Uchawi na athari zake Pwani na barani Afrika

Wazee wa Kaya daima wamekuwa wakihusishwa na tambiko za uchawi hivyo kuleta athari kubwa kwa baadhi yao ambapo vijana wamewaua kwa madai ya uchawi .

Katika maelezo ya historia ya watu wa Mijikenda, tumesikia kwamba kulikuwa na watu waliokuwa na vipawa mbali mbali na pia majikumu tofauti tofauti. Wazee wa Kaya, walikuwa makuhami ambao ndio waliokuwa na majukumu ya kuliongoza taifa kwa njia nyingi.

Wazee hawa ndio waliokuwa na majukumu ya kufanya maombi kwa niaba ya jamii nzima, ila tu walipotoka kufanya maombi hayo, walikuja kuwaeleza watu yale maagizo waliyopewa kutokana na maombi yao. Mengi ya waliyoamriwa kufanya kama jamii, yalifuatwa bila ya maswali kutoka kwa jamii, kwani, hawa ni watu waliokuwa na uwezo wa kuzungumza na ‘Mulungu’ na mara walipopewa maagizo ya kufuata, basi kila mtu alikuwa hana budi kuyafuata maagizo hayo.

Kama tunavyofahamu, kulikuwa na hata siku maalumu ambapo watu hawakufanya kazi’ jumwa’ ambayo ni siku iliyoheshimiwa sana na wana jamii na siku hiyo ilikuwa siku takatifu. Wazee walijitakasa siku saba kabla ya kwenda kwenye maombi, na siku nyengine saba baada ya maombi.

Siku hizi kuna wazee wanaojitwika mzigo wa uzee wa Kaya hata bila kujua umuhimu wa cheo hicho. Hii ni kwa sababu hawakufundishwa namna ya kuomba, na hata jinsi ya kujitakasa kabla ya kwenda kufanya hayo maombi. Ukweli ni kwamba wazee wa Kaya wa siku hizi ni watu wakujichagua wao wenyewe na hawana habari juu ya mambo anayotakiwa kufanya mtu anapoingia Kaya.

Nimeanza kwa kusimulia habari hizi za Kaya kwa sababu watu wengine hawafahamu kwamba mle Kaya, dawa za uganga na uchawi hazikuruhusiwa. Zaidi pia ni kwamba ni watu wa mbari fulani tu, waliopewa majukumu ya kujua mambo ya madawa, kwa usalama wa jamii. Ni watu hawa pekee kutoka kwa mbari fulani waliopata mafunzo ya madawa na hata uganga na uchawi.

Tofauti ni kwamba watu hawa hawakuwa na ruhusa ya kutumia ujuzi wao huo, bila idhini ya wazee. Ilifahamika wazi kwamba kungekuwa na madhara makubwa ikiwa elimu hii ingeingia kwenye mikono ya watu wasio na maadili ambao hawakula kiapo cha kutofanya mabaya.

Nchi ya Afrika Kusini imekuwa na itikadi ya makundi maalum ya wachawi hususan jamii ya Wazulu kama kina mama hawa wachawi katika miaka ya 1800s

Ustawi wa jamii ya Wamijikenda ulisambaratika wakati ambapo vijana waliasi wazee, wakitaka nao kuwa matajiri kama wale wazee. Wakahama Kaya na kuanzisha makao yao shamba. Vijana walipoanza kupata utajiri, wakahitaji kujihami kuzingira maboma yao, hapo wakaanza kuwashawishi vijana wenzao katika ile mbari iliyokuwa ikimiliki elimu ya madawa na wakanunua elimu hii.

Huo ukawa mwanzo wa kila mtu awaye yeyote kununua elimu hii ya madawa, na sasa tunaona matokeo yake. Ikawa kila mtu anaweza kuuziwa fimbo ya wazee na matumizi mabaya ya elimu hii yakadhihirika, na matokeo yake ikwa ni balaa kwa jamii nzima. Hata japo watu walikumbatia dini za kikristo na kiislamu, hawakuacha kutumikia itikadi hii ya uganga na uchawi, hivi kwamba uchawi unaweza kuhesabiwa kuwa mojawapo ya dini zinazosambaa.

