Ajabu ya shule kuwa zizi la anasa na ngono

JavaScript is disabled!

Please enable JavaScript to read this content.

Mtumizi wa dawa za kulevya

Lisemwalo lipo na kama halipo basi limo njiani laja ijapo kwa mwendo wa jongoo. Maisha ya kesho inamtegemea mtoto wa leo ambaye anayo miaka mitano hadi kumi (5-10) ambaye maadili yake itategemea jinsi atakavyolelewa na mzazi ama mwalimu wake.

Kuna Imani kubwa kwamba kuchaguliwa hivi majuzi kwa waziri wa elimu nchini, Professa George Albert Omore Magoha bila shaka kutalegeza kamba janga la shule kuwa mazizi ya anasa na ngono hususan katika kaunti ya Mombasa na Kenya nzima ambapo ni dhahiri wazi kwamba idara husika ama maafisa ambao wamekuwa na jukumu la kukomesha balaa hili wamefunikwa kwa nyuso za ufisadi baina yao na wenye kusimamia shule hizi.

Ni mwaka huu tu mnamo mwezi wa Februari wakati tarakwimu mpya zilitolewa na shirika la serikali linalotia jitihada za kupambana na madawa ya kulevya nchini, National Authority for the Campaign Against Drug Abuse (NACADA) lilipotoa tarakwimu kwamba idadi ya watoto wadogo wanaotumia mdawa ya kulevya na kujiingiza kwenye anasa ya kaunti ya Mombasa pekee ni zaidi ya 250,000.

Kisa cha Greenwood Academy

Wiki chache baada ya ripoti ama tarakwimu hii kutolewa, na kuelezea jinsi wanafunzi wanavyoanza kupayukia mihadarati kuanzia shule za msingi, kupevukia kwa shule za upili na kukogea sugu wakiwa kwenye vyuo vya serikali na kibinafsi, hakuna hatua yoyote ambayo imechukuliwa na idara husika ama wizara ya elimu kushughulikia suala hili.

Hivi majuzi tulishangazwa na uvumbuzi mwingine wa kisa cha kushangaza wakati nilipoona habari za kituo kimoja cha running nchini cha KUTV kupitia kwa mtandao wake wa dijitali katika upekuzi wake wa Makala waliyodokeza kama TABIA MBAYA SHULENI. Wale walioona kama mimi runinga hii wanajiuliza iwapi kunazo idara husika zinazoweka vizingiti vya kisheria katika shule kama hizi na nyingine ama ni mtandao wa ufisadi unawaangamiza watoto wetu.

Kulingana na ripoti ya runinga hii, kuwa shule hii imezingirwa na madai ya wanafunzi wake kuwa na uhuru wa kuingia na kutoka shuleni wakijivinjari kwa kila sampuli ya tabia zote mbovu bila ya usimamizi wa shule kuchunguza na kuchukua hatua yoyote ile. Kwa kifupi unaposikiza ushuhuda wa baadhi ya wanafunzi ama wakaribu wao ni wazi hapo ni zizi la anasa na ngono ikiwa kweli yasemwayo yapo.

Mtumizi wa madawa ya kulevya

Usimamizi wa shule

Kwenye runinga hii twamuona mwalimu msimamizi wa shule ya Greenwood Academy, Madam Njuguna kama walivyomtambua kwenye Makala yao ya Tabia mbaya shuleni, anayapunja madai hayo akidai kwamba kama shule hakuna tabia mbaya hizo.

Licha ya mwalimu kudinda, masimulizi ya baadhi ya wanafunzi katika taarifa tulizozinasa kutoka kwa taarifa zao za kushinikiza madai ya anasa na ngono pamoja na malalamishi ya mashirika mawili yasiyokuwa ya kiserikali ambayo yaliandikishwa taarifa zake katika kituo cha polisi cha Nyali kupitia kwa warakha wa OB 89/26/2/19 ni dhahiri wazi kuwa ni zamu ya waziri Prof. George Magoha kuanza mikakati sawa na ile aliyoweza kuthibiti wizi wa mitihani.

