For the best experience, please enable JavaScript in your browser settings.
Zaidi ya wasichana 20,000 hupachikwa mimba kila mwaka katika kaunti ya Kakamega asilimia kubwa wakiwa wamo chini ya miaka 16. Haya ni kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na shirika la AMREF kaunti hiyo ambapo ilibainika, Kakamega imo miongoni mwa kaunti tano nchini zinazoandikisha idadi ya juu ya wasichana wanaopachikwa mimba. Kaunti zingine ni Nairobi, Kilifi, Bungoma na Nakuru. Kulingana na Sylvia Wamugi (Afisa msimamizi wa AMREF Kakamega) zaidi ya wasichana 50 hupachikwa mimba kila siku kaunti hiyo huku maeneo bunge ya Shinyalu, Matungu na Malava yakiwa kati ya maeneo ambayo yanaongoza kwa visa hivyo.
Kando na upachikaji wa mimba, jinsia ya kike pia imo katika hatari ya kudhulumiwa kimapenzi ikiwemo kubakwa, kunajisiwa pamoja na kuozwa wakiwa na umri mdogo kinaya ikiwa jamaa waliojukumiwa kuwalinda na kuwakuza wakitajwa miongoni mwa wanaoendeleza dhulma dhidi yao na kuhatarisha kizazi kijacho. Kwa kipindi chini ya mwezi mmoja zaidi ya visa 10 vya dhulma kwa wanafunzi wasichana vimeripotiwa kaunti hii nyingi zikihusishwa na jamaa wa karibu huku waathiriwa wakikosa kupata haki nao washukiwa wakikosa kuchukuliwa hatua zozote zile.
Visa angavu
- Octoba 9 mwaka huu eneo bunge la Lurambi, kisa cha baba wa miaka 53 kumnajisi mwanao wa miaka 14, mwanafunzi wa darasa la 7 kiliripotiwa. -Inaarifiwa kuwa mshukiwa alitekeleza uovu huo wakati mamake mwathiriwa alikuwa ameenda kuhudhuria hafla ya mazishi kule Kabras ambapo babake mwanafunzi huyo alilazimishwa kushiriki ngono na yeye huku akimtishia kutogharamia mahitaji yake ya kila siku ikiwemo ile ya shule iwapo hawata shiriki tendo hilo. - Octoba 15 eneo bunge hilo hilo, kisa kingine cha babu wa miaka 80 kumnajisi mjukuu wake wa miaka 12 mwanafunzi wa darasa la 3 kiliripotiwa. Aidha mwathiriwa alifichuwa kuwa babu huyo ambaye amewahi stakiwa kwa kosa la kumnajisi mwanafunzi wa darasa la nane amekuwa akimtendea uovu huo mara kwa mara kwa kumhadaa na shilingi tano na viperemende na kisha kumwonya dhidi ya kumfichulia yeyote.
Novemba 5 eneo bunge la Malava, kisa cha baba wa miaka 50 kumnajisi na kumpachika mimba mwanao wa miaka 13 pamoja na kumnajisi mtoto mwingine wa dadake wa miaka 14 kiliripotiwa, huku mshukiwa akijitetea na kusema alitenda uovu huo kwa sababu ya upweke wa kuachwa na mkewe aliyemtoroka baada ya kumpachika mimba mwanawe.
Octoba 6 eneo bunge la Lurambi kisa kingine cha mwanaume wa miaka 56 kumnajisi msichana wa miaka 14 mwanafunzi wa darasa la 5 kiliripotiwa pia huku mwathiriwa akifichuwa kuwa mshukiwa huyo alimhadaa na shilingi 20 kabla ya kumnajisi. Hizi ni baadhi tu ya visa vilivyoripotiwa majumaa kadhaa zilizozipita nyingi zao zikiwa ni za mazoea kwa washukiwa huku haki ikikosekana kwa waathiriwa nalo swala la umaskini likijitokeza. Je utepetevu uko wapi?
Wazazi
Ni jukumu la mzazi kumkuza mwanawe kwa njia inayofaa ikiwemo kumshauri jinsi yakujilinda wakati wake wa ujana. Imebainika visa vingi vya dhulma kwa wasichana hutokea kati ya waathiriwa na jamaa zao wa karibu hii ikiwa na maana kuwa wazazi haswa wale wa kike wamefeli pakubwa kuwalinda wanao kwa kuwaacha mikononi mwa watu wasioaminika.