Kuna uchawi wa kumfanyia mtu hiana na ubatili, kuna uchawi wa kutafuta mali na mengineyo. Yote hayo yana madhara mabaya kwa jamii, kwani hata wale wanaoenda makanisani na miskitini, mwishowe huishia kwa waganga na wachawi.

Tumesikia habari za wazee kuuawa kwa kisingizio kwamba ni wachawi, lakini imebainika wazi kwamba vijana wanpotaka kuuza mali ya baba yao nao wakatae, basi watatafuta sababu, na watawakelea mashataka ya uchawi na kwa ajili hiyo basi wazee wengi wamepoteza maisha yao.

Miaka ya sitini na sabini walitokea waganga waliokuwa na nguvu za kipigana na nguvu hizi za uchawi. Wazee watamkumbuka Kabwere ambaye mwanzo wa huduma yake alisifika kwa kuwatambua wachawi na kuzima nguvu zao. Baadaye alikuja Kajiwe ambaye naye alikuwa na sifa hizo. Lakini ukweli ni kwamba  hawa ni watu ambao huja kwa msimu alafu wakapotea, au hata na wenyewe wakaingia kuwa wachawi wakiona faida zake. 

Kajiwe alijulikana sana miaka ya sabini na kuendelea hadi kifo chake. Kajiwe ambaye jina lake hasa ni Tsuma Washe, alizaliwa huko Buni Rabai, alikuwa mgema na baadaye akawa mvuvi. Ni wakati huo alipokuwa mvuvi ndipo yasemekana alichukuliwa na pepo wakamzamisha baharini miezi mitatu kumfundisha elimu hii ya kupigana na wachawi.

Tsuma Washe alikuwa kijana wa kawaida tu kama vijana wengine wa rika lake, kwa hivyo hakuna aliyefikiria kwamba siku moja angekuwa mganga mashuhuri wa kupigana na wachawi. Alipotoka baharini baada ya mda huo wa miezi mitatu, ndipo akajipatia jina Kajiwe kuendeleza kazi ambayo amepewa.

Inasemekana alipokuwa kwenye kitovu cha bahari, Kajiwe alikula tope za baharini kwa mda huo wa miezi mitatu.  Watu wengi wanaamini kwamba Kajiwe alifanya kazi nzuri sana wakati huo, kwani alisaidia kuwaondoa wachawi, na watoto wengi walifanikiwa kwenda shule na kukamilisha masomo yao, bila matatizo. Wachawi waliposhikwa na Kajiwe, walikiri uovu wao na baada ya kuoshwa na mkojo wa Kajiwe, waliapa kutoshiriki uchawi tena.

Tofauti yake na Tsokonde ni kwamba Kajiwe hakuwalisha viapo wachawi bali aliwaosha kwa mkojo na mkojo huo ulisemekana kuwa na nguvu ya kuvunja nguvu hizo za wachawi. Jina la Kajiwe lilijulikana mbali na hata huko Ukambani walijitokeza kina Kajiwe wengine, jambo ambalo lilimsababisha Kajiwe mwenyewe kukita kambi huko ukambani.

Inajulikana wazi kwamba huko Ukambani wako wataalam wa madawa ya uchawi ’kamute’ na kwingineko ni Tharaka na Mbeere. Ukweli ni kwamba katika kila sehemu ya Kenya utapata habari za uchawi, isipokuwa wachawi na waganga wa sehemu mbali mbali hutumia mbinu tofauti kwa uchawi wao. Wengine huruka usiku wakifanya mazingaombwe yao, na wengine wanafuga nyoka wakiwatumia kuwaumiza majirani zao.

Hakuna dalili za kudhihirisha nani mchawi nani siye mchawi

Athari kubwa ya uchawi ni kurudisha nyuma maendeleo, kwani mtu akionekana kuinua kichwa katika jamii, basi huandamwa na visa na mikasa.

Tatizo hili si la pwani pekee na wala si la Kenya pekee kwani imebainika kwamba sifa za wachawi barani ziko kila mahali. Hii ndiyo sababu sasa kuna wahubiri kila mahali wanaosifika kwa kupigana na mapepo na wachawi. Utaona hata katika runinga yako, watu wakitolewa mapepo na mambo ya uchawi.

