Alhamisi ya wiki iliyopita iliadhimisha miaka 41 tangu kifo cha baba wa taifa hayati Mzee Jomo Kenyatta, ambaye alifariki Agosti tarehe 22 mwaka wa 1978 katika jimbo la pwani.
Ikizingatiwa kwamba Mzee Kenyatta aliaga dunia akiwa pwani, pengine ni kama sadfa kwamba kwa muda mrefu pia kumekuwa na dhana na imani baina ya Wamijikenda kwamba baba wa taifa huyo alikuwa mzaliwa asili wa pwani.
Pengine huenda nadharia hii ni imani tu kwa kuwa hakuna ukweli hasa wa kuthibitika pasipo shaka, japo hata hivyo wahenga walinena kwamba ‘lisemwalo (huenda ikawa) lipo.’
Kwa kifupi tu ni kwamba baina ya Wadigo, kabila la Wamijikenda lililopo eneo la pwani kusini, kumekuwa na imani kuwa Mzee Kenyatta, ambaye ndiye baba mzazi wa rais Uhuru Kenyatta, alizaliwa na wazazi Wadigo huko pwani kusini.
READ MORE
Real 'dynasties' have come back together, can fresh 'hustlers' voice emerge?
First-term curse: Why every new president faces a crisis right after being sworn-in
National Treasury explores PPP models for mega projects after Adani Group exit
Ruto banks on Kinyanjui to win crucial Nakuru vote bloc in 2027
Ieleweke kuwa dhana hii, pasi na ukosefu wa ushahidi thabiti, imedumu kwa miaka mingi sana na hivyo basi simulizi yake imepokezwa kutoka kizazi kimoja hadi chengine.
Hivyo basi maneno haya yamekuwa yakisemwa wazi wazi na kwa wakereketwa wanaotaka kuulizia suala hii huwa sio vigumu kupatana na maelezo yake.
Kwa mujibu wa simulizi yenyewe, inadaiwa kwamba eti Mzee Jomo Kenyatta alizaliwa na wazazi Wadigo lakini baadaye walilazimika kumtupa mwana wao kwa kuwa kulingana na mila na tamaduni za wakati huo, mtoto huyo alionekana kuwa ‘kisirani’ na alifaa kutupiliwa mbali.
Ieleweke pia hata hivyo simulizi hizi hazijaweza kunyoosha kidole hasa ni katika familia gani alikozaliwa Mzee Kenyatta bali vyanzo tofauti tofauti huashiria kuwa alizaliwa aidha sehemu ya Ng’ombeni, wengine wakidai ni Waa, Tiwi ama sehemu ya Denyenye.
Japo cha kufurahisha ni kwamba sehemu hizi zote zinazo tajwa ziko katika eneo bunge la Matuga, kaunti ya Kwale.
Pambazuko ilipo lizamia suala hili iliweza kuongea na baadhi ya wazee Wadigo walokula chumvi na ambao walibainisha kuwepo kwa nadharia hiyo katika jamii ya Digo.
Kwa mfano mzee Juma Mwachuphi, mkazi wa Kiteje katika kijiji cha Mkumbi eneo bunge la Matuga na mwenye takriban umri wa miaka 90, alieleza jinsi alivyo pokezewa na wazee walio tangulia.
“Niliambiwa (Jomo Kenyatta) alizaliwa Digo na Wadigo lakini baada ya kuzaliwa alionekana ni kisirani kwa hivyo akatupwa,” asema mzee Mwachuphi.
“Alipotupwa wakatokea watu wakamchukua wakaenda naye bara. Lakini mpaka sasa watoto visirani wanazaliwa japo hawatupwi tena lakini hao (Wadigo) wa kale walikuwa wakiwatupa,” anaeleza.
Neno ‘kisirani’ linaelezwa kwenye kamusi ya Kiswahili Sanifu ya Oxford University kama 1. ‘hali inayoleta matokeo mabaya; ndege mbaya; nuksi’ na 2. ‘Mtu anayesababisha hali inayoleta matokeo mabaya; nuksi’.
Mzee Abdallah Mnyenze wa Muungano wa Wazee wa Kaya za Mijikenda na pia mwenyekiti wa Baraza la Wazee Pwani naye alifafanua kuwa kulingana na mila za Wadigo wa kitambo, mtoto aliyezaliwa na kuonekana kuwa kisira ni ilitokana na mtoto huyo kuonyesha alama ambazo zilitafsiriwa kama kituko ama kioja.
“Kwa mfano mtoto ambaye alizaliwa akiwa na meno ama alama fulani mwilini mwake zisizo za kawaida ndiyo alisemekana kama kisirani,” alieleza mzee Mnyenze.
Kigogo huyo wa wazee wa Mijikenda pia alibainisha kuwepo kwa nadharia hii inayoashiria kuwa usuli wa Jomo Kenyatta ni Digo.
“Inadhaniwa kuwa alizaliwa sehemu za Ng’ombeni,” alisema. Kulingana na mapokezi aliyopata mzee Juma Mwachuphi, yeye alielezwa kuwa Mzee Kenyatta alizaliwa sehemu za Denyenye.
Kwa mujibu wa imani hii kuhusu uzao wa baba wa taifa, watu ama mtu aliyemnusuru mtoto huyo mchanga aliyetupwa hatimaye alielekea na mwana huyo hadi kwao Ukikuyuni ambako ndiko alikolelewa mtoto huyo hadi akakua.
