Joho amnusuru Dori, Aisha apewa talaka

Wabunge wa Pwani Suleiman Dori (Msambweni), Aisha Jumwa (Malindi) na Mohammed Ali (Nyali) walipokuwa wakihutubia wanahabari. [Picha: Standard]

Baada ya kugundua kwamba majuto ni mjukuu, mbunge wa Msambweni alikuwa amefika mwisho wa ngamani za kisiasa pale alipoambiwa kwamba pamoja na mwenzake mbunge wa Malindi, wataonyeshwa cha mtema kuni wakati wa kikao cha uamuzi wa wajumbe wa chama cha ODM luiofanywa  mnamo Machi ya tarehe 1.

Kama kuna mtu ambaye aliathirika na subra ya hatima yake bila shaka siyo mwingine ila ni Suleiman Dori, mbunge wa Msambweni ambaye ijapo wengi hawaelewi ni kwa sababu gani aliponea chupu chupu, ukweli ni kwamba hii ilimbidi naibu mwenyekiti wa kitaifa wa ODM, gavana wa Mombasa Hassan Joho kuchukua hatua ya haraka baada ya kugundua kwamba Dori ameshtuka na nyumba yake tayari ilikuwa imeanza kuyumba yumba kama habari za kina zinavyotubashiria.

Hii inamaana kwamba ishara iliyoonekana na marafiki wa karibu na Dori na rafiki yao gavana Joho kwa kuwa hawa wote wamekuwa Warabu wa Pemba tangu Suleimani Dori na Mbunge mwingine rafiki wao Khatib Mwashetani kushawishiwa na gavana kugombea viti vya ubunge wa Msambweni na Lunga Lunga mwaka 2013.

Gavana Joho, Khatib Mwashetani na Suleiman Dori wote ni rika moja na marafiki wa dhati ambao wameshirikiana moja kwa moja siyo tu kimasuala ya siasa bali hadi kifamilia hivyo habari za kuaminika zatuongoza kwamba Gavana Joho muda huu wote hakuwa anapata usingizi wala amani kutokana na shinikizo la familia wa pande zote mbili ambazo zilimhimiza kumuokoa Dori ambaye tayari alikuwa ameanza kudhoofika kimawazo, fikra na hata mwili kuhusiana na jambo hili.

Yadaiwa wacha familia yake yote, yule ambaye alitishia kumuacha ni mke na kumekuwa na mazungumzo ya upatanishi kwa muda mrefu hivyo akawa anawazua mwisho wa hukumu ya chama na huku kwake hajui ashikilie nguzo gani ya nyumba endapo mke ataamua alivyotaka kuamua.

Kwa kuwa katika maadili ya dini kunao ushauri na ushawishi mkubwa kutoka kwa jamii wa pande zote mbili na marafiki, hatua ya chama cha ODM ya kumsamehe Suleiman Dori ama kwa hakika kumemfanyia wema siyo eti kwa kukwepa kampeini za uchaguzi mdogo wa Msambweni lakini kwa sababu kumempa uhai tena wa kifamilia.

Ijapo uamuzi wa chama haujapokelewa vyema na baadhi ya wanachama na wafuasi ambao wameona kuwepo kwa maonevu dhidi ya waasi wote wawili kwamba walistahili adhabu sawa, marafiki wa karibu na Dori wanazungumza kwamba hii ni afueni kubwa kwao kwani wanahofia kwamba umauzi wa ODM ungembana kama mbunge wa Malindi Aisha Jumwa, yamkini hawajui angedhurika vipi kimaisha.

“Alikuwa anashinda na kukaa peke yake kwa masaa mengi akionyesha ishara ya kuwa anakereka kimawazo nasi tukajua ni kwa sababu ya maamuzi ambayo chama chake kilikuwa kinajiandaa. Ni afueni sasa twamuona ameanza kutabasamu na taharuki imemtoka kuonyesha wazi kuwa alikuwa anajutia matendo yake”, azungumza mkaribu wake mmoja ambaye wakati mwingine walikuwa wakinywa chai naye mkahawani maarufu ulioko Nyali, Mombasa.

Siasa mchezo mchafu

Siasa ni mchezo mchafu na anayefaidi katika mchezo huu ni sungura mjanja wa falsafa hiyo.John Locke yule msomi na mwanafalsafa mahiri wa Uingereza alisema kuwa mwisho wa jambo huhalalisha mwanzo wake (the ends justify the means).

