Juma lililopita tulianza kuzungumzia mti unaoitwa muembe, na tukasema unapata asili yake katika sehemu za mpaka wa India na Burma. Maelezo zaidi yanasema miembe hupatikana katika kanda nzima ya milima ya Himalaya Mashariki kwenye mpaka wa Burma na India.  Kabla hatujaendelea tungependa kuwafahamisha neno la kizungu Mango lilikotoa asili yake.

Kwanza kabisa lazima tufahamu ya kwamba Mreno ndiye aliyekuwa wa kwanza kusafiri katika sehemu mbali mbali za dunia kutoka bara la Ulaya, na ndiye aliyekuwa wa kwanza kufika katika sehemu hizi na kupata tunda hili miongoni mwa mimea mingine kama vile mikanju na kadhalika. Kulingana na habari, neno Mango lilitokana na lugha ya Kimalay ambayo ni asili ya lugha ya Kitamil ambako maembe wanayaita Maangay.

Lakini kabla ya kuitwa Maangay liliitwa aamkaay, kisha maamkaay na hatimaye maangai. Hadi Vasco da Gama alipofika Calicut mji bandari wa sehemu za Malabar katika Pwani ya Kerala tunda hili embe lilikuwa halijulikani kabisa katika bara la Ulaya. Wareno walichukua jina la Kimalaya la Maanga na kulitumia kuliita tunda la muembe, lakini wakatoa ‘a’ moja kwenye neno maanga wakatumia neno “manga.”

Mmoja wa Wareno waliowasili Calcut akamwandikia barua rafiki yake Mwingereza kumfahamisha ya kamba wamepata tunda jipya nchini India linaloitwa ‘manga.’ Hizo ni siku ambazo hata mtambo wa kupigia chapa, yaani typewriter, ilikuwa haijagunduliwa, hivyo barua hiyo iliandikwa kwa mkono. Rafiki huyo mwingereza alilisoma neno ‘manga’ kama mango kwa vile maneno mengi ya Kireno yanaishia na hati O na mengi ya maneno yaliyopatikana katika ulimwengu mpya, yalikuwa yanaishia na ‘o’ kama vile avocado, potato, tomato na kadhalika. Kuanzia hapo neno Mango likaingia katika msamiati wa lugha ya Kiingereza.  

Habari nyingine kuhusu muembe zinatufahamisha ya kwamba taarifa kuhusu mti huu zilianza kuchapishwa kwenye vitabu katika lugha ya Sanskrit ambapo embe lilikuwa likiitwa Amra. Kulingana na taarifa hizo miembe imekuwa ikistawishwa na mwanadamu kwa zaidi ya miaka elfu nne. Imeelezwa kwamba mmoja wa wasafiri wa siku za awali kabisa kwenda nchini India kabla ya wasafiri wa baza Ulaya, aliyeitwa Hsiian-Tsang kati ya miaka ya 632 hadfi 645, ndiye aliyekuwa mtu wa kwanza kupeleka habari za miembe nje ya India.

Tunda hili liichukua nafasi kubwa katika kilimo cha matunda wakati wa falme za Moghul nchini India na Mfalme Mkuu Akbari The Great, ambaye alikuwa na shamba la miembe laki moja, katika miaka ya kuanzia 1556 hadi 1605. Aina mbali mbali za miembe iliyoimarishwa kupitia harakati mbali mbali za kiutafiti nchini India zinapata asili yake katika miaka hiyo.

Kitabu cha kumbu kumbu kuhusiana na ustawi wa tunda hili kilichoandikwa mwaka wa 1590 AD, kinachoitwa Ain-e-Akbari, yaani Encyclopedia Ain-e-Akbari, kina maelezo thabiti kuhusu maembe, aina zake mbali mbali na taratibu zake.  Kilimo cha maembe katika kanda ya Kusini Mashariki mwa Bara la Asia kilipatikana katika nchi za Ufilipino, Indonesia, Java, Malaysia na Sri Lanka. Usambazaji wa mmea huu katika nchi za Afrika Masahariki na Afrika Magharibi na baadaye huko Brazil ukafanyika katika karne ya kumi na sita. Mexico ilianza kupanda miembe katika karne ya kumi na tisa.

Miembe ilianza kupandwa huko Florida mwaka 1833. Kabla ya kufanywa miti ya kilimo cha kawaida katika mashamba, miembe ilikuwa miti ya mwituni nchini India. Utafiti mwingine unaeleza kwamba miembe ilisambazwa katika nchi ya China mnamo karne ya saba AD, ilhali miembe ilianza kupandwa katika kanda ya Afrika Mashariki katika karne ya 10 AD na kwingineko katika karne ya kumi na sita. Habari zinasema kwamba miembe mingi inayopandwa duniani siku hizi ni ile iliyofanyiwa utafiti huko Florida.