Kulingana na kumbukumbu zinazotambuliwa rasmi kihistoria kuhusu nasaba na maisha ya hayati Jomo Kenyatta, zinaeleza kuwa baba wa taifa alizaliwa huko Gatundu katika kauti ya Kiambu.
Baadhi ya wanahistoria wametofautiana kidogo kuhusu mwaka gani hasa aliozaliwa Mzee Kenyatta huku wengine wakitaja miaka tofauti baina ya 1891 hadi 1901, japo kumbukumbu nyingi zinaonekana kutaja 1891 kama mwaka aliozaliwa.
Kwa mujibu wa kumbukumbu hizi rasmi, wazazi wa Mzee Jomo Kenyatta walikuwa ni Muigai na Wambui. Akiwa mdogo hayati Kenyatta alibaatizwa kwa jina la John(ston) Kamau na kwamba babaake mzazi, Muigai, alifariki wakati Kenyatta bado alikuwa mdogo.
Jina la Jomo Kenyatta ni jina alojipatia yeye mwenyewe alipokuwa akifanya kazi Nairobi kwa baraza la mji wa Nairobi.
Historia yake pia inaeleza kwamba Mzee Kenyattta alijiunga na chuo cha wamishinari, Church of Scotland Mission takriban mwaka 1909 ambako alipata elimu yake ya mwanzoni.
Ukizingatia historia hii inayotambuliwa rasmi kama maelezo ya kuzaliwa na maisha yake ya udogoni, hivyo basi ni kizungumkuti kufafanua kitendawili cha kuwepo kwa dhana mbadala iliyodumu pwani kusini kwamba uzao asili wa Mzee Kenyatta ni Digo na wala sio Ukikuyuni.
Vile vile kuna baadhi ya mambo fulani kumhusu baba wa taifa Mzee Kenyatta ambayo yaonekana kutia nguvu nadharia hii ya Wadigo.
Kwa mfano jinsi Mzee alivyokuwa akiipenda ngoma ya kitamaduni ya Wadigo, yaani Sengenya. Kulingana na maelezo mengi kuhusu hili, inasemekana kwamba baba wa taifa hangezuru Mombasa ama pwani kusini wakati wowote bila ya kutaka kutumbuizwa na ngoma ya Sengenya.
Inaonekana aliienzi sana densi hiyo ya kitamaduni ya kidigo kiasi cha kwamba kutumbuizwa kwake ilikuwa sio kwa kuitazama tu bali alikuwa lazima ataishia kujimwaga uwanjani na kukatika vilivyo.
Halafu kuna rafi kize Mzee Kenyatta ambao walikuwa na uswahiba mkubwa mno karibu na udugu, kulingana na simulizi zinavyo elezwa.
Baadhi ya majina yanayotajwa ya marafi ki hawa ni kama vile mzee Bambaulo, Said Mwamgunga, Mbodze, Hamadi Darwesh, Bilashaka na wengineo.
Hata baadhi majina haya yamesalia kwenye kumbukumbu za kudumu kwa taasisi za elimu zilizopewa majina yao kama vile shule ya msingi ya Mwamgunga pamoja na shule ya msingi ya Bilashaka zilizoko eneo bunge la Matuga.
Kati ya swahiba hawa wa Jomo Kenyatta, marehemu mzee Bambaulo pia anatajwa sana na wengi kuwa mkaribu sana wa baba wa taifa.
Mzee Bambaulo alikuwa ni mkazi wa Waa na ambaye pia anasemekana kuwa mmoja kati ya Wadigo wa mwanzo kupata elimu ya Wazungu na hatimaye akawa mwalimu tajika.
Hata mwenyekiti wa Baraza la Wazee Pwani mzee Mnyenze anasema alikuwa mwanafunzi wa Bambaulo.
Inasemekana kwamba hakuna hata wakati mmoja Mzee Kenyatta angezuru pwani kusini bila ya kumtembelea rafi ki huyu wa dhati.
“Kenyatta alikuwa hatoki kwa Bambaulo,” asema mzee Juma Mwachuphi, akimaanisha kuwa rafi ki hao wawili walijumlisha muda mwingi sana pamoja.
Hadithi nyengine zasema kwamba mzee Bambaulo alikuwa mtu pekee aliyeweza kusimamisha msafara wa rais Jomo Kenyatta barabarani ili asalimiane na sahibu wake.
“Bambaulo alikuwa akisimama kati kati ya barabara msafara wa rais unapopita na ilikuwa lazima Kenyatta asimame na kuongea naye,” anaeleza chanzo chengine.
Ni urafi ki sampuli hii na wazee hawa wadigo ambao inaaminika ulitokana na marafi ki hao wote, akiwemo Mzee Kenyatta mwenyewe, kufahamu kwamba yeye alikuwa ‘mdigo mwenzao’.
Hata hivyo mbali na ufahamu huo, yaaminika kuwa haingewezekana ‘ukweli’ huo kusemwa wazi wazi kwani yeye alifahamika rasmi kama Mkikuyu na ingebakia kuwa namna hiyo. Bila shaka nadharia hii inazua maswali mengi ambayo majibu yake sahihi ni ngumu kupatikana.
Lakini pengine maswali mengine yakujiuliza ni, kama simulizi hii ya kumnasabisha Mzee Kenyatta na Wamijikenda haina ukweli wowote basi chanzo chake hasa ilikuwa ni nini? Na mbona dhana hii yaonekana kudumu zaidi ya miaka 41? Je familia ya rais Uhuru Kenyatta wanajua kuwepo kwa imani hii baina ya Wadigo?