Inaonekana kwamba kila alipo mwafrika sharti pia kuwe na uchawi. Nasema hivi kwa sababu nchi ya Haiti ambayo ina milikiwa na Waafrika waliopelekwa huko nyakati ya biashara ya utumwa, wao kwao uchawi ni kama dini, kwani imani yao ya Voodoo, ina nguvu zaidi ya Imani yao ya dini ya kikristo.

Tumesikia mambo mengi ya ajabu yanayotendeka huko kwa kutumia nguvu hizi za Voodoo. Jambo moja ambalo ni la dhahiri ni kwamba katika mataifa haya ambayo watu wake wanaamini na kushiriki mambo ya uchawi, maendeleo huwa haba sana. Nchi hiyo ya Haiti ni nchi maskini zaidi Amerika kusini, lakini ukweli ni kwamba imani hii ya Voodoo, waliitoa hapa barani Africa. Mambo wanayoyafanya mengine husemekana kuwa yanahusiana na dini na itikadi za kiafrika kwani wao walitoka huku Afrika wakauzwa utumwani, lakini hawakusahau mila na desturi zao za Kiafrika.

Swali linaliobuka ni je, hii ni sayansi au ni imani tu na kama ni sayansi, mbona basi tusiweze kuitumia kwa kuleta maendeleo barani badala ya kurudisha nyuma maendeleo? Siku hizi watu wengi hata wakristo wanaaminika kutembelea waganga na wachawi kwa sababu tofauti tofauti, kukabiliana na changamoto maishani. 

Wenzetu nchi za Ulaya na Marekani wametumia sayansi kwa mambo mengi ya kuwasaidia binadamu, kwa kutengeneza vifaa ambavyo vimerahisisha maisha na hata kumpeleka binadamu kuzuru mwezi na sayari nyengine za ulimwengu huu wetu. Tunasikia kwamba wenye nguvu za uchawi huweza kusafiri safari ya maili nyingi kwa sekunde chache, mbona basi sayansi hii isitumike kurahisisha maisha ya wananchi badala ya kuwaharibia wengine maisha yao?

Mtu akikosana na mwenziwe hata akiwa ndugu yake, atakimbia kwa mganga au mchawi ili kumharibia maisha mtu yule waliyekosana naye, bila ya kufikiria athari za kitendo chake. Kuna familia zinazokumbana na magonjwa yasioyoelezeka na wengine hufikiria kwamba ni kwa sababu ya hila za kichawi. Si rahisi kubaini ukweli, kwani akina Kajiwe sio wengi wanaoweza kutambua wachawi na kuzima nguvu zao za uovu.

Mchawi anayekisiwa kumsaidia aliyekuwa mwanasoka wa timu ya Arsenal kutoka Togo, Emmanuel Adebayor

Ukitaka kujua kama tatizo la uchawi ni kubwa hapa Pwani na Kenya nzima kwa jumla, mijini na vijijini wako waganga wanaotangaza kazi zao za kupambana na magonjwa yanayotokana na uchawi na urogi. Hawangekuwepo waganga hawa kama hawangekuwepo wachawi. Lakini swali ni; je kuna tofauti gani kati ya mganga na mchawi?

Watu wengine huishi wakihofia maisha yao na hata wengine huhama makao yao wakihofia nguvu za uchawi.

Visa tunavisikia vya washukiwa wa uchawi wakiuawa kwa kuchomwa au kukatwakatwa kwa mapanga na jirani zao wanaowashuku kuwa wachawi. Je inatosha kwamba dhana inaweza kuwa sababu ya kumuua jirani yako? Ukiulizwa kutoa ushahidi wa uchawi, je unaweza kuutoa ushahidi huo?

Kuna maswali mengi ambayo hayana majibu kuhusu imani hii ya uchawi, lakini ukweli si rahisi kubainika ila pengine kwa yule mwenye nguvu na kipawa cha kumtambua mchawi, ikwa kweli uchawi upo. Sijui wewe mwenzangu, je unaamini kwamba uchawi upo? Ikiwa umeshuhudia visa vya uchawi au matukio ya ajabu yanayolingana na uchawi, tafadhali tufahamishe ili tuendeleze mjadala huu.