Ikiwa mwanafunzi anaweza kunakiliwa kwenye taarifa yake kwamba anaweza kuingia shuleni na msokoto wa bangi ama mihadarati mingine kutoka kwa wenzake na wakatumia wapendavyo kisha waende nyumbani bila mushikili wowote.

Isitoshe inaelezwa kupitia kwa ushahidi wao kwamba shule kama hii ambayo ipo mahali ambapo hamna nafasi kamili ya bustani ya michezo isipokuwa ukuta unaozingirwa mazingira ya kimji mamboleo bila shaka hatari ya watoto kuingiliana ovyo wakati wa mapumziko (break) ipo kwa asilimia kubwa. Tayari, kulingana na wizara ya elimu ya kaunti ya Mombasa, majirani wa shule hii twaambiwa wameshawahi kulalamikia suala hili la utovu wa nidhamu.

“Ndugu yangu ananiambia rafiki yake hubeba mipira ya kufanyia mapenzi akienda shuleni hapo na kuzitumia na wanafunzi wenzake kwa kufanya ngono wakiwa chooni na akirudi nyumbani huwa akili yake inamzungumzia nchi ya Jamaica ishara kamili kwamba huwa amevuta bangi.” Asimulia mmoja wa wale waliopata fursa ya kuhojiwa na runinga kwenye safu ya Tabia Mbaya shuleni juu ya shule hii.

Mashirika lalamishi ikiwa ni pamoja na lile la Commission For Human Rights and Justice tayari wameandikia wizara husika za kaunti na kitaifa juu ya suala hili ijapo afisa mkurugenzi wa elimu wa kaunti Moses Makori alilipa kishogo na kuagiza vyombo vya habari kuanzia kumjuvya afisa wake wa kaunti ndogo ya Nyali, Mary Kanyoro.

Idara ya kaunti ya elimu ya serikali ya Mombasa halikadhalika wananunguzana kwamba kweli kumekuwa na malalamishi kadha wa kadha na utaratibu unafuatwa kuhakikisha wamechipuka na ukweli wa jinsi mambo yalivyo.

Serikali iko wapi?

Tunapozungumzia serikali, yajumuisha serikali ya kaunti za na idara zake husika ikiwa ni pamoja na inspekta wake wa elimu na masuala husika kama haya kwa shule zote, Wizara ya elimu chini ya waziri George Magoha na maafisa wake wa kaunti ya Mombasa na kaunti nyingine za Kenya kwenye shida kama hii bila kumsahau waziri Fred Matiangi kwa maafisa wake ambao wanastahili kuzama na kuzukia visa vya aina hii kwa kina.

Ripoti za Nacada zimeonyesha wazi kuwa wahusika wakuu wa mihadarati huvizia shule kama hizi wakijifanya wafanya biashara wa reja reja maeneoni mwa shule hizi kama vile wazuungushaji maji, vyakula na kadhalika ilhali wanashirikiana na baadhi ya wanafunzi.

Mkurugenzi mmoja wa bado ya NACADA Farida Rashid amenakiliwa na vyombo vya habari mwezi wa Februari akisema kuwa anashangazwa na hatua ya serikali ama idara husika ambazo zinaruhusu kutoa leseni ama vibali kwa biashara za anasa karibu na shule ama wizara ya elimu kuruhusu shule kuwepo mahali ambapo mazingira yake hayafai kwa maisha ya mwanafunzi ama mtoto.

Ripoti zaidi pia zaonyesha kwamba wanafunzi wengi wanaosomea katika shule za kibinafsi ndio wanaokumbwa zaidi na balaa hili la utumiaji wa mihadarati na tabia mbovu za kijamii. Kwa mfano, siyo tu shule ya Greenwood ambako kumepatikkana na visa vya aina hii bali ni miongoni mwa shule kadha wa kadha zinazosomwa na watoto matajiri.

Kisa cha mwaka jana

Mnamo mwaka uliopita, mwanafunzi mmoja katika shule ya kibinafsi alijitia kitanzi lakini kabla ya kufanya hivyo, aliandika barua ambayo baadaye, mama yake na watu walioshuhudia mauti yake walipigwa na butwaa.