Yamkini Aisha Jumwa yule Mbunge m’bishani wa Malindi alotimiliwa majuzi na chama kilichompeleka bunge cha Orange Democratic Movement al maaruf ODM hakufahamu haya na undani wa siasa za Kikenya.

Laiti Aishah angefata falsafa ya Locke ya kulenga juu badala ya kufata sheria na adabu nyingi katika siasa haya hayangempata kamwe.

Ukaidi wake wa kutobadili msimamo kwa kuogopa kuambiwa hana msimamo kumemponza pakubwa.Na hapa ndipo muasi mwenza Suleman Dori M’bunge wa Msambweni alivyompiku na kufuzu ilimu na falsafa nyeti ya Locke,

Yamkini Dori alisoma siasa ama alishauriwa vyema na wazee wa Msambweni na ndipo akaema hewala isiyo ya utumwa na kurudi chini na kuomba msamaha kwa chama cha chungwa ODM.

Maonevu ya jinsia

Kufukuzwa kwa Aishah kunaweza kutazamwa kwa njia mbali mbali.Kuna wale wanaona huyu mama kaonewa kwa sababu tu ni mwanamke.

Madai haya ya kuonewa kwa mwanamke ni jambo ambalo linadhihiri haswa miongoni mwa wanawake wanaoona mwenzao kaonewa na wanaume.

Machungu haya ya wanawake yamezidi kasi kwani tukio la kufurushwa kwa Aishah limekuja siku chache baada ya bunge la waume wengi kushindwa kutekeleza usawa wa wanawake katika nyadhifa kupitia kwa thuluthi mbili kwa tatu.

Aisha anaamini kuwa anaonewa na kuwa hana makosa.Swali ni je, ni kweli hana makosa na ni madume tu yaso haya wala kuona vibaya ndio wanamuonea bure bilashi?

Kwa wanaofahamu chanzo cha songombwingo hii watakumbuka kwamba Aishah alkuwa mstari wa mbele katika kumpigia debe Ruto awe Rais katika kura za 2022.

Aghalabu Aishah alijitowa kimasomaso kumuuza Ruto katika ngome sugu ya ODM yaani pwani.Alijitwika wajibu wa kuleta mapinduzi ya kichama katika pwani.

Aishah hakuwa peke yake katika kauli mbiyu ya ‘Ruto tosha’ kwani kulikuwa na kina Dori,Owen Baya,Mwinyi na wengineo.

Mgala muue na haki mpe

‘Ulimi ni kiungo kidogo sana mwilini lakini huweza kujenga na pia kubomowa’asema Bi Kutsetsera kifalsafa akiongeza kuwa kama Aishah angezungumza kwa heshima na kujutia kosa lake angesamehewa.

Je, Aishah alikuwa mjuaji ? kwanini alijipandisha juu na kuwapuza wakuu wake katika swala kubwa la siasa za kitaifa? .

Mgala muuwe na haki yake mpe Aisha mashallahu ni shujaa na wa kipawa chakuweza kuhutubu.Ana mnato wa pekee na asiyeogopa.

Tukumbuke Aisha alikuwa mwanasiasa wa pekee wa kike aliyesukumwa korokoroni kule Nairobi kiwa tuhuma za uchochezi.

Wengine waliotiwa korokoroni kule Pangani, Nairobi ni Johnstone Muthama, Junet Mohamed na Moses Kuria.Ushujaa huu ulimfanya kinara wake Raila kumpenda na kufanya apate umaarufu.

Hata wakati Aishah alipokuwa akimkrjeli Raila lakini yeye Raila alikuwa akicheka na kumfananisha na yule shujaa wa jadi wa kike wa kigiriama Mekatilili wa Menza.

Je, Aisha akiwa mgiriama ni mzimu wa Mekatilili wa Menza?.Pengine.Mwanadada huyu hacheki na mtu ni kama simba akiwa mnarani akitowa cheche za siasa.

Akiwa na sauti nzito isiyo hitaji kipaaza sauti inayotetemesha ardhi na matumbo ya wengi Aisha ana sifa adimu ya uongozi katika siasa inayopelekwa na ujasiri kwani ni mchezo mchafu.

