Serikali ya Kenya yalaumiwa kwa madai ya kuendeleza mapendeleo

Baadhi ya wakazi wa Kaunti ya Kakamega kwa upande wao wamelalamikia kutelekezwa na serikali ya Kitaifa kwa upande wa miradi ya maendeleo.

Wakiongozwa na Boaz Shikuku wamesema miradi ya Serikali ya kitaifa inatekelezwa kwa mapendeleo ikiegemea upande mmoja huku eneo la Magharibi likitelekezwa.

Aidha, wamedai kwamba hakuna mradi wowote kutoka kwa serikali ya kitaifa ambao umefanyika kwenye kaunti hiyo huku ujenzi wa Barabara ya Lurambikupitia Nambacha hadi Musikoma Kwenye kaunti ya Bungoma ukiwa umesitishwa.

Vilevile, wamelalamikia kufungwa kwa kiwanda cha sukari cha Mumias huku Rais akizindua miradi mipya eneo la Nyanza.

Wikendi iliyopita baadhi ya viongozi wa eneo la Magharibi akiwamo Mwakilishi wa Kike wa Kakamega Elsie Muhanda walimlaumu Rais Uhuru Kenyatta kwa madai ya kubagua maeneo mengine na kuelekeza miradi ya mabilioni ya fedha kwenye eneo jirani la Luo Nyanza.