo, ungefanyaje kama leo hii utakuwa kwa Facebook halafu upate kuna jamaa anatumia picha yako hasa kama yake ila tu jina anatumia tofauti? Haya ndio masaibu yalo wakumba Sharon Mathias na dadake toka nitoke Melon Lutenyo huko kwenye Facebook kwa mara ya kwanza wakati ambapo walikuwa hawajuani.
Mabinti hawa walio zaliwa katika hosipitali ya Kakamega na kutenganishwa miaka 19 iliyopita wame lizungumzia hili wao wenyewe katika mahojiano na vyombo vya habari. “Nilipatana na Melon kwa mara ya kwanza mwezi Aprili mwaka jana kwenye Facebook,” ali hadithia Sharon miezi miwili iliyopita katika mahojiano na runinga moja ya kitaifa.
“Siku moja nilipokuwa kwa Facebook nilienda kwa ule upande ambao unaweza kuwatafuta watu unao wajua halafu nikaona mtu anatumia picha yangu kama yake. Nilidhani akaunti yangu imevamiwa, kwa hivyo nikamtumia ombi la urafiki ndio ili nijue yeye ni nani,” alieleza.
Mfano wa sarakasi vile, Melon naye alipoona mtu asiye mjua ame muomba urafiki na mtu huyo anatumia picha yake, fikiria kama zile zile za Sharon ndizo zilimjia akilini. “Nilikubali mwaliko wake halafu nikaanza kumuuliza yeye ni nani maana picha anayotumia ilikuwa yangu,” alieleza upande wake Melon.
Ikawa kizungumkuti, huku kila mmoja akimshuku mwenziwe kuwa mkora anaye tumia picha ya wenyewe na kujisombezea kwamba ni yake. Kwa mujibu wa wasichana hawa, majibizano baina yao yaka ibuka huku pacha hao wasiojuana wakiulizana ‘maswali ya polisi’. Melon alisimulia jinsi mwenzake alitaka kujua yeye ni nani huku naye Melon akisisitiza kuwa Sharon ndio alifaa kujieleza mwanzo kwa sababu yeye ndiye aliyemtafuta.
“Mwishowe Sharon akakasirika na tukakata mazungumzo,” alisema Melon. Lakini kabla mazungumzo hayo kukatika siku hiyo, madada hawa pia walitupiana maneno machafu. “Mimi nilimuita pepo (mchafu) na yeye akaniita mimi jini. Sababu ya mimi kumtukana ni kwamba nilidhani ameiba picha zangu,” alidokeza Sharon.
Kulingana na Melon naye, yeye pia alirudisha tusi kwa tusi kwa sababu hiyo hiyo. Lakini ni wazi hata baada ya haya yote, kero iliyo wajaa nyoyoni mwao na hamu ya kutaka kujua zaidi kuhusu kizungumkuti hicho iliendelea kuwafanya wawasiliane tena na tena
Tamu uchungu wa dada mapacha
Melon na Sharon Kisa kilicho pigisha Wakenya wengi domo tangu kilipo jitokeza takriban miezi miwili iliyopita cha mabinti wawili wanao fanana mithili ya sarafu, hatimaye kilifika ukingoni hivi juzi.
Kwa jinsi walivyo fanana wasichana hawa, suala ibuka moja kwa moja ikawa ni uchu wa kutaka kujua kama walikuwa mapacha ambao walikuwa hawajuani. Isitoshe, ya kwamba wote wawili walikuwa wamezaliwa katika hosipitali moja, kwa wakati mmoja miaka 19 iliyopita ilizidisha joto la maswali.
Na kama ilivyo tarajiwa kwa tathmini za wengi walio pata kujua kisa cha mabinti hawa Sharon Mathias na Melon Lutenyo, majibu ya DNA yalibainisha kwamba kweli wawili hao ni mapacha na kwamba mama aliekuwa akimlea Melon ndio mzazi hasa wa pacha hao.
“Haiwezekani kupingwa kwa Rosemary Onyango kama mama mzazi wa Sharon Mathias na Melon Lutenyo, kwa kuwa chembechembe za uzazi zinafanana kwa asilimia 99.99,” ilisema ripoti ya matokeo ya uchunguzi wa DNA iliyo fanywa na shirika la Lancet Kenya.