Swala la wazazi kuona soni kwa kuwafunza wanao kuhusiana na madhara ya kushiriki ngono za mapema imetajwa pia kama sababu ya kuongezeka kwa mimba hizi za mapema huku wazazi wakitakiwa kuwapa mwanga wanao na ufahamu kuhusiana na swala hili ili kuwaepusha kupachikwa mimba hizi zinazoletwa na wao kufanyia miili yao majaribio. Umaskini katika familia imetajwa pia kama kichochezi kinachoiharibu jinsia hii huku wasichana wengi wakiishilia kufanya ukahaba ili kujikimu kimaisha kwa kujinunulia mahitaji yao ya kila siku.
Serikali
Kwa kusema serikali na maanisha vituo vya usalama vikiwemo vituo vya polisi, machifu pamoja na wazee wa nyumba kumi. Imekuwa kinaya kuona vikosi hivi vinavyotegemewa kukomesha visa vya dhulma vikiwa ndivyo vinavyochochea na kuzidi kuikandamiza jinsia hii nyingi za visa hivyo vikikosa kuchukuliwa kwa uzito na kulazimisha familia kusuluhisha visa hivyo kupitia njia za mkato, maelewano baina ya familia ya mshukiwa na mwathiriwa huku waathiriwa wakibaki kuathirika. Pia swala la ufisadi limejitokeza maafisa hawa wakilaumiwa kushrikiana na washukiwa na kuzihangaisha familia husika kila wanaporipoti visa hivyo ambavyo wao hulazimishwa kugharamia gharama za uchukuzi kabla ya mshukiwa kukamatwa huku wengine wakisuluhisha visa hivyo kinyumbani kwa familia kulipwa fidia ndogo ndogo kama kuku na pesa.
Wanafunzi wenyewe
Zaidi ya walimu 18 kaunti ya Kakamega walifutwa kazi mwaka uliopita kwa kupatikana na madai ya kuhusika moja kwa moja na maswala ya mapenzi na wanafunzi. Ilahali tunajaribu kuiokoa jinsia hii, wao pia wamekuwa walegevu wengine wakijivalia vijisketi vidogo na kuwavutia walimu wa kiume pamoja na vijana wengine ambao huishilia kuwanajisi ama kuwashawishi kushiriki nao tendo hilo wengine wakipachikwa mimba za kiholela.
Hatua ya kuikabili
Ni kutokana na furaha iliyoko ya kushiriki ngono miongoni mwa vijana walio balehe ndio kumechangia kuongezeka kwa visa vya wasichana kupachikwa mimba za mapema wengi wakilazimika kuacha shule. Wito umetolewa kwa wazazi, walimu pamoja na wahusika kuwaelimisha wanao kuhusu umuhimu wa kutumia njia za kupanga uzazi ikiwemo kutumia sindano pamoja na mipira ya kondomu iwapo ni lazima washiriki ngono huku wale ambao hawajawahi shiriki tendo hilo wakishauriwa kuepukana nayo hadi wakati wao utakapofika ili kujiepusha na visa vya mimba za mapema. Serikali nayo kupitia kwa wizara ya elimu inatakiwa kuanzisha vipindi vya masomo kuwaelimisha wasichana jinsi ya kujilinda na kuepukana na mimba za mapema. Pia wakati huu ukiwa ni msimu wa likizo ndefu, wazazi wanashauriwa kuzingatia mienendo ya wanao kwa ukaribu pamoja na kuwajukumisha kupitia talanta zao na kuhakikisha wana kazi kwani wengi huishilia kwa maswala ya ngono kwa kukosa kazi ya kufanya. Aidha jamii inashauriwa kujiepusha na mila na tamaduni zilizopitwa na wakati ikiwemo ile ya kuwaoza wasichana wakiwa na umri chini ya miaka 18 pamoja na kasumba ya wasichana kutengewa majukumu ya kinyumbani pekee kama kufua na kupika. Jinsia zote zina haki sawa wote wanahaki ya kupata elimu.
Stay informed. Subscribe to our newsletter