Barua kwa mke mwenzangu mpendwa.

Loading Article...

For the best experience, please enable JavaScript in your browser settings.

Mke mwenzangu mpendwa,

Pokea salamu furifuri kama mchanga wa bahari kutoka hapa kwangu. Natumai u mzima. Mie ni mzima kama kigongo.

Najua hautaraji kupokea barua kutoka kwangu. Uhasama kati yangu na wewe umedumu kwa mwongo mmoja sasa. Nakumbuka cheche za matusi ulizonirushia baada ya kujua kuwa mie mwandani wako wa kufa kuzikana nimegeuka mke mwenzio. Wengi walikushtumu na kukukejeli kwa kuniweka karibu nawe. Naomba radhi kwa kuwa rafiki wa jana na adui mkubwa leo.

Hata hivyo, sikukusudia wala kutaraji kuwa nitakuja kuwa mke mwenzio. Kama ujuavyo nilikuwa sijapata mume nilipofikisha miaka thelathini na tano. Nilichekwa kuwa nimekuwa bikizee na sitampata mume katu. Wachanganuzi walibaini kuwa ni kwa sababu nina madaha kama tausi. Wengine walisema kuwa sura yangu imechuchuka. Licha ya kuwasalimu na hata kutabasamu nilipokutana na wanaume njiani, hakuna hata mmoja aliyetabasamu au kuniomba hata nambari ya simu.

Kama marafiki wa jadi, tulikutana kwako mara kwa mara. Nilikushtakia hali yangu na namna ninavyosoneneka kwa kukosa mchumba. Kusema kuwa mume wako(wetu) alinikonyezea jicho au kutaka uhusiano nami ni kuwa mwongo. Ningeeleza waziwazi namna uhusiano wangu na mume wetu ulivyoanza lakini nitakuwa nakutonesha kidonda ambacho sina uhakika kama kimepoa

Jambo la muhimu kutaja ni namna ulivyokeketwa maini baada ya kujua kuwa mume wetu alinijengea nyumba ya ghorofa. Naarifiwa kuwa ulizua vurumai na kuapa kuwa unapaswa kujengewa nyumba kama hiyo ima fa ima. Ni muhimu kujua kuwa nilikuwa nimeweka akiba ya kujenga nyumba hiyo. Mume wetu alikataa kata kata nijijengee nyumba ilihali yeye ndiye mume. Nilipomweleza kuwa nataka nyumba ya ghorofa na yenye chumba cha mviringo cha kulala kule juu, alisema kuwa ndoto yangu na matakwa yangu yote yatatimizwa kulingana na uwezo wake. Alipopungukiwa kifedha wakati wa ujenzi, nilimuauni ili aweze kulipia wana wetu wote karo.

Nimejitia ububu kwa miaka kumi ili tusije tukachaniana nguo kadamnasi ya watu. Mashemeji waliponieleza yote uliyosema kunihusu sikupigwa mshipa au kuwaeleza mambo yako mengi ambayo nayajua lakini sijaona haja ya kuyasema. Najua nilifikwa majukumu ya kwenda kila mahali na mume wetu. Jambo hili halikukufurahisha.Tulipokutana karamuni hukupenda namna nilivyojitambulisha kwa jina la mume wetu huku nikiwa na ujasiri bila woga au aibu yoyote. Kwa nini ulitumia jina la babako na kukata kuzungumza na jamaa wote waliozungumza nami?

Ukewenza sio matakwa au kosa langu na lako, ni jinsi jamii inataraji tuwe. Ugomvi na uhasama kati yangu na wewe ni mwiba wa kujidunga sisi wenyewe. Mbona urafiki kati yetu kama jadi hauwezekani? Masaibu unayoyapitia ni yale yale ninayoyapitia. Muwe wetu anaponizaba kofi, wewe pia unazabwa. Anaporejea kwangu wakati ambapo jogoo wa kwanza anawika, naskika kwako ni vivyo hivyo. Ulinionea gere kuwa mume yuaishi kwangu, pia mimi nilikuonea gere kuwa mume yuaishi kwako. Sote tunajua kuwa alikuwa na hawara wake wa miaka mingi. Sote tumesalitiwa katika ndoa hii. Singependa kukuchosha na mengi mke mwenzangu. Najua ni zamu yako ya mume wetu kuja kwako (Iwapo atakuja.) Kwa sababu hiyo una mengi ya kufanya.

Madhumuni ya kukuandikia ni kukujuza kuwa nimeshidwa na maisha haya ya uke wenza. Ningependa tuendelee kuishi ili labda siku moja tuje tuwe marafiki. Lakini tutawezaje ilihali machozi yako ya jana ni machozi yangu ya leo? Chuki na masimango ya kila siku kutoka kwako na kwa familia ya mume wetu ni mambo yanayonivunja moyo kila siku. Aidha mume wetu kuwa na hawara wengi, kuja nyumbani kama tukizi la samaki kuishi nchi kavu na kutuchapa ni jambo ambalo siwezi kuishi nalo. Kwa sababu hii, nimefunganya virago vyangu na kurudi kwetu na wanangu watatu. Najua hutaraji kuwa nitakunja jamvi baada ya muda huu wote au kukubali kuwa nimeshindwa. Licha ya kuwa na miaka arubaini na tano na kupata jiko tena ni kama kutafuta sindano nyasini, sitakataa tama. Namwachia Mola yote. Nakutakia kila la kheri na naomba Maulana amkengeushe mume wako (wetu.)
Ni hayo tu.

Mke mwenzio,

Aggie Sikuku.