Tofauti na mwenzake mbunge wa Likoni Mishi Mboko mwenye kisauti kidogo cha kike cha kuparara Aishah hunguruma kama simba na kutowa mawazo mazito mazito ya mnato mwaanana.

Mwenyezi Mungu amemjalia Aishah mashallah kuwa na mwili mkubwa na si unene ule wa tepwetepwe wa kihindi bali uzito anaoweza kuubeba.Bibi huyu ni mrefu mwenye nguvu sifa inayowatisha wapinzani wa kiume ambao hutetemeka kwa kumuona tu!

Ni mwanamke ngangari mke bomba asiyezubaa.Ni mwanadada wa mjini anayejuwa mengi na asiye na zohali kufanya kile anachoamini kuwa sawa liwake lisiwake!

Kwa tathmini hii hatuwezi kumlaumu Aishah kwa kumuita mjuaji kwani ndivyo alivyo!.Hafichi kitu si mnafiki husema anachoamini.

Hata hivyo sifa hii ndiyo ilomponza.Katika siasa kuna wakati ambapo mtu huwa kinyonga ili yake yawe kama tulivyotangulia kutathmini falsafa ya John Locke.Kuna mfano mwengine.

Historia yatukumbusha nini?

Winston Churchill yule kiongozi wa Uingereza wakati wa vita vikuu vya pili vya dunia anatowa mfano wa kujigeuza katia siasa na hata kujidai muoga mradi ufanikiwe mwishoni!

Baada ya kushinda nchi kadhaa kama Ufaransa walosalimu amri  Dikteta wa Ujerumani Adolf Hitler alibaki na upinzani mmoja tu-Uingereza!

Hitler alivamia Uingereza kupitia English Channell na mwisho mamia ya ndege zake kuambaa katika jiji la London kama wingu jeusi tayari kulipua jiji hili la jadi.

Huku ndege hizo zikizunguka London Hitler alimtaka Churchill kusalimu amri na kutangaza katika vyombo vya habari.

Badala ya kukataa sharti la Hitler  huyu bwana mjanja sungura Churchill alikubali ’kusarenda’ lakini akawaweka majeshi yake hali ya hatari bandarini tayari kulipua ndege za Mjerumani zinapoondoka mipaka ya Uingereza.

Naam! Baada ya kusalimu amri Hitler aliona kashinda na kuamuru marubani wake warudi nyumbani.Loo! mara zilipokuwa zinatoka makombora yalidenguwa takriban ndege zote za Hiter.Huo ndio ulkuwa mwisho wa Hitler ambaye alijiuwa kwa fedheha ya kushindwa.

Mekatilili wa Menza

Aisha Jumwa angetumia mbinu za Churchill na John Locke kama muasi mwenza Dori aloomba chama cha ODM msamaha kwa makosa yake na akasamehewa.

Angeomba msamaha na angesamehewa kama Dori badala ya kuwa na msimamo mkali ilihali alikosea chama.

Aishah angepima maji na unga na nyakati.Kwa sasa yule aliyekuwa anampigia debe yaani Ruto yu tabani na anajitea mwenyewe na hata hana shughuli naye licha ya kumtetea.

Ruto ana vita vyake kwani amesongwa huku na kule.Amekuwa akiwatetea watu wake haswa mawaziri wanaotuhumiwa kwa ufisadi.

Ukweli ni kuwa Aishah alimuunga mkono Ruto baada ya makamu wa rais huyu kumuahidi maendeleo mengi na hata kuzinduwa miradi iliyokwama sehemu za pwani.

 

Kwa sasa Ruto pwani aiona paa kwani zile safari zake za kila wikiendi kuja kuogelea baharini zimeisha na kuwacha kina Aishah mdomo wazi chanda mdomoni mikono kiunoni!

Tamaa ya fisi ya maendeleo imeyeyuka kama theluji ya Kilmanjaro wakati wa kiangaza.Ruto sasa hana usemi wa kuleta maendeleo na mkono mtupu haurambwi unkuwa mkono birika hapendwi mtu apendwa pochi!

Dori aliyaona hayo na haraka akatanabahi kuwa mkono usouweza huna budi kuubusu.Aishah naye alikataa kukubali hayo na pengine aliona ‘iii!’ ama fedheha kuomba msamaha!

Mti mkuu ukianguka ndege huhangaika.Kukatwa makali Ruto kumefanya walomsujudia kama bwana pesa kuwa mashakani.