Mpigambizi Mswidi Volker Bassen ambaye alitoka ndani ya maji akipepetwa na roho akisema aliyoyaona chini ya bahari hayaelelezi kamwe.

Tukio la Mswidi mpiga mbizi aliyejitolea kusaidia katika juhudi za kuopoa miili ya mama na mwanawe waliozama baharini kutangaza kushindwa kwake kufaulu kama alivyo kuwa ameahidi mwanzoni limezua gumzo kubwa miongoni ya Wakenya.

Gumzo hilo limejaa shaka na dhana kwamba huenda mzungu huyo hakushindwa kupata gari yenyewe humo baharini ila huenda alinyoroshwa na mkono wa chuma wa serikali kueleza Wakenya kwamba hakufaulu.

Wakati juhudi za kuopoa miili ya mama Mariam Kighenda na mwanawe Amanda Mutheu zilikuwa bado hazijafua dafu wiki iliyopita, Mswidi Volker Bassen alijitokeza na kueleza imani yake kuwa kazi hiyo angeweza kuifanya kwa muda mchache sana.

Siku ifuatayo Bassen akakaribishwa rasmi na vitengo husika ili kushirikiana nao kuipata gari ilozama na hatimaye kutoa miili ya wawili hao ambayo hadi kufi kia wakati huo ilikuwa imelala kwenye matumbo ya bahari ya Kilindini.

Kwa mujibu wa mzungu huyo hapo mwanzo, alitathmini shughuli hiyo angeweza kuitekeleza ndani ya takriban masaa mawili kwa kutegemea vifaa vya kiteknolojia na tajriba alionayo katika fani ya upigaji mbizi.

 Hata hivyo, hadi kufi kia Ijumaa wiki iliyopita, Mswidi huyo akaeleza kwamba hali za operesheni hiyo hazikuwa kama alivyofi kiri na kwamba juhudi hiyo ilikuwa ngumu mno. Hivyo basi akaomba msamaha kwa kutofanikisha ahadi yake ya mwanzoni.

Habari hiyo Wakenya wameipokea kwa mchanganyiko wa hisia, ambapo wengi wao wanalipigia domo tukio hilo hasa kwenye ulingo wa mitandaoni na maredioni ambapo walijieleza huru fi kira zao.

Wengine wamemkashifu Mswidi huyo Volker Bassen, wengine wamemsifu na kumshukuru huku wengine wengi vilevile wanajiuliza maswali kuhusu mazingira yalojiri kupelekea kwake kutoa taarifa hiyo.

Kwa wanaoshuku mazingira hayo, wameiona kauli ya mzungu huyo kusukumwa na mkono wa serikali uliomlazimisha kuongea na vyombo vya habari na kutoa maneno ambayo serikali ilitaka ayatoe. Hili, wanadai wengi wenye fi kira hizo, lilisukumwa ili kuikinga serikali na aibu ambayo imeikumba kutokana na kushindwa kwao kuiopoa miili ya Mariam Kighenda na mwanawe hadi kufi kia wakati huo.

Isitoshe, dhana hii imeambatana na imani kuwa huenda Mswidi huyo aliweza kuipata gari husika iliozama baharini na ndio maana serikali ikamzuia kutoa habari ya ukweli.

“Yeye ni mtaalamu na alijua sababu gani alisema anaweza kupata miili hiyo ndani ya masaa mawili. Kuna uwezekano kuwa aliipata hiyo gari lakini akanyamazishwa kwa kuwa ingekuwa ni aibu kwa serikali, na ndiyo maana alilazimishwa kutofi - chua ukweli huo ili baadaye jeshi letu la wanamaji waweze kuonekana kwamba ni wao ndio wamepata hiyo gari halafu sifa zote ziende kwao,” alisema Gideon Lang’at kwenye mtandao wa Facebook.

Mwanahabari mmoja mzoefu wa Mombasa ambaye amekuwa akiripoti taarifa kuhusu operesheni hiyo pia alieleza fi kira kama hizo.

“Serikali wanadhani Wakenya ni wajinga. Itakuwaje sasa huyu Mswidi anatueleza changamoto zile zile ambazo kuanzia mwanzo vitengo husika vya serikali ndio vimekuwa vikisema zinaikwaza operesheni hiyo. Hapa kuna kitu, sio bure,” alitilia shaka mwaandishi huyo wa shirika moja kubwa la habari.

Mkenya mwengine naye alisema, “ Jeshi la wanamaji hawakutaka aibu, walimwambia ahusike lakini ole wake aseme ameona kitu.”

Mwishoni wa wiki iliyopita Mswidi huyo alipoongea na wanahabari akiwa ameanda mana na msemaji wa serikali Cyrus Oguna, aliomba msamaha kwa kuwapa watu moyo kwamba angeweza kufaulu, huku akisema kwamba kazi yenyewe ilikuwa ngumu mno kinyume na fikira zake za mwanzoni.

“Ndani ya bahari hakuna kabisa uwezo wa kuona chochote kwa kutumia macho halafu kuna kina kirefu sana mahala hapa,” alisema Volker Bassen, huku akiwasifu wanajeshi wanamaji kwa ushujaa na kujitolea kwao muhanga.

“Hawa wapiga mbizi wanahatarisha maisha yao. Hii ni operesheni ya kuopoa miili na sio ya kuokoa maisha na pengine ni wakati sasa wa kuzingatia hatari zilizopo (kwa wapiga mbizi),” alieleza mzungu huyo.

Ni kauli hii ambayo wengi hawajaiamini kuwa hali halisi ya mambo. “Hivyo ndivyo alivyoambiwa aseme,” alisema jamaa mmoja aitwaye Humphrey Karanja.

Wakenya wengine pia wamemsuta mzungu huyo kwa kile walichokiona kama kuwadanganya watu kwamba aliweza kufanya kazi ambayo haiwezi.

“Wakati mwengine usiingilie mambo mazito bila ya kufanya uchunguzi wa kutosha,” alisema Brian Ambuyo. Daniel Masinde naye alitamka kuwa huyo Mswidi yuafaa kukamatwa na kuweka ndani kwa kuchezea Wakenya shere.