Wanakandarasi wa Uchina waliojenga Barabara kuu ya Thika, bado wanadai serikali ya Kenya shilingi milioni 428.6.
Kulingana na Mkaguzi Mkuu wa Serikali, Nancy Gathungu, Hazina ya kitaifa bado haijafuta mswada ambao haujakamilika na pia ameonya kwamba ikiwa serikali itashindwa kufanya hivyo basi walipaushuru ndio watakabiliwa na adhabu zaidi.
Gathungu amesema ukaguzi uliofanywa kwa Mamlaka ya Kitaifa ya Barabara Kuu ya Kenya (KENHA) ulifichua kiasi kamili cha shilingi 428, 623, 554 kufikia Juni 30, 2021.
Ameilaumu KENHA kwa kucheleweshwa malipo hayo.
Ameongeza kwamba Benki ya Uchina ya Exim ambayo ilifadhili mradi huo, haijalipwa shilingi bilioni 3. 6 ambazo zilitumika kujenga barabara ya Nairobi Southern Bypass.