Hali ya Raila, hali ya Ruto!

Loading Article...

For the best experience, please enable JavaScript in your browser settings.

Aliyekuwa kinara wa Nasa Raila Odinga akimsalimu Naibu wa Rais William Ruto katika hafla iliyopita. [Picha: Standard]

Leo ukiambia andika nsha fupi isiyozidi maneno ishirini kuhusiana na sampuli za siasa za viongozi wawili wa Kenya, waitwao Raila Odinga na William Ruto, ukiwa mtaalam na mdadisi wa siasa ya Kenya, utaandika tu; Hali ya Raila, Hali ya Ruto! Mifano yao inajitokeza tangu miaka ya 1992/97 kwa Raila akiwa anashindana kisera za kisiasa na babake n ahata wazee wengine kwenye chama cha FORD. Ushindani wake Raila ulimsukuma kukataa kukaliwa chapatti chamani cha FORD Kenya na hatimaye kuanzisha chama chake cha NDP kabla ya kuungana na KANU na baadaye kuyeyukia mbali mkaribio wa uchaguzi mkuu wa 2002.

William Ruto naye alichipuka kama kijana wa KANU kuanzia misingi ya kisiasa mnamo 1992 akiwa na kina Cyrus Jirongo na wengine kuhakikisha wametingisa jogoo kwa ushupavu mkubwa hadi kuangukia kuwa kipenzi cha professa wa siasa ya Kenya, Rais mstaafu Daniel arap Moi. Naye kama Raila, alidinda kusukumwa pembeni na mara kwa mara alikuwa akisutwa kwa kutowatii wakongwe wa kisiasa kutoka Bonde la Ufa. Mnamo uchaguzi mkuu wa 2002, Raila alikubali kwamba kidole kimoja kamwe hakiwezi kumvunja chawa hivyo, akabumburusha chama chake na kuunda kingine kuwekwa kwenye ushirikiano wa NARC akimtuza

Mwai Kibaki kama yuatosha kwa urais wa 2002. Alijua dawa ya moto (Mkikuyu) Uhuru Kenyatta ni (Mkikuyu) Mwai Kibaki na ndivyo ilivyokuwa kwenye matokeo ya uchaguzi mkuu. Hapa, kama alivyo na msimamo wake wa kidete, William Ruto hakumuondokea rafiki yake Uhuru Kenyatta na aliamua kufa naye kiume. Yaaminika aliona hali siyo hali kadiri ya matokeo ya urais yajavyo na akamrai Uhuru Kenyatta akubali matokeo na kuganga yajayo baada ya 2002.

Pentagon ya 2007 Ruto twaweza sema kwamba mtindo wake wa siasa hauna tofauti kabisa na ule wa Raila. Siasa za kifua, ukakamavu wa mbio za kampeini na lugha ya majukwaani. Wale ambao walikuwa wanachama wa ODM wa karibu naye na Raila, wanakubaliana nasi kwamba hali yake, hali yao. Kwa wengi, Ruto alikuwa nyota na mzungumzaji mkubwa mwenye msukumo fulani na anayeweza kupita nawe ukiwa umekaa vibaya njiani.

Raila alikuwa vivyo hivyo hasa baada ya kukorogana na serikali ya mpwito ya Kibaki hapo 2005. Tabia yake amekuwa akianza msururu wa siasa punde uchaguzi unapokwisha. Alipotofautiana na Kibaki, Raila alianza kampeini za mapema na ndio maana aliweza kusumbua PNU sana katika uchaguzi wa 2007. Wakati huu alikuwa amezoa upinzani wa KANu isipokuwa Uhuru Kenyatta ambaye alibadilika dakika ya mwisho kumsaidia Kibaki. Ruto alidinda akawa pamoja na Raila na vigogo wengine hadi mwisho wa matokeo.

Twaambiwa pia tofauti ya Ruto na Raila ni kuwa Raila wakati mwingine anaongozwa na ushauri wa wengine kama vile kina James Orengo lakini Ruto, akisimamia papo ni hapo. Baada ya shakala-bagala ya matokeo ya uchaguzi wa urais wa 2007, azma ya Ruto ilikuwa ni ushindi wa meno kwa ukucha lakini hata baada ya kung’angana na msimamo wake huo, alipata uwaziri tu.

Handisheki na 2022 Marafiki wa William Ruto wanasema kwamba afanyayo leo ya kutangatanga nchi nzima ni mtego wa kisiasa ambao Raila Odinga amegundua kuchelewa kisiasa. Awali, yaamiika ilikuwa ni Raila atumie salamu za ‘Handisheki’ na kamati maalum ya kuzoa maoni ya marekebisho ya katiba ya BBI kumpeperushia bendera ya kutua karibu na uchaguzi wa urais wa 2022 lakini, hapa

Ruto akajua na akaanza mapema. Ukiangalia historia ya umaarufu wa Raila Odinga tangu 1997, ni kuanza pilka pilka zake za siasa mapema na kukoroga umma na misemo yake kabla yaw engine kuanza kupenya penya mashinani. Leo hii, Ruto yadaiwa amemuwahi mapema kwa kuwa wote ni Warabu wa Pemba wanaojuana kwa vilemba. Ishara sasa yajitokeza wazi kuwa huenda uchaguzi mkuu wa urais 2022 ukawa baina ya fahali hawa wawili ijapo mzee aonekana yungali na vihunzi kadhaa vya kuruka uwanjani kabla kufikia kamba ya mwisho.

Marekebisho ya Katiba Jinsi mienendo ya Wakenya inavyojitokeza, twabashiria vituko na viegezo kwenye zoezi la marekebisho ya katiba iwapo kweli yatakuwa hivi karibuni. Twangoja kuona makadirio ya bajeti yam waka 2019/2020 kama tutaona fedha za kufanyia zoezi hili.

Imani yetu ni zoezi liendelee ili tuone mbivu na mbichi za matokeo yake. Wengi wanasema zoezi hili likifanyika kati ya 2020 na 2022, ni mtihani tosha kutudhihirishia kati ya ndume hizi mbili, Raila na Ruto nani nani atakuwa fahali dhidi yao. Hii ni kwa sababu, kunayo ishara kwamba mmoja atapinga marekebisho haya ya Katiba (bila shaka naibu wa rais Ruto) na mwingine atashinikiza mabadiliko (Raila).