Siku chache baada ya baraza kuu la chama cha ODM kumtimua mbunge wa Malindi Aisha Jumwa Karisa, mbunge huyo ameukosoa utaratibu uliotumiwa na kamati kuu ya chama hicho kumtimua chamani.
Akiongea huko Malindi baada ya kulakiwa na wafuasi wake waliokuwa wamebeba mabango yenye maandishi ya “tulimchagua kiongozi wala sio chama,” amesema hakubaliani na uamuzi huo, kwani sheria na taratibu hazikufuatwa hivyo yeye bado ni mbunge wa Malindi kwa mujibu wa Katiba.
Jumwa amesema hatingishiki na hatatishwa na uamuzi huo, akisisitiza kwamba hakuna uchaguzi mdogo utakaofanyika ndani ya eneo bunge la Malindi na kwamba uamuzi huo hauwezi kum`maliza kisiasa .
Ameongeza kwamba vita vya kisiasa anavyopigwa ni ishara kwamba amekuwa tishio kwa wengi kisiasa, na kwamba hatakubali siasa za uonevu za jamii ya Mijikenda, na kuongeza kwamba hataomba msamaha.
“ODM inasema ilimaliza taratibu zake, mimi Aisha Jumwa naanzia hapo, niko nao papa kwa hapa, wasifikiri mimi nimechaguliwa kutishwa tishwa my friend umegonga mwamba, Aisha siye yule wa kuonewa na hivi mnavyo niona sihitaji kumuomba msamaha mtu yeyote, na hakuna kura zitaregelewa hapa Malindi,” akasema Jumwa.
Jumwa amewataka wanawake kujitokeza katika harakati za kutafuta nyadhifa mbali mbali za uongozi pasi na hofu yoyote, akiwataka wanawake kusimama imara wasidhallishwe.
Amesema maonevu yanayofanyiwa wanawake viongozi ndiyo sababu ya kutopita kwa sheria ya kuleta usawa wa jinsia bungeni kwa mara ya nne.
Hata hivyo wafuasi wake, wameutaja uamuzi huo kama maonevu na kuapa kumuunga mkono.
Mwakilishi wa wadi ya Kakuyuni Nickson Mramba na mwenzake wa Jilore, Daniel Chiriba, wamesema uamuzi huo utapelekea kuheshimiwa kwa sheria za vyama vya kisiasa na kujenga misingi ya vyama.
Chiriba amekitaka chama kurudisha wadhifa wa kamishna kwa mbunge yeyote wa chama cha ODM kutoka Pwani ambaye anatii sheria za chama, na kuongeza kwamba watamuunga mkono yeyote atakayechaguliwa kupeperusha bendera ya chama hicho.
“Hili ni thibithisho kuwa chama kina msimamo na endapo mama atarudi kwenye debe tutahakikisha kuwa tunachangua mtu ambaye ataheshimu cha cha ODM na tunamuomba Raila ile nafasi ambayo alikuwa anashikilia bungeni ipewe mtu wa hapa pwani,”akasema Chiriba
Naye mwenzake wa Kakuyuni, Nickson Mramba amesema kufurushwa kwa Aisha hakutasambaratisha chama cha ODM kama inavyodhaniwa, akisema umaarufu wake binafsi ulitokana na chama cha ODM.
Mramba amemtaka Jumwa kubeba msalaba wake mwenyewe kwa kukosa kutii sheria za chama.
Stay informed. Subscribe to our newsletter
“Watu wa Malindi wamefurahi sana kwa uamuzi wa chama, hivyo tunasubiri spika wa bunge la kitaifa kutangaza kiti hicho kuwa wazi ili tuende kwa uchaguzi ndio tuone kama kweli Aisha atachukua kiti hicho. Kwa sasa hatuna mbunge na itakuwa fundisho kwa wengine na kama ana watu kweli tunamsubiri kwa debe Malindi bado ni ODM na Raila hapa,” akasema Mramba.
Aisha Jumwa aliondolewa kwenye chama hicho kwa kukiuka maadili na sera za chama kwa kujihusisha na naibu wa rais William Ruto ambaye ni wa chama cha Jubilee na kusema hadharani kuwa atamuunga mkono wakati wa uchaguzi wa mwaka 2022.
Mbunge wa Msambweni Suleimani Dori aliliandikia barua ya kuomba msamaha kwa baraza kuu la ODM.
Jukumu sasa ni la Katibu mkuu wa chama cha ODM Edwin Sifuna kumwandikia barua msajili wa vyama vya kisiasa nchini kumfahamisha uamuzi wa kumtimua Jumwa, kabla ya msajili wa vyama kubuni jopo la kumsikiza Jumwa na badaye kumfahamisha spika wa bunge la Kitaifa uamuzi wake, ambapo hatimaye ataifahamishi tume ya uchaguzi nchini IEBC endapo kutahijika kuwa na uchaguzi mdodo Malindi .
Jumwa angali bado yuko na nafasi ya kuendaa mahakamani kupinga kutimuliwa kwake na ODM.