Kaunti ya Mombasa ni kivutio cha utalii kutokana na bahari na mandhari safi ya kupendeza ila cha kushangaza ni kwamba Mombasa umekuwa mji ambao unazidi kutiliwa shaka kutokana na visa vya utovu wa usalama. Licha ya waziri wa usalama wa ndani Dakta Fred Matiangi kuzuru Mombasa na kutoa onyo kali na mageuzi katika idara ya usalama, magenge mapya yanaendelea kuchipuka hapa Mombasa.
Kulingana na ripoti iliyotolewa na shirika la kutetea haki za binadamu la Haki Afrika, watu 40 wameripotiwa kuuawa na magenge ya kihalifu katika kipindi cha mwaka mmoja, huku washukiwa 30 wa magenge hayo, ndio ambao wamekamatwa na maafisa wa polisi kufikia sasa.
Magenge hayo hatari ya kihalifu yanawahangaisha wakazi hasa katika maeneo ya Kisauni, Nyali, Likoni na Mji wa Kale. Kuna baadhi ya maeneo hasa katika eneo bunge la Kisauni, wapangaji wengi wamehama kutokana na magenge ambayo yamekuwa yakiwahangaisha wakazi huku wafanyibiashara za nyumba wakikadiri hasara inayosababishwa na ukosefu wa wapangaji.
Hivi punde zaidi watu 12 walijeruhiwa kwenye shambulizi inayodaiwa yalitelezwa na kundi lililochipuka hivi karibuni la 86 Batallion, katika mtaa wa Free Town eneo bunge la Nyali. Miongoni mwa makundi hayo ya kihalifu ni pamoja na Wakali Kwanza Wakali Pilipili, wakali wao, wajukuu wa bibi, akili za kiusiku, vijana wa leba, na 86 batalion miongoni mwa makundi mengine.
Katika mtaa wa Mtopanga ninakutana na Zawadi Katana mjane mwenye watoto wawili, akiwa mwingi wa mawazo. Anasimulia jinsi vijana wadogo wa umri wa mtoto wake walivyomua mumewe, alipokuwa akibarizi wakati usiku. Anasema muda waliotumia maafisa wa usalama kufika kwenye eneo la tukio, haukuwa wakuridhisha ikizingatiwa kwamba vijana hao walishambulia maeneo hayo kwa takribani saa moja.
READ MORE
KRA in fresh plan to weed out graft at port
Junior golfers set for battle at Nyali course
“Vijana wadogo sana walivamia na kumkatakata mume wangu kwa mapanga, na kuniachia mzigo mkubwa sana. Vijana hawa wamewahangaisha watu wengi sana,” akasema Zawadi ambaye alijawa na mengi majonzi. Lakini je ni nini kinachowafanya vijana wadogo kujiingiza katika magenge haya? Gazeti la Pambazuko lilikukutana na Sniper ambalo silo jina lake halisi na tukakubaliana kwa sababu za kiusalama tulibane jina lake hakika, kwani anasema alikuwa mwanachama wa kundi la Wakali Wao linaloorodheshwa miongoni mwa makundi hatari zaidi hapa Mombasa. Akibainisha chanjo cha kujiingiza kwenye kundi hilo la kihalifu alitaja ukosefu wa ajira na kukaa bila kitu cha kufanya ndiko kulikomfanya kujiunga na kundi hilo. Anakumbuka jinsi wandani wake walivyojitenga punde alipotiwa mbaroni na raia waliokuwa na ghadhabu kali.
“Uhalifu wataka kitu kidogo, nikichukua kitu kidogo napata pesa ya haraka. Niliketi mitaani bila shughuli ya kufanya, na nikaona nijingize katika kundi hili, lakini saa hii nimeacha hata nafanya kazi yangu ya bodaboda,’ akasema Sniper. Anadai kuwa fedha alizokuwa akizipata kupitia kupora wakaazi hazikumsaidia badala yake alizitumia kiholela kwa misingi kuwa atapata nyengine.
Anadai kuwa aliasi kundi hilo kutokana na ushauri kutoka kwa baadhi ya marafiki, hali iliyochangia kuwepo na kisasi baina yake na wafuasi wa genge hilo. Hata hivyo anawashauri vijana wenzake ambao walijingiza katika makundi ya kihalifu kuachana na uhalifu akisema hakuna manuafaa yeyote mtu anayopata. Idara ya usalama kupitia kamanda wa Likoni Jane Munywoki inasema, ingawa changamoto za polisi zipo lakini juhudi zao za kuwasaka na kuwakamata wahalifu hazilali.
“Tunaendelea na mikakati ya kuyasaka mageni ya kihalifu hivyo tunawataka wazazi wawatunze watoto wao kwa sababu wengi wao wana umri mdogo sana, wa kati ya miaka kumi hadi kumi na mitatu,’ akasema Munywoki. Polisi hapa Mombasa wanazidi kutoa wito kwa wazazi na wakaazi kwa ujumla kufanya kazi pamoja nao katika kutoa taarifa zitakazopelekea kuwakamata wahalifu hao. Shirika lisilo la serikali la Haki Afrika linashikilia kuwa kulingana na utafiti wao watu 40 wameuawa mikononi mwa makundi haya ya kihalifu katika kipindi cha mwaka mmoja, huku wahalifu 30 wakiuawa na kukamatwa kwenye makabiliano na maafisa wa polisi.
Polisi nao yadaiwa kuzembea kazini na kula milungula hali inayochangia kuathirika kwa usalama. Afisa wa Kitengo cha dharura kwenye shirika lisilo la kiserikali la Haki Afrika Mathias Shipeta anaeleza kwamba magenge haya yalichipuka kama makundi ya kucheza mpira kabla ya kuingilia uhalifu katika maeneo ya kisauni. Baadaye walikosa wafadhili wa kuwasaidia kukuza vipaji vyao hali iliyochangia kugeukia uhalifu. Kadri muda ulivyozidi kusonga kuliibuka kundi lengine lililojiita Wajukuu wa Bibi nalo makazi yake yakawa ni Likoni na viunga vyake.
Genge la vijana wa labour nalo yadaiwa kuwapa ulinzi wanasiasa katika kampeni kabla ya kuingilia uhuni uchaguzi ulipoita, hivyo Shipeta anasisitiza kwamba ongezeka la uhalifu Mombasa limechangiwa sana na siasa. “Wanasiasa wengine waliwatumia vijana hawa na kuwaahidi mambo ambayo hawakuyatekeleza na imechangia pakubwa sana vijana hao kujiunga na uhalifu,” akasema Shipeta.