Kwa mujibu wa chama cha wasafirishaji mashehena kwa njia ya barabara, wanaharakati wa haki za kibanadamu na viongozi wengine Mombasa, suala tata linalohusu usafirishaji wa mizigo kupitia reli ya SGR limeishia kufanyiwa mzaha na serikali kuu.
Huku wakikariri sababu yao ya kuendeleza msururu wa maandamano mapema wiki hii, chama hicho cha wasafirishaji (KTA), kilifichua kuwa hadi kufikia mwishoni wa wikiendi iliopita amri ya kusimamisha kwa muda uamuzi huo ilikuwa bado haijatekelezwa bandarini Mombasa.
“Kufikia leo hii saa kumi na mbili jioni, Halmashauri ya Bandari (KPA) bado inasafirisha mizigo yote inayoelekea bara bila ya kuwapatia wenye mizigo hiyo uhuru wa kuchagua njia gani ya usafiri wangependa kutumia,” ilisema taarifa ya chama cha KTA wikiendi iliyopita.
“Waziri husika alitangaza kwa ulimwengu wote Alhamisi ya tarehe tatu mwezi Oktoba kwamba hiyo amri ilikuwa imesimamishwa (kwa muda) lakini hadi kufikia jioni ya leo meneja husika wa KPA bado anasubiria amri hiyo (rasmi) kwa maandishi,” ilisema taarifa hiyo.
“Ni wazi sasa kwamba tangazo lile (la waziri) lilikuwa ni la kuwahadaa umma ili kupunguza ghadhabu (zao),” iliendelea kusema.
READ MORE
Githere swings to victory in Mombasa course
Preparations in top gear for second edition of Sotet golf tournament
Mombasa own source revenue increases by Sh90 billion
Why Kenya should turn from diesel to electric trains as it extends railway
Hivyo basi, kulingana na tathmini hii ya KTA, bodi ya chama hicho ilifikia uamuzi wa kuendeleza msukumo wa maandamano ya amani Jumatatu ya wiki hii kwa kile wanachokiona kama kuchezewa shere za serikali kwenye suala hilo. Katika maandamano yenyewe yaliofuatia siku ya Jumatatu kama walivyo ahidi, maafisa wa polisi walitubua maandamano hayo katika vuta nikuvute ambayo hatimaye iliishia kwa baadhi ya wakereketwa hao kukamatwa.
Takriban watu 20 hivi walitiwa mbaroni baadhi yao wakiwemo mkuu wa shirika la Haki Afrika Hussein Khalid pamoja na viongozi wa shirika la wafanyi biashara, Fast Action Business Community.
Matukio haya sasa pia yanaendelea kuongeza chumvi kwenye dhana nzito za baadhi ya wakereketwa Mombasa kwamba viongozi wa kisiasa wa eneo hilo huenda ‘wamekosa meno ya kung’ata’ katika juhudi za utetezi.
Itakumbukwa kwamba majuzi tu wakati Waziri wa Usafiri James Macharia alipotoa tangazo la kuamrisha upya kusimamisha agizo la ulazimishaji wa usafiri wa shehena zote zinazoelekea bara moja kwa moja kupitia reli ya SGR, alikuwa ameandamana na viongozi wa pwani wakiongozwa na gavana wa Mombasa Hassan Joho.
Mkuu wa KPA Daniel Manduku pamoja na mwenzake wa Shirika la Reli Philip Mainga pia walikuwepo. Gavana Joho alieleza imani yake kwamba tatizo hilo ambalo limelaumiwa kunyonya uchumi hasa wa mji wa Mombasa litapata suluhu mwafaka.
Hata hivyo siku ya Jumatatu ambapo maandamano hayo yalifanywa, mbunge wa Mvita Abdulswammad Nassir hakuuma maneno alipoulizwa kuhusu matokeo ya makubaliano ya viongozi wa Mombasa na serikali majuzi.
“Ni wazi kwamba (serikali) walidanganya, kwa sababu hakujakuwa na tofauti yoyote (bandarini) hadi sasa. Walidanganya,” alisema Abdulswammad.
Katika sarakasi nyengine iliyoshuhudiwa wiki iliyopita kuhusiana na suala lilo hilo, mbunge wa Kisauni Ali Mbogo alikumbana na hasira za wanaharakati ambao walimzuia kutoendelea na hotuba yake kwa wanahabari kwa sababu ya kuonekana ‘kumsafisha’ rais Uhuru Kenyatta juu ya jambo hilo.
Isitoshe, wakereketwa wa chama cha Fast Action Business Community walionekana kukerwa sana pale mjumbe huyo wa Kisauni alipowashauri kusitisha maandamano yao kwa misingi kuwa tatizo hilo serikali imeshalishughulikia.
Hivyo basi kutokana na hali halisi ya mambo bandarini hadi kufikia mwanzoni wa wiki hii ambapo inaonekana kuwa amri ya waziri Macharia bado haijatekelezwa wala amri hiyo haijawasilishwa rasmi kwa usimamizi wa KPA, huenda viongozi wa kisiasa Mombasa walichezwa shere na serikali kuu?
Itakumbukwa pia kwamba jambo kama hilo hilo tayari limeshashuhudiwa siku za hivi karibuni ambapo waziri Macharia alitoa agizo kama hilo lakini halikutekelezwa, hali ambayo ndio iliyopelekea kuanzishwa kwa misururu ya maandamano kupinga sera hiyo.