Leo hii Mombasa ni mji uliokua na kujengwa si haba, huku matokeo ya hesabu ya watu yalotolewa majuzi yakionyesha kwamba sasa hivi Mombasa iko na idadi ya watu 1,208,333.
Mji huu ambao ndio kitovu cha biashara na viwanda katika eneo la pwani pamoja na kuwa mji mkuu wa pili nchini, uko na historia ndefu ambayo imejumulisha karne nyingi zilizopita.
Mwanajiografia wa kale Ibn Batuta aliyewahi kuzuru pwani ya Afrika Mashariki aliandika katika kumbukumbu zake zinazo tambuliwa rasmi na wanahistoria pamoja na wataalamu wa sayansi ya akiolojia maelezo kuhusu mji unaoaminiwa kuwa Mombasa kwenye miaka ya 1300s.
Katika baadhi ya maandishi yake, mwanajiografia na mtembezi huyo mwenye asili ya Morocco, alieleza kukuta mji uliokuwa na makazi ya wenyeji na misikiti iliyojengwa kwa mbao.
Kwa mujibu wa chapisho la kiutafiti ‘Mombasa – Archaeology and History’ liloandikwa na msomi Herman Kiriama, Ibn Batuta pia hakuwa mtembezi pekee wa zama za kale alowahi kuutaja mji huo. Mwanajiografia mwengine, Muhammad Al-Idrisi, aliyewasili pwani ya Afrika Mashariki miaka mingi kabla ya Ibn Batuta alieleza wasifu wa Mombasa takriban miaka ya 1100s kuwa mji uliochangamka kibiashara na wenye bandari nzuri kwa uchukuzi wa baharini.
READ MORE
Kenya grabs golf title in this year's EAC Inter-parliamentary games in Mombasa
Let new railway station reflect Mombasa's growth and heritage
Kenya faces ban as Tong-IL Moo-Do International Martial Arts event hangs in balance
“Mji huu uko eneo la pwani na kwenye kisiwa ambacho chombo cha baharini chaweza kukizunguka kwa siku mbili,” Al-Idrisi amenukuliwa katika chapisho la Herman Kiriama.
Hata hivyo wanahistoria wameeleza kwamba japo kuna ushahidi wa kutosha kwamba Mombasa ni mji uliokuwa umejengeka kwa karne nyingi zilizopita, visa tofauti tofauti vya uvamizi vilisababisha watu kutawanyika na miji yao kubomolewa katika vipindi mbalimbali vya historia.
Ushahidi wa hivi majuzi ambao Wakenya wengi sasa wanaujua ni uchimbuzi ulofanywa na wajenzi wa ukarabati wa bustani la Mama Ngina walipochimbua mabaki ya kijiji cha Waswahili wa zamani mahala hapo. Inaaminika kwamba Waswahili walokuwa wakiishi hapo takriban karne ya 15 walilazimika kuhama walipokuwa wanakimbia mashambulizi ya Wareno walokuwa katika kampeni ya kuteka kisiwa cha Mombasa.
Simba na Chui Vilevile katika maelezo ya Waingereza walowasili Mombasa mnamo karne ya 19, yanatoa picha nzuri zaidi ya wasifu wa mji wa Mombasa jinsi walivyoukuta mwishoni mwa karne hiyo. Wengi katika kizazi cha sasa huenda wakafurahishwa kujua kwamba Mombasa ya kitambo ilikuwa ni msitu ambapo wanyama hatari kama akina Chui, Simba pamoja na nyoka wenye sumu kali walikuwemo.
Kwa mujibu wa kitabu ‘Mombasa the Friendly Town’ kilichoandikwa na John H.A. Jewell na kinacho elezea historia ya Mombasa, kimenukuu kumbukumbu za Waingereza kuhusu visa fulani ambavyo wakati huo bila shaka vilikuwa ni vya kujaza hofu kubwa.
Hakukuwa na barabara “Utakapotoka nje ya njia nyembamba za mji wa kale, kulikuwa hakuna barabara isipokuwa vijinjia vya kupitia watu kwa miguu,” amenukuliwa Mwingereza Charles Hobley kwenye maandishi yake ya mwaka wa 1890.
“Hata njia ya kuelekea Kilindini ilikuwa na upana wa kama futi nne pekee na ilipenyeza kwenye msitu ambao ulikuwa umeizunguka. Msitu huo ulikuwa umejaa Bafe (aina ya nyoka hatari) ambao ungewaona wengi ukiwa unatembea,” aliandika Hobley.
“Chui walikuwa wakizurura zurura nyakati za usiku huku wakivamia mbuzi za wenyeji mara kwa mara, na siku moja asubuhi habari zilichipuka kwamba Chui mmoja alikuwa amelala kwenye mti mkubwa sehemu ya kusini mwa barabara kuu.” “Hata hivyo alitokomea msituni kabla tuchukue bunduki zetu (kwenda kumwinda),” alieleza Mwingireza huyo kwenye sehemu ya chapisho lake ‘A Guide to Mombasa and Surroundings.’
Pia alirekodi kwamba miaka miwili baada ya kuwasili kwake Mombasa, aliwahi kuhusika katika uwindaji wa Simba humo kisiwani! Mwandishi John Jewell pia anaeleza kwamba mwaka ule wa 1890 ambapo Charles Hobley alisimulia kisa cha Chui kuzurura maeneo ya mji wa kale, mzungu mwengine pia aliwahi kuua Simba.
“Mwaka huo huo Count Etienne de Kiegle aliua Simba huko Tudor kwa kumtegea chambo cha ng’ombe aliomfunga kwenye mti halafu yeye akapanda juu ya mtu huo kumngojea,” ameandika Jewell.
Mnamo Februari 1945 Simba watatu waliuawa, na hata takriban miaka 60 tu iliyopita kisa chengine cha wanyama pori pia kimetajwa.
“Na hata hivi karibuni mwaka wa 1958 Chui mmoja hatimaye alipigwa risasi kwenye pori la mibuyu baada ya kumaliza wiki kadhaa humo kisiwani akivamia mbwa na kuwafanya kitoweo,” imesimuliwa.
Ukizingatia kwamba leo hii kila pembe ya kisiwa cha mji wa Mombasa, yaani eneo la Mvita, imejengwa majumba ya kila aina yakiwemo magorofa makubwa ni ngumu kuvuta taswira ya jinsi sehemu hiyo ilivyokuwa miaka 60 pekee iliyopita. Sasa ikiwa eneo la Mvita tu kulikuwa na akina Simba na Chui je sehemu za Kisauni, Changamwe, Likoni, Nyali na Jomvu ilikuwaje?