Bila shaka kisa hiki kilikuwa ni cha aina yake, kuanzia simulizi ya jinsi madada hawa walivyojuana na kupatana, jinsi walivyo zua msisimko nchi nzima na kugonga vichwa vya habari na jinsi wasichana wenyewe walivyo jibeba kwa kuonyeshana upendo na imani kwamba walikuwa na chimbuko moja. Na ndio maana wakenya walimiminisha maoni na mawazo yao mitandaoni kuanzia siku ya Jumamosi matokeo hayo yalipo tangazwa rasmi.
Stay informed. Subscribe to our newsletter
Hususan kwa mtandao wa jumbe fupi Twitter, upesi heshitegi kama vile #Melon Lutenyo, #Rosemary Onyango, #Lancet Kenya na kadhalika zilitia fora kwa maelfu ya maoni. Kama kawaida, kwanza kabisa wakenya hawakuwa wapungufu wa dhihaka na vichekesho. “…Mtoto wa Mluhya awezi potea lazima arudi nyumbani,” alisema Fredrick Matakala kupitia Twitter. Wengine wanao fanana na watu maarufu walipata fursa hii kwa mawazo bonzo.
“Tume shamalizana na kisa cha Sharon na Melon. Lancet Kenya sasa si mufanye DNA nyengine ya mimi na ndugu yangu William Ruto,” alisema Enock Bett huku akiwa amechapisha picha yake kuonyesha jinsi anavyo fanana na naibu rais Ruto.
Waziri wa usalama Fred Matiangi naye hakusazwa kwenye sarakasi hii, jamaa mmoja akiitisha DNA ifanywe kubainisha usuli wa waziri huyo wa usalama na muigizaji filamu mmoja wa Nigeria eti kwa kuwa wanaonekana kufanana sana. Mwanahabari na mtangazaji gwiji Tony Gachoka, almaaruf TG naye alizua mtazamo dhihaka kuangazia athari za ‘mpango wa kando’ baina ya wanandoa. “Haya ndio matokeo wakati bibi yako atakuwa na mpango wa kando halafu watoto (watakao zaliwa) waje kukutana baadaye katika maisha yao,” alisema Gachoka.
Mbali na dhihaka, kuna wale walio hisi kwamba haya yote yasingetokea iwapo sio uzembe au uhalifu wa madakitari katika hosipitali kuu ya Kakamega walipo zaliwa madada hao, na hivyo basi kuelekeza vidole vya lawama. “...Ni wazi kwamba madakitari wa Kakamega wali sababisha mtafaruku kwenye kiangulio ambamo Sharon na Melvis walikuwemo. Yatakiwa madakitari hao washitakiwe kwa uzembe,” alisema Abuga Makori.
“Matokeo ya DNA yamebainisha kwamba Sharon na Melon ni mapacha wa kufanana, na kwamba walitenganishwa walipo zaliwa. Upotofu wa maadili katika hosipitali zetu una ghadhabisha mno,” Weelo Willis naye aliongeza.
Wengine walishangazwa sana hadi wakashindwa la kusema. “Nafikiria tu jinsi Rosemary na Angeline wanacho pitia hivi sasa kwa kujua kwamba Sharon na Melon ni mapacha wa Rosemary. Na kwamba Melvis ni mtoto wa Angeline. Angalia jinsi ukweli ulivyo jitokeza. Ni ngumu sana kuelewa,” alisema Mwalimu Joshua. Wengine nao hawakuchelea kufananisha hali hii na mwelekeo wa siasa zinazo zunguka vita dhidi ya ufisadi nchini. “…kongole Kenya kwa kuimaliza kesi hii. Natamani kama ufisadi ungekuwa unabebwa kwa njia hii bila ya kujivuta vuta,” alisema Ingwe Levy.
“Kongole Kenya maana kwa mara ya kwanza tumeshuhudia uchunguzi kuanzia mwanzo wake hadi tamati,” alisema jamaa mwengine kupitia akaunti yake @Im_Pachira.