Mwenyekiti wa Tume ya IEBC Wafula Chebukati. [Standard]

Tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC itaanza rasmi shughuli ya kukagua upya mipaka ya maeneo bunge yote nchini kuanzia mwezi Machi 2019.  

Shughuli hiyo ya kikatiba ya hulazimika kufanywa kila mara moja chini ya muda usiopungua miaka minane. Ukaguzi huo unapaswa kukamilika mwaka mmoja kabla ya uchaguzi mkuu.

Mwenyekiti wa tume hiyo Wafula Chebukati alidokeza kuwa kufanikiwa kwa shughuli hiyo itategemea pakubwa na uwepo kwa fedha.

"Kwa upande wetu, tume ipo tayari kuanza kutekeleza shughuli ya kukagua mipaka isipokuwa uwepo wa fedha utachangia pakubwa kufanikisha zoezi hili,” Chebukati alisema.

Chebukati alidokeza kuwa tayari wameiandikia barua shirika la kitaifa la takwimu (KNBS) ili kupewa matokeo rasmi ya sensa iliyofanywa mwaka jana.

"Tumeiomba shirika la KNBS itupatie ripoti na matokeo kamili ya sensa ya mwaka 2019," alisema chebukati.

Ripoti ya sensa ya mwaka jana ilopotolewa wanasiasa waliikashifu na kuipaka tope takwimu zilizotolewa kwa madai kuwa hazikuwa zinadhirisha hali halisi ya idadi ya watu mashinani.

Baadhi ya wanasiasa wanahofia kuwa huenda tume ya IEBC itatupilia mbali maeneo bunge kadhaa endapo itatumia ripoti hiyo.

Magavana Muthomi Njuki (Tharaka Nithi), Francis Kimemia (Nyandarua), Wycliffe Oparanya (Kakamega) na John Nyagarama walitishia kwenda kortini kuishinikiza shirika la knbs kurudia shughuli ya kuhesabu watu.

"Hatujaridhishwa na matokeo hayo ya sensa, na kama tume hiyo haitachunguza na kubadili takwimu hizo, basi hatatukuwa na budi ila kufika mahakamani na kuomba kubatilishwa kwa matokeo hayo".  Njuki alisema mwaka jana.

Shughuli ya ukaguzi wa mipaka hutegemea pakubwa takwimu za sensa, historia ya jamii ya eneo husika, uwepo wa miundo msingi, na hali ya uchumi ya eneo ili kuweka mipaka mipya ama kusalia kwa mipaka iliyopo.