Kabla ya kumaliza mtihani wake wa kidato cha nne, kijana mwendazake alikamatwa akiwa na msokoto wa bangi. Usimamizi wa shule ambayo alisomea ulimwita mzazi wake wa kike kwenda shuleni kuzungumzia masuala ya nidhamu ya mtoto wake lakini kwa makubaliano kwamba kijana arubu makosa yake kwa maandiko na kuomba msamaha usimamizi wa shule.

Kwenye barua yake alikubali kufanya makosa lakini akatubu kwamba amekuwa akileta madawa shuleni baada ya kutumwa na wenzake. “Mwenzangu ameniagiza kutoka juma lilipotita kwamba nimletee msokoto wa bangi kutoka nyumbani kwa sababu anahitaji kuivuta baada ya mtihani. Kazi yangu nikuileta alafu anilipe baadaye,” aliandika kwenye barua yake ambayo ilinakiliwa na gazeti moja humu nchini.

Jambo la kuhuzunisha ni kuwa baada ya kutubu kwa kuandika warakha huo, mwanafunzi huyu alijitia kitanzi papo hapo maeneo ya shule. Kisa hiki kilishuhudiwa mwaka jana.

Katika kisa kingine cha kuvunja moyo, mwanafunzi mwingine wa darasa la saba katika shule ya msingi ya serikali (umma) pia alishikwa akiwa na msokoto wa bangi huku walimu wakisikika wakisema hilo limekuwa ni jambo la kawaida siku hizi.

Marufuku

Daima dawa, msimamizi wa chama cha walimu cha KNUT (Kenya National Union of Teachers) tawi la Mombasa, David Mulei amekuwa akishinikiza kusitishwa kwa wafanya biashara wa reja reja karibu na maeneo ya shule na aidha kupiga marufuku leseni za biashara za anasa karibu yake na kuhakikisha pia shule za kibinafsi zinafuata maadili ya kielimu yafaayo lakini siyo kwa sababu ya biashara.

Kamishina wa kaunti ya Mombasa Evans Achoki naye amekuwa akilizungumzia suala hili lakini hatujui vikwazo viko wapi ikiwa wakati mwingine ushahidi unaweza kujitokeza lakini hakuna hatua yoyote inachukuliwa.

Msimamizi wa utawala katika jimbo la pwani John Elungata anasema akinukuliwa kuhusiana na suala hili kwamba majumba ya starehe (mabaa) hayafai kuwa karibu na maeneo ya shule. Anasema shule inatakiwa kuwa hatua zaidi ya mita 300 kutoka kwa masuala ya mji mamboleo. Hatahivyo, wasimamizi hawa wameshindwa kutoa mwongozo wa je ni vipi ikiwa mtu anakodi jengo la shule ya kibinafsi karibu na majengo mengine ambayo yamekuwa yakiendesha biashara zao karibu na shule hizi.

“Tumeona shida kama hii katika eneo ambalo shule ya kibinafsi yenye utata mwingi wa maadili ya Greenwood hapa Links Road ikiteta na majirani wao ambao ni mkahawa wa Robertos kwa wanafunzi wao kukosa nidhamu wakiwa kwenye madarasa yao,” asimulia mfanya biashara mmoja anayeendesha kazi yake karibu na msikiti unaoangalia kwa upande wa pili wa barabara hii.

Katika taifa letu la Kenya maadili ya kiutu katika jamii yamezikwa katika kaburi la sahau na hatimaye Wakenya wote kujitosa katika jinamizi la uporaji mali, kampuni za ufisadi na ubinafsi na kupanda siasa za chuki zisizokuwa na mrengo wa kushoto wala kulia ila zile za bora mimi na familia yangu. Wizi umekuwa ukianzia na mwanafunzi wa darasa la nane hadi chuo kikuu kuiba siri za mitihani kwa mfumo wao maarufu wa Bomba. Kazi ipo kwa Waziri George Magoha.