Uwanja wa shule wageuzwa soko la dawa za kulevya Mombasa

Loading Article...

For the best experience, please enable JavaScript in your browser settings.

Picha ya wanaotumia dawa ya kulevya. [Picha: Pambazuko]

Uwanja wa shule ya Msingi ya Freea town umegeuzwa sasa kuwa uwanja wa kuuza dawa za kulevya hasa katika siku za wikendi. Kila siku za Jumamosi na Jumapili uwanja huo hujaa mamia ya watu wengi wao wakitazama mpira huku wengine wakifanya biashara ya kukodisha viti kwa watu ambao wamekuja kutizama mpira,ambao huwa unachezwa hasa kila wikendi katika uwanja huo.

Katika siku hizo ni nadra sana kuona maafisa wa polisi wakizunguka ili kuangalia hali ya usalama iko namna gani, ikizingatiza kuwa kuna idadi kubwa ya watu ambao usalama ungehitajika kwa maana huenda hata zogo likatokea katika uwanja huo. Katika siku hizo za wikeendi pia mimi huenda katika uwanja huo ili kutazima mpira lakini cha kushangaza huwa ninatazama “mpira tafauti,” nilipata mahali nikasimama na kuegemea ukuta wa shule ya Freea Town, ili nipate fursa ya kuuangalia mpira vizuri. Hata hivyo kando yangu kulikuwa na vijana ambao hata wengine walikuwa wamelala na wengine wakiuza bangi na dawa nyengine za kulevya kisiri.

“Oyaaaa mwana kuwa makini na hizo kete anaweza kuwa ni afisa wa polisi huyo hapo, ambaye ameegemea ukuta hapo. Lazima uwe makini mwana kunaweza haribika wakati wowote ama vipi mwana,” akasema mmoja wa vijana hao.

Wasi wasi uliwaingia vijana hao ambao wao wenyewe walikuwa walevi na dawa za kulevya vile vile  walikuwa wanawauzia wateja wao mihadarati hiyo mmoja kwa mmoja, ambao walikuwa wanamiminika wakinunua kwa njia ya kijificha. Ilinibidi niwe makini hata picha ambazo nilizipiga ilinibidi niwe mwangalifu sana wasijue kile nilichokuwa nafanya.

“Nifungie haraka haraka niko job mwana , mwana lakini usiwe unanipiga picha kwani tuko kazi maanake hizo simu zenu nazijua sana unaweza kuwa unatutega sauti halafu utushike,” akasema jamaa mmoja ambaye alifikia pia kununulia mihadarati yake.

Cha kushangaza ni kuwa biashara hiyo inafanywa kwa njia ya upesi Sana hata mtu ambaye haungekuwa makini hangejua ni nini nikichokuwa kinaendelea mahali hapo kwa sababu muda wa dakika ishirini wale wateja ambao walifika kwa wauzaji hao ni zaidi ya 10.

Wasiwasi wangu mkubwa ni kuwa hata baadhi ya wateja ambao wananunua bidhaa hizo no vijana Kati was umri wa miaka 17 na 20 hivi wanaostahili kuwa shuleni. Sikutaka vijana wale kujua ni nini ambacho nilikuwa nafanya kwa sababu licha ya kuwa walikuwa wanavuta bangi hizo hadharani mbele ya umati mkubwa wa watu ambao walikuwa wanatazama mpira sikuwa na budi pia mimi kuuvumilia moshi mkali wa bangi ambao ulikuwa ukifuka hewani na kuwaingiza na wale wasiovuta pia. Jamaa mmoja ambaye hakutaka  jina lake litajwe anasema kazi hiyo imekuwa ikifanywa mara nyingi hasa siku za wekendi ambapo watu wengi huwa wamepumzika.

“Usifikirie watu wengi wanakuja hapa kutazama mpira, wanatazama “mipira” mingi sana hapa. Kazi ndio hiyo ambayo umeiona maunga ndio wanauzia watu dawa za kulevya hapa. “Ukiwaangalia wote hawa ni kama wamelala lakini akili zao ziko imara na wanashuku sana watu wageni ambao hawajawaona hata ukitaka kununua hawakuuzii kitu,” akasema.